Muhongo pasportWakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency), umekumbwa na kashfa baada ya kutoichunguza kampuni ya msambazaji wa mafuta ya Sahara Energy Resources Limited ya Nigeria.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kulikuwa na maelekezo ya kuchunguza chanzo cha kuchanganywa kwa mafuta ya ndege (JET A1) katika matangi kutoka kwa wakala huyo, ambayo baadaye yalikiukwa na uchunguzi haukufayika.

Kumekuwa na mkanganyiko wa taarifa kutoka kwa vyanzo mbalimbali kuhusu kilichotokea hasa kati ya kampuni ya Sahara Energy Resources Ltd na wapokeaji wa mafuta. Taarifa kutoka kwa vyanzo vyetu zinasema mafuta hayo yaliyoingizwa nchini Mei 4, mwaka huu yalikaguliwa na shirika la viwango nchini (TBS) na kuonekana yako safi.

“TBS walikagua mafuta hayo yakiwa bado katika meli na kuthibitisha kwamba yalikuwa na ubora unaostahili. Vilevile Mkaguzi mwingine binafsi alikagua na kutoka na majibu kwamba mafuta yalikuwa yanakidhi viwango kwa mujibu wa taratibu zilizopo pia,” kinasema chanzo chetu.

Akizungumza na JAMHURI, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa wakala huo, Michael Mjinja amekiri kuletwa kwa shehena hiyo ya mafuta Mei 4, mwaka huu na kushushwa mpaka Mei 8. Anasisitiza kwamba taratibu zote zilifuatwa, kwa maana ya mafuta kupimwa kama yanakidhi viwango kabla hayajashushwa kutoka katika meli.

“Ninakumbuka meli ile ilibeba shehena mbili za mafuta, moja ikiwa petroli na nyingine mafuta ya ndege… yalipimwa na hati zinazoonesha kwamba yalikidhi viwango zipo. Vivyo hivyo hata kampuni nyingine binafsi ilipima na kuthibitisha kwamba mafuta yalikidhi viwango,” anasema Mjinja.

Anasema, siku kadhaa baada ya mafuta kushushwa katika matangi ya TIPER, kampuni ya Puma ililalamika kwamba mafuta yalikuwa yamechanganywa. Yaani petroli na mafuta ya ndege. Mjinja anasema baada ya kufuatilia ilibainika ni kweli.

“Tulichukua hatua za haraka za kumtaka (Sahara Energy) aondoshe mafuta katika matangi ya TIPER pamoja na kusafisha mabomba ya mafuta. Alifanya hivyo kama tulivyoelekeza. Huku tukiwaomba wahusika waseme wamepata hasara kiasi gani, jambo ambalo halijafanyika mpaka sasa,” anasema Mjinja.

Mwezi Mei, mwaka huu Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliiagiza kampuni hiyo ya Sahara Energy Resources Limited kuhakikisha inasafisha matangi pamoja na mabomba ya mafuta na kuagiza kuwa endapo isingetekeleza agizo hilo ingekuwa mwisho wa kampuni hiyo kufanya kazi nchini.

Prof. Muhongo alinukuliwa bungeni akisema, kampuni hiyo haitakiwi kupewa zabuni nyingine hadi hapo uchunguzi utakapokamilika wa kubaini ukweli wa mafuta hayo kuchafuka kwa kuchanganyika na petroli.

“Sisi tulichofanya ni kuwasikiliza hao wapokeaji wa mafuta (receivers). Sisi tulichokifanya ni kuondoa usitishaji [wa kuagiza mafuta] kutokana na kutofanyika kwa uchunguzi kama ilivyoelekezwa na wapokeaji wa mafuta,” anasema Mjinja.

Kaimu Mkurugenzi huyo anasema, wapokeaji wa mafuta wanasema hawataki uchunguzi huru ufanyike kama ambavyo ilipendekezwa na Waziri dhidi ya Sahara Energy Resources Ltd. “Sijui kwa nini hao receivers wamekataa uchunguzi usifanyike…walichosema ile ripoti yao ambayo walitofautiana ibaki hivyo, hawataki independent team ichunguze,” amesema Mjinja.

Anasema katika timu ya uchunguzi ya kwanza, hata yeye Mjinja haelewi kwa nini hao wapokeaji wa mafuta wameamua kukataa uchunguzi huru usifanyike. Anasema kwa mtazamo wake wapokeaji wa mafuta wanaonekana kuipinga kampuni ya Sahara Energy Resources Ltd, hivyo wanajaribu kukwepa uwajibikaji wa mafuta yale yaliyochanganywa.

“Baada ya kusema uchunguzi hautakiwi tena sisi tukaondoa hilo zuio, na tukawaandikia hao wapokeaji wa mafuta watuletee gharama zote ambazo zipo… nia ni tujue gharama kiasi gani, zipi zimelipwa na zipi hazijalipwa. Mkataba wetu unasema watakwenda kwenye usuluhishi… ambao unaweza kuchukua muda mrefu zaidi, wakati wengine wanasema kwamba wapewe muda zaidi wa kukokotoa gharama,” anasema Mjinja.

Mjinja anasema, wakala wake utawaandikia barua hao wapokeaji wa mafuta kuleta gharama ambazo wamezitumia katika sakata zima la mafuta yaliyochanganywa. Anasema hakuna kanuni ambazo zinambana mkandarasi anayeleta mafuta nchini endapo linajitokeza tatizo kama hilo.

“Tunafikiria kubadili kanuni ili ziweze kuwabana wazabuni… ndio hivyo tunaendelea kujifunza maana sisi ni wapya katika utaratibu huu. Nilikuwa namuomba Mungu, Sahara Energy Resources Ltd asiende kwenye usuluhishi maana hatuna kanuni ambazo zinaelekeza tumsimamishe ili kupisha uchunguzi. Ninashukuru kwamba jambo hilo halikufikishwa huko kwenye usuluhishi,” anasema Mjinja.

Mjinja hakuwa na jibu sahihi alipoulizwa iwapo anafanya kazi kwa kufuata maelekezo ya wapokeaji wa mafuta au Serikali iliyotoa maagizo kupitia kwa Waziri Prof. Muhongo.

Kampuni ya Sahara sasa imepewa zabuni nyingine kuangiza mafuta ya kuingiza nchini bila kufahamika nini kilitokea hadi mafuta ya ndege yakachanganyikana na petrol, suala ambalo vyanzo vyetu vinasema ni la hatari na huenda lina msukumo wa utovu wa maadili nyuma yake.

2189 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!