madaraka1Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ziara nchini Uingereza hivi karibuni kuhudhuria mkutano wa viongozi wa dunia kujadili tatizo la rushwa. 

Tatizo la rushwa lipo katika kila pembe ya dunia na ni mojawapo ya matatizo ambayo Serikali ya Rais John Magufuli imekusudia kupambana nayo. Wengi wanasema ni tatizo ambalo haliwezi kwisha kamwe, na ni kauli ambayo si rahisi kupingana nayo.

Kwa waumini Wakristu, Biblia inasimulia kisa cha shetani kujaribu kumshawishi Yesu akubali mambo yake shetani ili Yesu aweze kutawala falme zote za dunia. Na si vibaya kujiuliza kuwa iwapo hata Yesu mwenyewe alikumbana na vishawishi vya rushwa, si kweli kuwa tatizo hili linashinda uwezo wa mwanadamu kulikabili? 

Kuota kuwa rushwa inaweza kwisha ni sawa sawa na kuamini kuwa maisha ya duniani yanaweza kuwepo bila dhambi. Lakini kukiri kuwa rushwa haiwezi kutoweka isiwe sababu ya kuacha kupambana nayo, kama ambavyo kuwapo kwa dhambi hakuwazuwii viongozi wa dini kuhubiri maisha yanayofuata maadili.

Mkutano wa London ulienda sambamba na mkutano wa wanamajumui wa Afrika ulioandaliwa Arusha, Mei 11, mwaka huu kujadili changamoto na mikakati ya kuwaunganisha wajasiriamali wa Afrika na wenye asili ya Afrika katika kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati yao, na kukabili changamoto zinazowakabili. Mojawapo ya changamoto zilizoainishwa ni tatizo la rushwa. 

Na swali la msingi lililoulizwa ni hili: wajasiriamali wanawezaje kutoa mchango wao wa kufikia malengo wanamajumui wa Afrika ndani ya mazingira ya jamii ambazo kwa kiasi kikubwa zimezoea na kukubali kuishi na rushwa?

Mojawapo ya maazimio yaliyotokana na mjadala juu ya rushwa ni uamuzi kuwa wajasiriamali wanaounga mkono malengo ya kuunganisha nguvu na umoja na ushirikiano wa wana wa Afrika na wale wenye asili ya Afrika kushikilia msimamo wa kutotoa rushwa katika shughuli zao. 

Unapozingatia mizizi iliyoshamiri ya rushwa ni uamuzi ambao utaonekana hautekelezeki na ambao mmoja wa washiriki wa mkutano wa Arusha alitahadharisha usiwe tu mojawapo ya milolongo ya maazimio mengi ambayo hutolewa kwenye mikutano ya aina hiyo bila kuwekewa mikakati thabiti ya utekelezaji.

Yapo matatizo mengi yaliyokabili jamii na ambayo yalionekana hayana ufumbuzi ambayo yalipata mikakati mipya kuyatatua kwa kupewa tu majina mapya. Pengine tatizo la rushwa nalo linapaswa kupewa jina Jipya. 

Ukimwi uliacha kuwa ugonjwa tu siku nyingi na kuitwa janga, na kwa kufanya hivyo mipango na mikakati ya kupambana na ugonjwa huu ikabadilika na kupata msukumo mkubwa zaidi. Kubadilisha jina la tatizo peke yake hakuondoi tatizo, bali kunabadilisha mtazamo wa wana jamii juu ya tatizo lenyewe na kuifanya jamii ifikirie na kuunda mikakati mbadala ya kupambana na tatizo lililopo mbele yake.

Kwa hiyo, katika ngazi ya mikakati, ipo haja ya rushwa kupewa mtazamo mpya ambao unaiinua kutoka tatizo ndani ya jamii, na kuwa hatari inayokabili jamii. Binadamu wengi, hasa wale wasioishi katika mazingira yenye nyoka huamini kila nyoka ana sumu, na jambo la kwanza watu wengi wanaokabiliana na nyoka wanalofanya ni kumuua nyoka aliye mbele yao. Kama uamuzi ni au maisha yangu au ya nyoka, basi uamuzi wa kwanza wa binadamu ni kulinda uhai wake na kutoa uhai wa nyoka. Labda rushwa inapaswa kutazamwa kwa misingi hiyo hiyo, kwamba inatishia uhai na ustawi wa jamii na inakuwa basi jukumu la kila mwanajamii kushika fimbo na kuiangamiza kila inapojitokeza.

Lazima kukiri kuwa ipo aina ya rushwa ambayo ni vigumu kupambana nayo, hata kufanya mikakati dhidi ya kuiondoa kuwa migumu. Ni vigumu kwa anayeombwa rushwa na daktari ili ndugu yake mgonjwa apate matibabu kuwa na uamuzi wa kukataa kutoa rushwa. 

Lakini wajasiriamali wanayo nguvu kubwa zaidi ya kuweka msimamo wa kukataa kutoa rushwa. Mara nyingi rushwa inatokana na uwezo wa rasilimali anazomiliki mjasiriamali, kwa hiyo akigoma kutoa rushwa, basi anakuwa ametumia silaha madhubuti ya kupunguza tatizo la rushwa.

Hata hivyo, mjasiriamali mmoja peke yake kuweka msimamo huo haitasaidia kupunguza kushamiri kwa rushwa dhidi ya wajasiriamali iwapo wenzake wataendelea kutoa rushwa. Mafanikio yatakuja tu iwapo jamii nzima ya wajasiriamali watakuwa na msimamo huo, na ndiyo jambo la msingi ambalo azimio mojawapo la mkutano wa Arusha linasisitiza. Wanamajumui wa Afrika wanatambua kuwa ipo nguvu kubwa katika umoja, hata katika kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa.

Sababu ya msingi iliyoleta mafanikio kwenye mapambano dhidi ya ukoloni kwenye nchi nyingi ni uamuzi wa wanajamii kuwa utaratibu wa nchi moja kuitawala nchi nyingine na kuwaweka wanaotawaliwa chini ya mfumo usioheshimu haki na utu wa watu wake kuwa ni suala ambalo halikubaliki. Uamuzi tu kuwa ni suala ambalo halikubaliki ni msukumo mkubwa katika kufanikisha mapambano dhidi yake. 

Ni kweli kuwa nchi inapokuwa imejikomboa dhidi ya ukoloni hutokea wakati mwingine kuwa viongozi wale wale ambao awali walikuwa viongozi mahiri dhidi ya ukoloni waligeuka- hao hao, kuwa viongozi mahiri wa kukumbatia na kuruhusu kushamiri kwa rushwa, ama kwa ushiriki wao moja kwa moja, au kwa kutochukua hatua madhubuti kupambana na tatizo la rushwa ndani ya nchi zao huru. 

Lakini msimamo ule ule wa kukataa ukoloni ni msimamo huo huo pia ambao unaweza kutumika kukataa viongozi wanaokumbatia au kuruhusu kushamiri kwa rushwa. Silaha muhimu ni uamuzi wa pamoja wa kukataa.

Uamuzi wa pamoja wa wajasiriamali kukataa rushwa hautamaliza rushwa ndani ya jamii, lakini ni silaha kubwa ambayo inaweza kupunguza rushwa kwa kiasi kikubwa.

By Jamhuri