Alhamisi ya January 10, 2013 kwangu imekuwa siku ya historia ya kipekee. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) lilinikabidhi jukumu la kuwasilisha maoni ya Wahariri kuhusiana na tunayotaka yawemo kwenye Katiba mpya.

Nawashukuru Wahariri kwa heshima ya pekee waliyonipa kufanya kazi hii na naamini niliifanya kwa ufanisi kutokana na pongezi ninazozidi kupata tangu siku ya kuwasilisha.


Kwa misingi ya uwazi, ingawa zimechapishwa habari na baadhi ya televisheni kutangaza kwa muhtasari tulichokiwasilisha, naomba kupita safu hii ya Sitanii, leo nakufikishia wewe msomaji wangu mapendekezo ya Wahariri.


Sitanii, Katiba ya sasa haitambui uhuru wa vyombo vya habari na wala hakuna hata neno moja lenye kutamka vyombo vya habari tangu ibara ya 1 hadi ya 152 ambayo ni ya mwisho. Kwa mantiki hiyo, tunakata Katiba mpya iwe na ibara tatu zifuatazo:- Uhuru wa Vyombo vya Habari (Freedom of the Press/Media), Haki ya Kupata Habari (Right to Information/Access to Information) na Uhuru wa Kutoa Mawazo (Freedom of Expression).


Yafuatayo ni mawazo niliyoyawasilisha kwenye Tume kwa niaba ya TEF na tunataka Katiba mpya iwe na ibara tatu zinazotamka hivi:-

1.0. Uhuru wa Vyombo vya Habari (Freedom And Independence Of The Press/Media)

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Jukwaa la Wahariri tunataka Katiba iwe na Ibara ifuatayo kuhusiana na Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa kutamka kwamba:-

1. (a) Katiba hii inahakikisha (guarantees) uwapo wa uhuru wa vyombo vya habari

(b) Milele Bunge halitatunga sheria yoyote yenye kudhibiti au kufisisha kwa njia yoyote iwayo uhuru wa vyombo vya habari

(c) Kwa Katiba hii na sheria nyingine yoyote isiyoendana na Katiba hii, milele haitaruhusiwa kudhibiti (censorship) habari nchini Tanzania

(d) Hakupaswi kuwapo vizuizi katika kuanzisha magazeti au vyombo vya habari binafsi

(e) Wahariri na Wachapishaji wa Magazeti na vyombo vingine vya habari hawapaswi kudhibitiwa au kuingiliwa na Serikali, na wala wasiadhibiwe au kusumbuliwa kutokana na mawazo, au maoni wanayotoa kupitia tahariri, au maudhui yaliyochapishwa/au kutangazwa na vyombo vyao.

(f) Mawakala wote wa vyombo vya habari wanapaswa, wakati wote, kutekeleza misingi, masharti na malengo ya Katiba hii, na wanapaswa kusimamia wajibu na uwajibikaji wa Serikali kwa watu wa Tanzania.

(h) Chombo chochote cha habari chenye wajibu wa kusambaza taarifa kwa jamii ambacho kinachapisha taarifa kuhusu au dhidi ya mtu yeyote kinawajibika kutoa fursa ya kuchapisha mawazo ya upande wa pili, ikiwa yapo, kutoka kwa mtu ambaye taarifa au chapisho linamhusu.

 

1.2. Vyombo vyote vya habari (Vya Umma na Binafsi) vinapaswa kutoa fursa sawa na kuwezesha uwasilishaji wa maoni na mawazo pinzani

•Masharti ya Ibara Ndogo ya 1 na 2 hapo juu (au ya Katiba hii kulingana na Ibara zitakavyopangiliwa) yatatekelezwa kulingana na sheria zitakazotungwa kwa kuongozwa na busara, bila kupingana na malengo ya msingi ya Katiba hii katika maeneo ya masilahi ya taifa kama; usalama wa taifa, utulivu na maadili ya umma na kwa nia ya kulinda heshima, haki na uhuru wa watu wengine.


•Kwa nia ya kuepusha mashaka, masharti ya ibara hii yasitumike kudhibiti haki za msingi za binadamu na uhuru unaotolewa na Katiba hii.


