Mbunge wa Morogoro Kusini, Prosper Mbena (CCM), ametajwa kuwa miongoni mwa walionufaika na mgao wa fedha zilizochotwa kwenye Akaunti ya Tergeta Escrow, JAMHURI limethibitishiwa.
Anatajwa kuwa miongoni mwa waliobeba fedha hizo kwenye magunia kutoka benki. Wakati wa mgao huo, Mbena alikuwa Katibu wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete. Alishika wadhifa huo kwa miaka saba kuanzia mwaka 2008 hadi 2015 alipoingia kwenye siasa.
Vyanzo vyetu vinasema Mbena ndiye aliyekuwa kiunganishi katika kuchukua fedha kutoka katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic yaliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (PAC), iliyoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (sasa ni Mbunge wa Kigoma Mjini), ilithibitisha pasi na shaka kwamba zilichukuliwa kwa kutumia magunia na viroba (sandarusi).

Kwa miaka yote majina ya waliochota fedha hizo yameendelea kuwa siri kubwa, ingawa kwa sasa tayari wameshaanza kujulikana.
Gari lenye namba za usajili za Ikulu linatajwa kutumiwa kwenye ukwapuaji huo uliosababisha mtikisiko mkubwa nchini.
“Kuna gari iliyokuwa ikitumiwa na waliokuja kuchukua fedha katika benki ya Stanbic, ilikuwa na namba ST 403A… Gari hilo lilibeba fedha mara mbili, yaani vilijazwa viroba likaondoka na kurejea tena kuchukua viroba vingine,” kimesema chanzo chetu.

Chanzo chetu kimemtaja, Albert Marwa, kuwa ni mmoja wa watu wa karibu waliokuwa wakimuunganisha mmiliki wa kampuni ya PAP, Harbinder Sethi Singh. Marwa ambaye ni mfanyabiashara na mtu mwenye uhusiano wa karibu na watu maarufu hapa nchini, kwa sasa anaishi Uingereza.
Marwa ndiye aliyemleta nchini Sethi, huku akitumia nafasi yake ya kufamiana na viongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne kujipenyeza na kufanikisha kuchotwa kwa mabilioni ya shilingi kutoka kwenye akaunti ya Escrow.
Mbena mwenyewe amekuwa hapatikani kuzungumzia sakata hili, licha ya JAMHURI kumtafuta mara kadhaa na hata kumwandikia ujumbe mfupi wa maandishi bila mafanikio.
Kutoka katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), taarifa zinasema jina la Mbena lipo kwenye orodha ya wanaohojiwa na maofisa wa taasisi hiyo.
“Hakuna shaka kuwa ameshahojiwa na huenda kwa siku chache zijazo akaunganishwa na watuhumiwa wengine,” kimesema chanzo chetu.
Mwishoni wa mwaka 2013 Mbena akiwa Katibu wa Rais alimwandikia aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina, aruhusu kutolewa kwa fedha kwenye akaunti ya Escrow, kama ilivyokuwa imeshauriwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati huo, Jaji Frederick Werema. Jaji Werema ni miongoni mwa waliojiuzulu kutokana na kashfa hiyo.
Mapema baada ya kuvuja kwa barua aliyoandika kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha; Ikulu ilitoa onyo kwa vyombo vya habari kuripoti matukio yaliyofanyiwa uchunguzi wa kina na yenye kufuata maadili na taaluma ya habari, badala ya kufanya kazi kwa kile ilichosema ‘kuongozwa na ushabiki.’

Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, ilipinga  kuhusishwa kwa Mbena katika kuingilia kwake mpango wa uchotwaji wa Sh bilioni 306 katika akaunti hiyo iliyoibua hoja nzito nchini kiasi cha Bunge kuingilia kati na kusababisha kujiuzulu kwa mawaziri kadhaa, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo; na Waziri wa Ardgi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Akaunti ya Escrow ilifunguliwa baada ya kutokea kwa mgogoro wa kimaslahi baina ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Tanesco.
Mtu mwingine anayetajwa kwenye sakata la kuhamisha fedha za Escrow ni Shabani Gurumo ambaye kwa wakati huo alikuwa Mnikulu.
Gurumo, alipohojiwa kwenye Baraza la Maadili, alikiri VIP Engineering and Marketing kumwingizia fedha kwenye akaunti yake kama ilivyoelezwa na shahidi wa upande wa malalamiko, Basilio Mwanakatwe.
Gurumo akakiri kuzipokea fedha alizopewa na Rugemalira na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi.
“Ningeweza kufanya hivyo bila kutumia fedha hizo (alizopewa na Rugemalira). Nina fedha zaidi ya hizo za Rugemalira,” alitamba Gurumo mbele ya Baraza hilo.
Alisema kila mfuko wa suruali aliyovaa umesheheni fedha, hivyo daima maishani mwake hapatwi na ukata kiasi cha kutegemea fedha za Rugemalira.
“Hapa nina fedha na huku nina fedha,” alisema Gurumo mbele ya Baraza hilo, huku akijipigapiga kwenye mifuko ya suruali aliyovaa.

