Wakazi Dar kupata maji zaidi

Na Mwandishi Wetu

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam na Pwani (Dawasa), Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Davis Mwamunyange, amewatoa hofu wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Pwani kuhusu upatikanaji wa huduma ya maji.

Akizungumza na wanahabari baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea miradi ya majisafi kwa ajili ya kujionea maendeleo ya miradi hiyo, Jenerali Mwamunyange amesema kukamilika kwa mradi huo kwa kiasi kikubwa kutapunguza adha ya maji kwa baadhi ya maeneo kama si kumaliza kabisa tatizo la maji.
Miongoni mwa maeneo ya mradi aliyoyatembelea ni pamoja na mfumo wa maji uliopo Bunju, mfumo wa maji Salasala, mfumo wa maji Makongo na Changanyikeni pamoja na kutembelea matanki ya kuhifadhia maji katika maeneo ya Madale, Goba na Kibamba.

Jenerali Mwamunyange akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi ya Dawasa, Mhandisi Gaudence Aksante, pamoja na mwenyeji wao, Ofisa Mtendaji Mkuu, Mhandisi Cyprian Luhemeja, ameonyesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huku akiwataka makandarasi kukamilisha miradi hiyo kama walivyokubaliana.
“Ziara hii imekuwa fursa nzuri sana kwangu kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Dawasa, nimeweza kujionea mwenyewe hali halisi ya mradi huu na namna mradi huu utakavyoongeza kiwango cha upatikanaji wa maji jijini Dar es Salaam,” amesema Jenerali Mwamunyange.

“Hatua iliyofikiwa ni nzuri, inatia moyo na wananchi wawe na matumaini makubwa kwamba sasa huduma ya maji itakuwa bora zaidi baada ya kukamilika kwa mradi huu, kasi ya makandarasi sasa hivi inaridhisha baada ya hatua kuchukuliwa na mamlaka kuwahimiza kwa kushirikiana na wizara,” amesema Jenerali Mwamunyange.
Amesema licha ya changamoto walizoeleza awali zilizochangia kupungua kwa kasi ya ujenzi wa mradi huo, tayari changamoto zimetatuliwa  na sasa wanaendelea vizuri na kwamba kwa kasi iliyopo wataweza kumaliza mradi mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza huduma ya upatikanaji wa maji ambapo watu milioni moja wanatarajiwa kufikiwa na huduma hiyo.
Amesema mradi huo ukianza hali ya mivujo ya maji iliyopo kwa baadhi ya maeneo itapungua kwa sababu maji yatakwenda kwa watu na kwamba awali tatizo lililokuwepo ni kwamba maji yalikuwa ni mengi lakini mtandao wa maji ni mdogo, kwa sasa matumizi yataongezeka.

“Tatizo la wizi wa maji tumeliwekea mkakati ambao utahakikisha linakwisha, kwa sababu wizi wa maji ulikuwepo kutokana na kukosekana kwa maji, lakini sasa huduma ya maji ipo na tayari tumeanza kuwaunganishia wananchi maji kwa mkopo, hivyo wajitokeze tu kuomba kuunganishiwa huduma ya maji,” amesema Mhandisi Luhemeja.