•Kutapaswa kuwapo Sheria ya Bunge ya Kuanzisha Baraza la Habari la Taifa, ndani ya miezi sita tangu siku ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, Baraza ambalo litakuwa na wajumbe kumi na watano kutoka taaluma mbalimbali. Makundi ya kitaaluma yanapaswa kutoa wajumbe kwa idadi ifuatayo:-

(a) Mwakilishi mmoja kutoka kila kundi;-

(i) Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania

(ii)  Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS);

(iii) Muungano wa Waandishi wa Vitabu

(iv) Muungano wa Maktaba

(v) Vyuo vya uandishi wa habari; na

(vi) vyama vya wafanyakazi;

(iii) Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

(b) Wawakilishi wawili kutoka katika kila kundi lifuatalo;-

(i) Vyama vya Wahariri

(ii) Vyama vya Waandishi wa Habari

(iii) Bunge la Tanzania; na

(iv) Makundi ya dini yanayotambulika;

 

•Baraza la Habari la Taifa litachagua Mwenyekiti wake

•Wajibu wa Baraza la Habari la Taifa ni;

•Kusimamia vyombo vya Habari

•Kuweka viwango vya kitaaluma kwa vyombo vya habari

•Kufuatilia utekelezaji wa viwango vilivyowekwa

•Kukuza taaluma na weledi katika vyombo vya habari

•Kusikiliza kwa njia ya maridhiano mashauri/malalamiko dhidi ya vyombo vya habari

•Gharama za uendeshaji wa Baraza la Taifa la Habari, ikiwa ni pamoja na mishahara, posho na malipo ya uzeeni yanayopaswa kulipwa kwa watu wanaotumikia katika Baraza yanapaswa kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina.

•Kwa mujibu wa Katiba hii, Baraza la Habari la Taifa ndicho kitakuwa chombo cha mwisho katika kusimamia tasnia ya habari nchini

2.0 Haki ya Kupata Habari (Right to Information/Access to Information)

2.1. Kila Mwananchi ana haki ya kupata —

(a) Taarifa zilizopo mikononi mwa Serikali;

(b) Taarifa zilizoko mikononi mwa mtu mwingine na zinahitajika kwa ajili ya utekelezaji au ulinzi wa haki yoyote na misingi ya uhuru; na

(c) Taarifa zilizoko mikononi mwa mtu au taasisi ikiwa taarifa hizo ni za lazima kwa utekelezaji au ulinzi wa masilahi ya jamii

2.2. Kila mtu anayo haki ya kufanya masahihisho au kufuta taarifa zisizo za kweli au za upotoshaji zinazomuathiri

2.3. Serikali inapaswa kuchapisha na kutangaza taarifa muhimu zinazolihusu taifa bila kushurutishwa.

3.0. Uhuru wa Kutoa Mawazo (Freedom of Expression)

3.1. Kila mtu ana haki ya Uhuru wa Kutoa Mawazo, unaohusisha—

(a) Uhuru wa kutafuta, kupokea au kutoa taarifa au mawazo;

(b) Uhuru wa ubunifu wa kisanii; na

(c) Uhuru wa kitaaluma na uhuru wa utafiti wa kisayansi

 

3.2. Haki ya Uhuru wa Kutoa Mawazo haitahusisha—

(a) propaganda kwa ajili ya vita;

(b) Uchochezi wa kuanzisha vurugu;

(c) Hotuba za Chuki; au

(d) Utetezi wa chuki inayochochea—

(i) ukabila, udini, ubaguzi kwa watu wengine au kuchochea mapambano; na

(ii) Mazingira yoyote ya ubaguzi yaliyoainishwa na kuzuiliwa na Katiba hii.

 

3.3. Katika kutekeleza Haki ya Kutoa Mawazo, kila mtu anapaswa kuheshimu haki na heshima ya watu wengine.


Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja maelezo haya tunaambatanisha nakala ya mapendekezo ya vifungu hivi katika lugha ya kiingereza.


Pia tunasisitiza kuwa tunaomba mapendekezo haya yapate ibara tatu ndani ya Katiba Mpya kwa kila moja kujitegemea katika eneo lake; Uhuru wa Vyombo vya Habari (Freedom of the Press/Media), Haki ya Kupata Habari (Right to Information/Access to Information) na Uhuru wa Kutoa Mawazo (Freedom of Expression).


Je, unayaonaje mapendekezo haya? Tuwasiliane.


1022 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!