Msaidizi wa Singh achekelea
Mmoja wa waliokuwa wasaidizi wa karibu wa Singh, Vasilios Tavlaridis, amezungumza na JAMHURI na kuonyesha kufurahishwa na namna ambavyo Serikali imemkamata na kumfikisha mtuhumiwa huyo kwenye vyombo vya sheria.
Tavlaridis, ambaye ni raia wa Ugiriki, anasema ni wakati mahsusi sasa kutumia muda huu kuibadili Tanzania kwa maslahi ya wanyonge, akiamini kuwa fursa kama hii huwa haijitokezi mara kwa mara.
“Mawazo yangu ni kwamba tunatakiwa kutumia jukwaa hili kwa ajili ya mabadiliko makubwa ili baadaye watu kama huyo Sethi (Singh) wasije kujitokeza kupitia mgongo wa uwekezaji wakati wanawaibia Watanzania.
“Watanzania wanahitaji kuona nchi yao ikisonga mbele, ili kizazi kijacho kinufaike na matunda mazuri ya nchi yao, masuala kama hiyo mikataba ya kitapeli ya uwekezaji katika sekta ya nishati inatakiwa kukomeshwa.
“Ninajaribu kuwafahamisha Transparency International pamoja na mashirika mengine ya kimataifa kwamba tayari Sethi anashikiliwa na mamlaka za Tanzania ili taarifa hiyo pia itangazwe kwenye vyombo vya habari nje Ulaya,” amesema.
Tavlaridis anasema ni wakati sasa vyombo vya dola vifuatilie kuhusu fedha za Sethi huko nje ya nchi, huku akisisitiza kwamba anafahamu baadhi ya maeneo ambako singasinga huyo ameficha fedha alizozipata kutokana na sakata la Escrow.
“Niko tayari kuja Tanzania kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwapatia ushahidi kuhusu Sethi,” amesema Tavlaridis.

BoT wamhusisha Mbena, Gurumo
Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilimkariri Katibu wa Rais, Mbena, akielekeza utoaji fedha ufanywe kama ilivyoshauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Hatua hiyo iliondoa minong’ono ya chini chini ya kwamba Ikulu ilibariki hatua za utoaji fedha hizo.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) alimtaja Mnikulu Gurumo, kwamba kwenye mgawo naye alipata Sh milioni 800.
Kwenye orodha mpya iliyotolewa walikuwamo baadhi ya watumishi wa umma ambao wangine ni wafanyakazi katika Wizara ya Nishati na Madini.
Viwango vya fedha zilizowekwa kwenye akaunti hizo vinashabihiana kwa makundi ya watu kadri mhusika (Rugemalira) alivyopanga. Awamu moja ya ugawaji fedha huo inaonyesha kuwa zilitumika Sh 3,314,850,000 ambazo zilisambaza kwa wahusika kwa siku moja.

Majina ya waliopewa fedha na Rugemalira na kiwango kikiwa kwenye mabano ni Evelyn Rugemalira (Sh 808,500,000), Alice Kemilembe Marco (Sh 80,850,000), Rashid Abdallah (Sh 80,850,000, Annuciater C. Bula (Sh 40, 425,000), Laureaan R. Malauri (Sh 40, 425,000), Theophillo Bwakea (Sh 161,700,000), Jesca James Rugemalira (Sh 808,500,000), na Steven Roman Urassa (161,700,000).
Wengine ni Michael Muhanuzi Lugaiya (Sh 80,850,000), Eric Sikujua Ng’maryo (Sh 80,850,000), Lucas Kusima Simon (Sh 40,425,000), Jerome Mushumbusi (Sh 808,500,000), Loicy Jeconia Appollo (Sh 80,850,000), Rweyongeza Alfred (Sh 40, 425,000), Gaudence Talemwa (Sh 40,425,000) na Manzelline aliyepewa Sh 80,850,000).
Watu Maarufu kwenye mgawo huo ni Balozi wa Heshima wa Botswana hapa nchini, Emmanuel ole Naiko (Sh 40, 425,000), Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka (Sh bilioni 1.6), Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh 40, 425,000), Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja (Sh 40,425,000), Waziri wa zamani na aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Katiba, Paul Kimiti (Sh 40,425,000), Mchungaji Alphonce Twimann (Sh 40,425,000), Askofu Method Kilaini (Sh 80, 850,000) na Askofu Eusebius Nzigirwa aliyepata Sh 40,425,000.
Kwenye orodha hiyo wamo majaji wawili-Aloysius Mujulizi (Sh 40.4) na Profesa Eudes Ruhangisa (Sh 404.2). Pia wamo Mtendaji Mkuu wa RITA, Philip Saliboko (Sh 40.2) na ofisa wake hapo RITA, Rugozobwa Theophil (323.4).

