Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mara inaendesha uchunguzi dhidi ya mataeli ambao wamewakopesha watumishi wa umma fedha kwa riba kubwa na kuzalisha mafia yanayofikia Sh bilioni 1.3.

Mkuu wa Takukuru Mkoani Mara, Alex Kuhanda ameliambia JAMHURI kuwa fedha hizo zilikopshwa kwa walimu kati ya mwaka 2017 na 2019.

Katika hatua nyingine, wiki chache baada ya kubainika kuwepo kwa watu wanaowakopesha watumishi wa umma kwa masharti magumu na kuwadhulumu fedha zao, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara inafenikiwa kuwarejeshea Sh milioni 204 watu waliokuwa wametapeliwa na wakopeshaji hao.

Aidha, Takukuru pia inawashikilia viongozi  nane wa vyama vya ushirika (AMCOS) za Nyamatare na Chaume Mesaga wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara, kwa tuhuma za ubadhirifu na wizi.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Alex Kuhanda, ameliambia JAMHURI kuwa fedha hizo zilikuwa zimeporwa isivyo halali na wakopeshaji hao ambao wanaendesha shughuli zao bila ya kuwa na vibali halali kutoka kwa taasisi husika.

Amebainisha kuwa wakopeshaji hao wamekuwa wakiwabambikiza watumishi mbalimbali riba kubwa kupita kiasi. Waathirika wakubwa wa mikopo hiyo ya mitaani wametajwa kuwa waliokuwa watumishi wa umma ambao wamestaafu, hasa walimu.

Uchunguzi wa Takukuru ulibaini mathalani kuwa kuna mtumishi aliyekopa kiasi cha Sh900,000, na kutakiwa kulipa Sh1,260,000 kwa riba ya asilimia 40, ambayo ipo juu kinyume cha sheria.

Hata hivyo, kutokana na kuchelewesha malipo hayo, mstaafu huyo alilazimika kulipa Sh12,500,000, malipo ambayo ni sawa na riba ya asilimia 1,388.

Mstaafu mwingine alikopa kiasi cha Sh milioni tano ili alipe Sh milioni saba, sawa na riba ya asilimia 40 lakini akajikuta akilipa Sh milioni 20 sawa na riba ya asilimia 300.

“Mtindo huu umeenea maeneo mengi na kiasi cha fedha ambacho hadi sasa tumefanikiwa kuokoa ni kama Sh milioni 32.5 hivi. Tumekamilisha taratibu za kuzirejesha fedha hizo kwa wahusika,: anasema Kuhanda.

Mahakama

Takukuru imebaini kuwa wakpeshaji hao matapeli wanatumia zaidi mahakama kama mbinu ya kuwabana watumishi wanaotaka kukopa.

Akifafanua, anasema wakppeshaji hao huenda mahakamani kufungua kesi ya madai pale mkopaji anaposhindwa kurejesha mkopo.

Taarifa zinathibitisha kuwapo kesi zaidi ya 80 za aina hiyo mkoani Mara, ambazo baadhi yake tayari zimeshatolewa uamuzi.

Kwa mujibu wa Kuhanda, Takukuru imepitia hukumu 41 za mkopeshaji mmoja ambaye alifungua kesi dhidi ya akidai walimu 41 aliowakopesha kiasi cha Sh52,926,000.

“Mkopo huo ulikuwa na riba ya asilimia 23 kwa hiyo alistahili kulipwa jumla ya Sh65,098,900 pamoja na riba. Riba pekee ni Sh12,172,900. Kitu cha ajabu, mkopeshaji huyu alifungua kesi kadhaa mahakamani,” Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Kuhanda ameeleza na kuongeza:

“Na katika hukumu 41 tulizopitia, mkopeshaji huyu aliiomba Mahakama iwaamuru wadeni wake wamlipe kiasi cha Sh194,924,041.”

Hiyo ni faida ya ziada ya Sh129,825,141, sawa na riba ya asilimia 245.3, ambapo Mahakama ilimpa ushindi mkopeshaji huyo.

Kuhanda amethibitisha kuwa baada ya kuhojiana na mkopeshaji huyo, alikiri kutokuwa na vibali vya Serikali vinavyompa uhalali wa kuendesha biashara hiyo.

