Sasa ni dhahiri kuwa MSCL haifahamiki vizuri. Kwa mshangao mkubwa wafanyakazi wa MSCL tumeona taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alipohojiwa na Gazeti la JAMHURI wiki iliyopita akasema kuwa hakuna mali za MSCL zilizohamishiwa TPA, wanasema wafanyakazi wa MSCL katika taarifa yao kwa JAMHURI inayoendelea hapa chini.

Ifahamike kuwa TPA ilianza rasmi katika Maziwa Makuu yaani Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa mwaka 2006. Pia ifahamike kuwa MSCL iliundwa Mwaka 1999 (ikitengwa kutoka TRC ambako ilikuwa ni idara tangu enzi za EAC).

Kwa miaka takribani saba MSCL ilikuwa ikijiendesha kama kampuni ya umma  kwa kujitegemea ikiwa haipo chini ya TRC yaani tangu mwaka 1999 hadi 2006 na wakati huo wote Bandari zote katika Maziwa Makuu, meli, karakana, vinyakuzi, magari na trekta, majengo yote (ghala, stoo, ofisi, sehemu za kupumzikia abiria, sehemu za kutunzia mizigo) na vyelezo vya meli (viwili Ziwa Victoria na kimoja katika Ziwa Tanganyika) zikiwa chini ya MSCL na siyo TRC, kabla ya kuanzishwa TPA Mwaka 2006.

MSCL ilinyang’anywa Bandari, vyelezo vyote, majengo yote, baadhi ya magari, trekta, karakana na hata baadhi ya vipuri vya meli na vifaa vya uzamiaji (ikabaki na mzamiaji asiyekuwa na vitendea kazi), mali zote hizi ilipewa TPA mwaka 2006. MSCL ikabaki na meli tu, hata raslimali watu miongoni mwa waliokuwa MSCL walihamishiwa TPA na wengine wakabaki MSCL (hawa waliobaki MSCL ndio wanaoteseka na kudhalilika kwa maamuzi yaliyofanywa pasipokuzingatia kanuni na sheria za utumishi wa umma).

Wakati mabadiliko haya yakifanyika mwaka 2006, MSCL haikuwa chini ya TRC. Kwa hiyo siyo kweli kwamba kuna mgawanyo wa mali zilizotoka TRC kwenda TPA. Wafanyakazi na Watanzania wameshangazwa na kauli ya Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuliho wanahoji kauli yake kuwa MSCL haikunyang’anywa mali ililenga nini.

Baada ya kuhamishwa mali hizo uwezo wa MSCL kujiendesha ulipopungua. Uhamishaji wa mali ulisimamiwa na Serikali na ilitamkwa kuwa lengo lilikuwa ni maandalizi ya kuibinafsisha MSCL. Maelekezo ya Serikali kwa MSCL yalikuwa ni MSCL kujiendesha kwa kulipa mishahara kwa wafanyakazi, kugharamia matengenezo madogo ya meli, kuendesha ofisi na pia kukabili gharama zote za uendeshaji wa meli.

Serikali iliahidi kusimamia matengenezo yote makubwa ya meli (Major overhaul kwa Main engines na Generators). Jukumu hili lilitekelezwa kwenye meli moja tu (MV Umoja mwaka 2012/2013). Meli nyingine zote hazijatengenezwa kwa kiwango kinachositahili kwa vile Serikali haijawahi kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo hayo. MSCL imekuwa inalazimika kutengeneza kwa dharura meli zinapoharibika, lakini si matengenezo ya kiwango kwa ukosefu wa pesa za kutosha kukabili gharama hizo.

Inawezekana Katibu mkuu wa wizara hii hakuwa anaufahamu ukweli huu kwa vile ana muda mfupi tangu alipoteuliwa mwanzoni mwa mwaka huu, lakini wapo watendaji hapo wizarani wanaoifahamu MSCL vizuri. Na hao walishiriki kwa namna moja au nyingine kuidunisha hasa ofisi ya Mkurugenzi anayeisimamia Kampuni hii yaani Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira.