Ushiriki wa Ikulu
Hatua ya Ikulu kudai kwamba Katibu wa Rais, Mbena, hakuandika barua ya maelekezo ya kulipwa kwa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, kulizidi kuibua maswali juu ya usiri uliokuwa ukiendelea serikalini kuhusu kashfa hiyo.
Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilijaribu kumsafisha Mbena kutoka kwenye kashfa hiyo ambayo kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hatua zote za utoaji fedha hizo zilipelekwa kwa Waziri Mkuu na Rais.
Kipengele cha 7.0. cha utetezi huo wa BoT kinahusu ‘Ushauri wa kuujulisha uongozi wa nchi’.
Kinasema hivi: “Mnamo tarehe 24 Oktoba, 2013, BoT ilimuandikia PST [Katibu wa Hazina], ikimuomba kuchukua hatua kadhaa kuhusiana na malipo ya IPTL. Miongoni mwa mambo yaliyoshauriwa na BoT yalikuwa ni:
“(i) Kwamba ufungaji wa Escrow Account uzingatie kwamba mamlaka ya kufanya hivyo yako kwa Paymaster General;
“(ii) Kwamba, kwa kuzingatia unyeti wa suala hili na ukubwa wa malipo husika, Waziri wa Fedha apate fursa ya kuwajulisha Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu ili waeleze kama
wanaridhia au la; na
“(iii) Kwamba GoT [Serikali ya Tanzania] iombe kutolewa kwa kinga itakayoikinga GoT dhidi ya madai yanayoweza kujitokeza baada ya malipo hayo kufanyika.”
Maelezo hayo ya BoT yakaafafanuliwa na wafuatiliaji wa sakata la Escrow kwamba yanathibitisha ushirikishwaji wa viongozi wakuu kwenye utoaji fedha hizo.
Ofisa mmoja ndani ya BoT, aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema: “Ikulu haiwezi kuchomoka katika hili, pengine inataka kusema Mbena alishiriki yeye mwenyewe kama yeye bila kufuata utaratibu. Ikulu inataka kusema Mbena, ama alighushi barua, au hakuwashirikisha wakubwa kutoa maelezo hayo.”

Anasema BoT isingeweza kuchukua hatua kubwa ya kuruhusu utoaji fedha kama isingepata baraka kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Ikulu.
Kipengele cha 10.0 cha utetezi wa BoT kinahusu Kibali cha kuhamisha fedha kwenda IPTL.
Kinasema: Mnamo tarehe 14 Novemba, 2013, PST aliwasilisha kwa utekelezaji, maagizo ya Mheshimiwa Rais ambaye aliagiza kwamba “Maamuzi ya Mahakama Kuu yatekelezwe kama alivyoshauri AG”. Maagizo ya
Mheshimiwa Rais yaliwasilishwa kwa PST kwa barua ya tarehe 13 Novemba, 2013, na ilisainiwa na Katibu wa Rais, Bwana Prosper Mbena.”
Baada ya kupata maelekezo hayo, ndipo BoT ilipomwandikia PST, ikiomba muongozo kuhusiana na suala la madai ya TRA kuhusiana na VAT.
Barua hiyo iliandikwa Novemba 15, 2013, na nakala yake kupelekwa kwa AG.

Kilichozingatiwa na BoT ni kwamba madai ya kodi za
Serikali yanachukuliwa kama madai yenye umuhimu wa juu katika malipo yoyote.
Kwenye taarifa yake, BoT inasema: “Hata hivyo, BoT ilikwenda mbali kuhakikisha kwamba utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama, pamoja na Makubaliano ya kukabidhi fedha unapata baraka za wakuu wa nchi kama vile Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu.”
Rekodi za Bunge (Hansard) zinaonyesha kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliihusisha Ikulu moja kwa moja na uchotwaji wa fedha hizo, Sh bilioni 320 kutoka Tegeta Escrow.
Alimtaja Mnikulu Gurumo, kwamba ni miongoni mwa waliopata mgao wa Sh milioni zaidi ya 800.

