Na Khalif Mwenyeheri

 

Ikiwa ni takriban mechi nne zimechezwa tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), hivyo kila timu ikiwa imecheza jumla ya mechi 22, huu ndio wakati ambao bodi za klabu zinazoshiriki ligi hiyo uvumilivu huwashinda.

Presha inakwenda hadi kwa mashabiki ambao hawatamani kuona timu zao zikishuka daraja, maana zikishuka kurejea ligi kuu ni ‘balaa’.

Timu kama Aston Villa, Leeds United, Nottingham Forest, Portsmouth tangu washuke daraja ni kama wamesahaulika kwenye dunia ya soka.

Ligi Daraja la Kwanza nchini Uingereza inasemekana ni moja ya ligi ngumu barani Ulaya na yenye ushindani, licha ya uwekezaji mkubwa kwenye timu, bado timu ikishuka daraja kurudi ligi kuu si kazi rahisi.

Timu kama QPR iliposhuka daraja mpaka leo imebaki stori. Aston Villa vilevile, licha ya uwekezaji mkubwa unaofanywa kwenye timu hizo.

Baada ya kuwa na matokeo ya kusuasua, Bodi ya Klabu ya Manchester United ilifanya uamuzi wa kumtimua kocha, Jose Mourinho, ili timu yao ibaki katika nafasi nne za juu, hadi hivi sasa wameshinda zaidi ya mechi tano mfululizo chini ya Ole Solskjaer.

Klabu ya Fulham ambayo kwa hakika inahitaji muujiza kubaki ligi kuu, wakamtimua Meneja Slavisa Jokanovic, ambaye aliipandisha timu hiyo daraja, nafasi yake ikachukuliwa na Claudio Ranieri.

Bado timu hiyo ipo nafasi ya pili kutoka mwisho, hali hiyo inawaweka baadhi ya makocha matumbo joto kutokana na timu zao kuwa mkiani katika msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Makocha wa klabu za Southampton, Cardiff City, Newcastle United, Fulham na Huddersfield wapo hatarini kupoteza  vibarua vyao muda wowote kuanzia hivi sasa.

Kwa kipindi hiki timu zinatafuta nafasi nzuri ya kukaa katika msimamo wa ligi, kwani biashara ni asubuhi na jioni mahesabu.

Hivyo kusajili wachezaji wanaoonekana ni wazuri wanaweza kuzisaidia timu ziendelee kubaki kwenye Ligi Kuu ya Uingereza ni muhimu kwa wakati huu.

Makocha wafuatao wana nafasi kubwa ya kuwa makocha kwa timu zinazoshika mkia katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Sam Allardyce (Big Sam)

Sam Allardyce kipindi hiki hutupiwa macho na wamiliki wengi wa timu ili kuzibakiza katika ligi kuu, kwani amekuwa mwenye bahati katika kuhakikisha anazitoa timu mkiani na kuzibakiza katika ligi kuu, amefanikiwa katika misimu mitatu.

Msimu wa kwanza ni msimu wa mwaka 2015/2016, katika mzunguko wa pili wa ligi ya Uingereza baada ya Gus Poyet, kuvurunda Big Sam aliikuta timu mkiani akaisaidia kubaki ligi kuu, msimu wa 2016/2017, baada ya kumaliza mzunguko akiwa wa 17 katika ligi.

 Crystal Palace ilimtimua Frank de Boer na mabosi wa klabu hiyo wakaamua kumpa nafasi Big Sam na aliitoa timu hiyo mkiani mwa ligi ya Uingereza, hivyo ana nafasi kubwa ya kupewa klabu zilizopo mkiani mwa ligi ya Uingereza.

Mwaka 2017/2018 alifanikwa kuirudisha Everton katika nafasi nzuri ya ligi kabla ya kujiuzulu na timu yake kuchukuliwa na Marco Silva.

Jose Mourinho

(The Special One)

Licha ya kufungiwa virago na ‘Mashetani Wekundu’, lakini usishangae kuona Jose Mourinho amekabidhiwa  kuinoa timu yoyote pale Uingereza, hususan zile zilizopo mkiani, kwani ana mbinu za ushindi na ni miongoni mwa makocha wenye mafanikio na uzoefu wa ligi kuu.

Allan Pardew, ambaye ni miongoni mwa makocha waliowahi kutamba katika Ligi Kuu ya Uingereza akiwa na Klabu ya Newcastle United, vilevile ni miongoni mwa makocha wanaoweza kupewa nafasi.

By Jamhuri