MSCL kuwekwa chini ya ofisi ya Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira ndiyo mzizi wa matatizo yote yanayoendelea hadi Kampuni kufikia katika hali iliyonayo leo. Haifahamiki ni kwa nini MSCL haikuachwa chini ya Mkurugenzi wa Usafirishaji wa Vyombo vya Majini baada ya kutoka TRC ilhali shughuli za kampuni hii ni za usafirishaji kwa njia ya maji.

Kuhusu wafanyakazi kuhusika na hujuma mpaka kufikia katika hali hii si kweli. Tunasema hii ni hoja ya kupikwa yenye lengo la kutaka kuficha ukweli. Wateule wa Mkurugenzi ndio wanaosimamia kwa uwazi na kwa kificho biashara na Kampuni kwa: Ku-supply mafuta kwenye meli na mwaka jana wamefanikisha uhamishaji wa bima za meli kutoka Shirika la Bima la Taifa kwenda kampuni binafsi ya Ndege Insurance (ni nani asiyejua kinachoendelea pale mtu/kampuni binafsi anapofanya biashara na taasisi za umma?).

Matokeo ya uhamishaji huo wa bima ni kuwa gharama ya bima kwenye meli za kampuni imepanda! Pia wameingiza kwenye bima vyombo ambavyo vina miaka karibu kumi vikiwa havifanyi kazi kinyume na maelekezo ya Bodi ya kampuni.

Bodi ilitoa maelekezo ya kulipia Bima meli zinazofanya kazi tu. Kitendo cha kuhamisha bima kutoka NIC kwenda Ndege Insurance kimeacha maswali mengi ambayo hayajapata majibu, kwani Menejimenti ya MSCL chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ilikiuka maelekezo ya Bodi ya kampuni na palikuwa na ulazima upi kuingiza katika bima vyombo ambavyo havifanyi kazi?

Wafanyakazi hawana tatizo na Katibu Mkuu wa Wizara kwani angalau yeye ameonyesha dhamira ya kuwa karibu na wafanyakazi kwa kufanya ziara na kuzungumza nao, lakini Mkurugenzi mwenye dhamana na Kampuni hajawahi hata mara moja kuzungumza na wafanyakazi!

Wanachopokea wafanyakazi kutoka kwa Mkurugenzi huyo kupitia kwa menejimenti ya Kampuni na wateule wake ni lugha za vitisho kama vile kufukuza kazi, kuhamisha vituo/vitengo vya kazi, kupunguza wafanyakazi na kutoa likizo bila malipo. Bodi ya Kampuni pia haijawahi kuzungumza na wafanyakazi angalau kuwapoza na kutoa picha ya kinachoendelea katika kipindi hiki kigumu ambapo wafanyakazi wana miezi mitano sasa hawajapata mishahara.

Mambo mengi na mipango mingi ya Serikali kuhusu MSCL kwa muda mrefu yamefanywa kuwa siri kubwa. Usiri huo umewaacha wanaostaafu katika hali ya mateso kwa kukosa stahiki zao za msingi na kwa ajili hiyo wanakabiliana na ugumu katika kufuatilia stahiki zao kwenye Kampuni na kwenye mifuko ya jamii.

Hali zao kiafya zimedhoofika na wengine wametangulia mbele ya haki bila kupata stahiki zao za utumishi. Hili limebainika baada ya miundo ya utumishi wa wafanyakazi wa MSCL kujulikana kuwa imebadilishwa kiujanja ujanja bila ridhaa yao!

Ndio maana wafanyakazi wamebaki kutojiuliza kama Kampuni ni mali ya umma au ni mali ya mtu binafsi? Inafahamika wazi kuwa meli za MSCL ni mali ya Serikali, lakini inashangaza kuona kuwa wafanyakazi waliopo wametolewa kwenye muundo rasmi wa utumishi wa umma!