Kafulila aibana Ikulu
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), wa wakati huo, David Kafulila, alisema jeuri ya vigogo wa Serikali kukataa kujiuzulu ulikuwa ni mtego kwa Rais Jakaya Kikwete.
Anasema ushahidi unaonyesha baadhi ya maofisa wa Ikulu wamehusika kwenye kashfa ya Escrow kwa kuchotewa mamilioni ya shilingi.
Anasema ni kwa sababu hiyo ya kuhusika kwao, ndio maana wahusika walikuwa wanapata jeuri kuona kuwa hawapo peke yao kwenye sakata hilo.
Alisema: “Rais anapaswa kusafisha kuanzia Ikulu ili kuipa ofisi yake uhalali kwani watendaji wake wasio waadilifu kama hawa wanaotakiwa kujiuzulu na kugoma.
“Viongozi wa CCM, kina Kinana, Mangula wametamka watu hao wachukuliwe hatua, Bunge nalo limetamka hilo, iweje Ikulu iwabebe, wananchi sasa mnatakiwa mpime wenyewe…”
Akasema Baraza la Mawaziri halikujulishwa zaidi ya kujadili suala hilo baada ya sakata hilo kutokea. Anasema huo ni ushahidi tosha kuwa Ikulu inahusika. Kwa mtazamo wake, kama Spika angekuwa makini, Serikali yote ingeanguka.
Alisema ripoti ya Takukuru juu ya IPTL iliyojaa jinai za wahusika kama ilivyofichwa ya mwaka 2000, haitatolewa hadharani.
“Ndiyo maana nasema hii siyo mara kwanza Ikulu kuficha ripoti za Takukuru kuhusu ufisadi wa IPTL, mwaka 2000 ilichunguza kuhusu vigogo waliohusika katika mkataba huu na namna rushwa ilivyotumika lakini haikutoka,” alisema.

Taarifa ya Benki ya Mkombozi
Baada ya sakata la Escrow kupamba moto, Benki ya Mkombozi iliyotumiwa kwenye mgao wa fedha hizo, ilitoa taarifa kwa umma. Taarifa hiyo ilikuwa:

Utangulizi
Taarifa hii inatolewa kwa umma kutokana na ripoti mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari mitandao ya kijamii na taarifa iliyotolewa kwenye mjadala katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
1. Ufunguzi wa akaunti ya VIP engineering and Marketing (VIP)
Kampuni ya VIP engineering and Marketing ni kampuni ambayo imesajiliwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania. Kampuni hii ilifungua akaunti katika benki ya biashara ya Mkombozi na hivyo kuwa moja kati ya wateja wa benki. Benki ilijiridhisha na ilizingatia taratibu zote za ufunguzi wa akaunti husika kwa kuzingatia sheria za nchi na kanuni zinazozitaka benki kupata nyaraka muhimu kutoka kwa mteja wakati wa ufunguzi wa akaunti hiyo.
Nyaraka hizo ni pamoja na kuwepo kwa cheti cha usajili wa kampuni, kanuni za kampuni, idhinisho la kampuni kumruhusu moja kati ya wanahisa wake kuendesha akaunti pamoja na picha na hati ya kusafiria ya mhusika wa kuendesha akaunti hiyo.

2.0 Mauzo ya hisa za VIP
Kampuni ya VIP ilileta mkataba kwenye benki ya Mkombozi wa mauziano ya hisa za asilimia 30 baina ya VIP na kampuni ya Pan Africa Power Solutions (PAP) ambazo inamiliki katika kampuni ya IPTL. Mkataba huo ulisainiwa tarehe 19 Ogasti, 2013. Bei ya asilimia 30 ya hisa hizo ilikuwa ni dola za Marekani milioni 75. Katika kifungu namba 2.4 cha mkataba wao kinaelekeza fedha za mauzo ya hisa zilipwe kwenye akaunti ya VIP iliyopo benki ya Mkombozi. Mkataba huo wa mauziano ya hisa baina ya kampuni hizi mbili ulitambuliwa na hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotolewa na Jaji J.H.K Utamwa tarehe 5 Septemba, 2013.

