Wafanyakazi mbalimbali nchini wameahidi kukisulubu Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu ujao (2015), ikiwa Serikali haitatengua Sheria mpya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge kabla ya kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni, pamoja na vipengele vingine, inafuta fao la kujitoa na hivyo kutaka wananchi waliostaafu au kuacha kazi kutopewa mafao yao kabla ya kufikisha umri wa miaka 55 au 60.

 

Fao la kujitoa linampa mwanachama wa mifuko ya jamii uhuru wa kuomba mafao yake wakati wowote, baada ya kuacha au kustaafu kazi serikalini, katika mashirika, taasisi na kampuni.

 

Wakizungumza na JAMHURI na wengine kutoa maoni yao katika mitandao tofauti ya kijamii, wafanyakazi mbalimbali wamesema sheria hiyo ni kandamizi kwa vile inawanyima wananchi uhuru wa kuchukua na kutumia fedha zao walizokuwa akikatwa kwenye mishahara wao.

 

Mwalimu aliyejitambulisha kwa jina la Moris, anasema, “Ukimlazimisha mtu asubiri mpaka afikishe umri wa miaka 55 wakati alikuwa anaweka akiba yake kwa kuidunduliza, itakuwa ni kumnyanyasa na ni kinyume cha haki za binadamu.”

 

Anaendelea; “Halafu hii kauli ya Mkurugenzi wa NSSF (Dk. Ramadhani Dau) kwamba nchi nyingine duniani hazina sheria ya fao la kujitoa. Sijui hafahamu kwamba hata sheria za nchi hazifanani, na inawezekana hajui pia mapokeo tulinayo huku Tanzania kuhusu madai ya mafao ya wastaafu.


Adha ambazo zimekuwa zikiwakumba wastaafu wakati wa kufuatilia na kudai mafao yao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na serikalini, wakiwa wameshazeeka ni miongoni mwa sababu zinazotolewa kupinga sheria hiyo mpya.


Mwalimu James Irenge, aliyemfundisha Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere, ni miongoni mwa wastaafu wanaotajwa kufariki wakiwa hawajalipwa mafao yao licha ya kuyadai kwa muda mrefu.


“Wabunge na Serikali kwa jumla waache kasumba ya kupitisha sheria zinazogusa haki na maslahi ya wananchi bila kuwashirikisha kwa kupata maoni yao. Unapoacha kuwashirikisha wadau husika ni sawa na kufanya hesabu ya moja jumlisha moja toa mbili ambayo jibu lake ni sifuri. Wewe unapitisha sheria ambayo kesho itapigiwa kelele!” Anasema Mwalimu Moris anayetaka Serikali ya CCM isionewe haya kuondolewa madarakani mwaka 2015 kama haitafuta sheria hiyo mpya.


Mfanyakazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Hosea, anasema sheria hiyo mpya itasababisha wastaafu na watu walioacha kazi kabla ya kufikisha umri wa miaka 55 kukosa fedha za kujigharimia matibabu, kulipa ada za watoto wao na mahitaji mengine muhimu.

“Hii ni dhuluma kwa mfanyakazi aliyechagua kuingia kwenye mfuko huu kwa masharti yaliyokuwapo kabla,” anasema Hosea.


Anaongeza kuwa ni fedheha kusikia viongozi wa Serikali yetu wanataka kutumia taratibu za nchi nyingine, kuendesha nchi yetu huku wakijua mazingira na sheria za nchi havifanani.

 

“Huyo Dk. Dau anachotaka kufanya ni ku-copy (mambo ya nchi nyingine) na  ku-pesti (paste) (kuyahamishia Tanzania). Lazima tufanye mambo yetu kulingana na mazingira tunamoishi. Kwani tunaishi Ulaya na Marekani?” Anahoji Hosea.


Dk. Dau anasema fao la kujitoa limeondolewa kuendana na mfumo wa kimataifa, kwani duniani kote hakuna hilo na kwamba hata Zanzibar na Kenya hakuna kitu kama hicho.


Alitoa tamko hilo wakati akihojiwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).


“Wabunge, wao miaka mitano tu wanachukua mafao yao, mbona wao hawasubiri miaka 55?” Anahoji mfanyakazi mwingine na kuongeza kuwa haoni sababu ya kuirejesha Serikali ya CCM madarakani mwaka 2015 kutokana na udhaifu iliouonesha katika kuhudumia wananchi.

 

“Kimsingi haiingii akilini kama ajira ya mfanyakazi itasitishwa akiwa na umri wa miaka 30 halafu asubiri miaka 25 ndipo apate mafao yake wakati umri wa Mtanzania kuishi ni miaka 47 kwa mwanaume na miaka 44 kwa mwanamke 44,” anasema Mwakalinga.

 

Kwa upande wake, Rais wa Muungano wa Wapigakura Tanzania (TANVU), Milton Lutabana, anaeleza kusikitishwa na kitendo cha Serikali kumpangia mwananchi muda wa kuchukua na kutumia fedha zake.


“Sasa hivi kwa kujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wastani wa mtu kuishi ni miaka 50 hadi 55. Sasa unapomwambia mtu kwamba adai fedha zake baada ya kufikisha umri wa miaka 55, maana yake ni kwamba adai akiwa marehemu au akiwa nani?” Anahoji Lutabana.


“Lakini sasa mimi ninafikiri huu ni muda mwafaka kwa Watanzania kuona kama kweli bado Serikali ya CCM inastahili kuendelea kuwa madarakani, katika mazingira haya ya kuzungusha na kunyanyasa wafanyakazi juu ya mafao yao,” anasema Lutabana.


Katibu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Kanda ya Ziwa, Ramadhani Mwendwa, anasema kitendo cha Serikali kupitisha sheria hiyo mpya kilitosha kuwa sababu ya kuiadhibu katika Uchaguzi Mkuu ujao, lakini akasema hilo linaweza lisifanikiwe kutokana na umaskini uliokithiri kwa wananchi wengi.


“Watu maskini, watu wenye njaa hawawezi kukwepa rushwa, lazima watapokea tu, hakuna mwenye njaa siku moja atasema anakwepa kitu, mwenye njaa hula kila kitu. Kwa hiyo hata kuwachagua viongozi kwa njia ya rushwa watachagua tu, wagombea wakitoa rushwa watapita tu kwa kupigiwa kura,” anasema.


Tayari wafanyakazi wakiwamo wa migodini wametaka Sheria mpya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) irudishwe bungeni kwenye mkutano unaoanza leo mjini Dodoma, irekebishwe kwa manufaa ya wafanyakazi waliostaafu na kuacha kazi.

 

Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholas Mgaya, ameitaka Serikali kufanya mabadiliko ya haraka kuhusu sheria hiyo au kuandaa utaratibu utakaohakikisha mwanachama atakayejitoa kutoka mifuko hiyo anapata haki yake kwa wakati.

 

Anasema TUCTA haitashindwa kuchukua hatua za kisheria kama SSRA itaendelea kushikilia msimamo wa matumizi ya sheria hiyo.

3897 Total Views 10 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!