Kuhanda amesema kuendelea kwa Mahakama kupokea kesi za namna hiyo kunazidisha hisia kuwa matapeli hao wanaitumia Mahakama kuendeleza wizi wao na kutakatisha fedha.

“Niziombe Mahakama zetu mkoani Mara na popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukataa kutumiwa na wezi hawa,” Kuhanda amepaza sauti.

Ameeleza kuwa Mahakama zinatakiwa kuliona suala hilo kama ni janga linalowaathiri wastaafu waliolitumikia taifa kwa uadilifu. Pia ni chanzo cha watumishi wa umma kuishi kwa madeni yasiyolipika na hivyo kuathiri utendaji kazi na malezi ya familia.

Kwa mwaka huu 2020, Taasisi hiyo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Mara, imefanikiwa kurejesha kwa raia Sh milioni 204 katika operesheni yake.

Kati ya fedha hizo, Sh milioni 61.3 ni zile walizokuwa wameporwa wastaafu wanne na wakopeshaji wasiokuwa na vibali kutoka mamlaka za Serikali.

Amcos

Kuhusu viongozi wanane wa AMCOS wanaokamatwa na Takukuru, Kuhanda amesema wamewekwa chini ya ulinzi kwa tuhuma za kufuja Sh milioni 18.8.

Kwa mujibu wa bosi huyo wa Takukuru, kiasi hicho cha fedha ni mali ya wakulima wa pamba msimu uliopita 2019. AMCOS hizo ni ya Nyamatare na Chaume Mesaga, Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.

Kuhanda amesema kuwa viongozi wa AMCOS ya Nyamatare wanatuhumiwa kufuja Sh milioni 13.2 na Chaume Mesaga Sh milioni 5.6.

Kukamatwa kwa viongozi hao kumefuatia agizo la Rais Dk. John Magufuli, alilolitoa Oktoba 2019, akiwa ziarani mkoani Lindi.

Kuhanda amesema baada ya kutiwa nguvuni, vingozi hao wamekubali kurejesha fedha hizo ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanzia wili iliyopita.

“Takukuru tunahakikisha wakulima waliouza mazao yao wanalipwa. Zoezi hili ni endelevu na viongozi wote wanaodaiwa kufuja fedha za wakulima wahakikishe wanalipa fedha hizo ifikiapo tarehe 21 Februari, 2020,” amesema Kuhanda.

Ufisadi mwingine

Katika hatua nyingine, Kuhanda aliliambia JAMHURI kuwa mwaka jana Takukuru Mkoani Mara ilibaini mkondo wa ufisadi aliouita utakatishaji fedha.

Katika malalamiko ya wastaafu 12 waliyoyapokea kwa kipindi cha robo mwaka 2019, inaonesha wastaafu hao 12 walikopa kwa viwango tofauti, jumla ya Sh19,990,000.

Ndani ya kati ya miezi sita na nane walitakiwa kulipa riba ya Sh143,837,750, sawa na asilimia 719.5.

“Ukiweka na deni mama, wastaafu hawa walilipa kiasi cha Sh163,827,750, sawa na riba ya asilimia 819.5 ya mkopo. Kwa mfano mstaafu mmoja ambaye wakati akisubiri mafao yake baada ya kustaafu, alikopa kiasi cha Sh milioni 17.4 na kutakiwa kulipa riba ya Sh milioni 88.6, sawa na asilimia 509.2 na kufanya deni zima kuwa Sh milioni 108,” alisisitiza katika taarifa yake. Tukio hilo lilishawahi kutipotiwa na JAMHURI.

Uchunguzi ulibaini kuwa, mstaafu mwingine aliyekopa Sh2,490,000 alitakiwa kulipa riba ya Sh22,510,000, ambayo ni sawa na asilimia 904.

Mwingine ni aliyekopa Sh2,100,000 na kutakiwa kulipa riba ya Sh31,000,000, ambayo ni sawa na asilimia 1,476. Mikopo hiyo ilikuwa ya muda wa miezi sita hadi minane.

1104 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!