Ni jambo la ajabu kwa meli za Serikali kukabidhiwa kwa watumishi wenye ajira zisizokuwa katika muundo wa watumishi wa umma na ni hatari kwa usalama wa vyombo, abiria na mali zinazosafirishwa kwenye meli wakati wafanyakazi kwenye vyombo hivyo wana matatizo lukuki ambayo hayajapata ufumbuzi. Swali linalozuka ni kuwa Serikali imekodisha meli zake kwa watu binafsi? Na kama ni hivyo, kwa utaratibu/mkataba upi?

Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga Billioni 50.5 kwa lengo la kuifufua MSCL lakini fedha hizo ni kwa ajili ya miradi ya ukarabati wa meli na ujenzi wa meli mpya tu, hakuna fungu la mishahara ya wafanyakazi!

Tunaiomba Serikali itafute ufumbuzi wa haraka kuhusu swala la mishahara ya wafanyakazi na ifanye mchakato wa haraka kuitoa Kampuni kwenye usimamizi wa Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira na kuiweka chini ya Mkurugenzi wa Usafirishaji wa Vyombo vya Majini kuondoa mizengwe, umwinyi na ukiritimba uliopo kwa sasa.

Hili litasaidia kuleta amani miongoni mwa wafanyakazi na kuepusha misuguano isiyokuwa ya lazima baina ya wafanyakazi na Serikali, lakini pia kurejesha imani kwa wananchi kwani sasa hawapati huduma za uhakika za vyombo vya umma katika maziwa makuu.

Ikumbukwe kuwa MSCL ndio Kampuni pekee nchini ambayo imekuwa ikitoa huduma ya kusafirisha maiti bure na pia inatoza nauli kwa gharama ndogo kwa abiria na inasafirisha mizigo kwa tozo nafuu, kwa mfano:

1.      Gunia moja la Parachichi lenye ujazo wa kilo 100, MSCL (pamoja na gharama za wabebaji na tozo za TPA) inatoza Sh 2,000/ ambapo kwenye magari ni Sh 10,000/;

2.      Tani 10 za mzigo wa ndizi (pamoja na gharama zote za wabebaji na tozo za TPA), MSCL inatoza Sh 350,000/ wakati kwenye magari ya mizigo ni Sh 800,000/, na;

3.      Tani 10 za mizigo ya kawaida (mixed goods), MSCL pamoja na gharama za wabebaji na tozo za TPA ni Sh 250,000/ wakati kwenye magari, mzigo huo unatozwa Sh 800,000/

Anayeumia katika kufidia gharama hizo ni mtumiaji wa mwisho, yaani mwananchi wa maisha ya chini tunaomba Serikali itusaidie.

Katika toleo la gazeti hili la JAMHURI wiki iliyopita, Katibu Mkuu Dk. Chamuliho amesema Serikali haijaitelekeza Kampuni ya MSCL kwani katiba bajeti ya mwaka 2016/2017 imetenga Sh bilioni 20 kwa ajili ya ukarabati wa meli ya MV Victoria na ana uhakika itaanza kazi ndani ya mwaka huu wa fedha, Sh bilioni 21 kama malipo ya awali kwa ajili ya ununuzi wa meli mpya, Sh bilioni 5.9 kwa ajili ya ukarabati wa MV Liemba ya Lake Tanganyika na Sh bilioni 3.6 kwa ajili ya ukarabati wa MV Butiama.

Amesema usafiri wa meli utaimarika hapa nchini na matatizo wanayopata wafanyakazi sasa yataisha baada ya ukaguzi wa hesabu kukamilika na hoja yao ikawasilishwa rasmi serikalini kwa hatua za utekelezaji. Hadi sasa usafiri wa meli katika Ziwa Victoria unasuasua na wengi wanaona kama Serikali imewatekeleza kutokana na meli karibu zote kutofanya kazi kwa sasa kwani wakazi wa Kanda ya Ziwa huo ndiyo ulikuwa usafiri wa kutegemewa kwa watu wengi.

1415 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!