3. Mchakato wa kulipa kodi ya serikali
Benki ilitambua kwamba katika mauziano hayo ya hisa ni lazima kodi ya Serikali ilipwe na hivyo iliizishauri pande zote mbili kupeleka mkataba husika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufanyiwa makadirio ya kodi husika. Tarehe 20 Januari, 2014 TRA iliiandikia barua kampuni ya VIP na nakala ya barua hiyo kuletwa kwenye benki ya Mkombozi. Katika barua hiyo TRA iliitaarifu kampuni ya VIP kuwa makadirio ya kodi yatokanayo na mauzo ya hisa ni shilingi 38,186,584,322.00 ikiwa ni kodi ya mauzo ya hisa ya asilimia 30 za mauzo ya hisa kutoka VIP kwenda kwa PAP (Capital gains and stamp duty).
TRA pia iliiagiza benki ya Mkombozi kuhakikisha kuwa inalipa kodi hiyo kwa niaba ya VIP mara tu fedha zitakapoingia kwenye akaunti yake.
Malipo ya kodi ya shilingi 38,186,584,322.00 yalilipwa TRA kwenye akaunti 11120100 iliyopo katika Benki Kuu ya Tanzania na TRA ilikiri kupokea kodi hiyo kwa barua yake yenye kumbukumbu namba 3-4/100/100/223/4 ya tarehe 24 Januari, 2014.

4. Ufafanuzi wa mambo mbalimbali
4.1 Benki ya mkombozi kuhusika katika kusafisha fedha chafu
Fedha zote zilizoingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo kwenye benki ya Mkombozi zilitokana na mauziano ya hisa kati ya VIP na PAP kwa mkataba uliotambuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania. Chanzo cha malipo hayo ni kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya PAP iliyopo katika benki ya Stanbic na kuingizwa kwenye akaunti ya VIP iliyopo katika benki ya Mkombozi.
Fedha hizo zilihamishwa katika mafungu mawili. Fungu la kwanza ilikuwa ni shilingi 73,573,500,000.00 zilihamishwa kwa njia ya TISS kwa kumbukumbu namba 000000050720 ya tarehe 23 Januari, 2014 na fungu la pili ni dola za Kimarekani 22,000,000.00 zilihamishwa kwa TISS kwa kumbukumbu namba 000000050812 ya tarehe 23 Januari, 2014. Malipo mengine ya asilimia kumi ya mauzo ya hisa yalilipwa kwenye akaunti ya Mkombozi iliyopo Benki Kuu ya Tanzania. Kutokana na mchakato huo benki ya Mkombozi ilijiridhisha kuwa fedha hizo ni malipo halali na siyo fedha chafu.
Benki ya Mkombozi haijihusishi na utakasishaji wa fedha chafu na haramu katika uchumi wa Tanzania.
4.2 Malipo yatokanayo na akaunti ya VIP
Malipo toka kwenye akaunti ya mteja hufanywa kutokana na maelekezo ya mteja. Benki ikishajiridhisha kuwa fedha ya mteja ni halali na ipo kwa mujibu wa sheria na hamna zuio lolote toka katika mahakama hapa nchini hutekeleza malipo kwenye akaunti ya mteja kutokana na maelekezo yake.
Benki ilijiridhisha kuwa malipo yote yaliyofanywa kutoka kwenye akaunti ya VIP ni halali kwa kuwa chanzo cha pesa hizo ilikuwa ni halali kutokana na mauzo ya hisa na ulipwaji wa kodi ya Serikali kama ilinyoelezwa hapo juu. Kutokana na sababu hiyo benki haikuwa na shaka juu ya malipo hayo.
4.3 Malipo taslimu kwa wateja na kubeba fedha kwenye viroba, mifuko ya rambo na magunia
Benki inatoa tamko kuwa malipo yote yaliyofanywa katika akaunti ya VIP yalilipwa kupitia akaunti za walipwaji. Hakuna fedha zilizolipwa taslimu kwa wateja na kubebwa kwenye viroba au magunia kama ilivyoripotiwa Bungeni. Pesa iliyotoka kwenye akaunti ya VIP tarehe 6 Februari, 2014 kiasi cha shilingi 3,314,850,000.00 ililipwa kwenye akaunti nane za wateja tofauti na siyo kubebwa kwenye viroba au magunia.
Na zile zilizotoka toka benki ya Stanbic zilizotajwa hapo juu zilitumwa kwa njia ya TISS na siyo kubeba kwenye magunia au viroba.
4.4 Malipo kwa mfanyakazi wa benki ya Mkombozi
Gazeti la Mawio la tarehe 20-26, Novemba, 2014 toleo namba 0122 liliandika kuwa mwanasheria wa benki ya Mkombozi ajulikanaye kwa jina la Rweyengeza Alfred alipokea malipo toka akaunti ya VIP ya shilingi milioni 40.2.
Benki inatoa tamko kuwa haina mfanyakazi anayetambuliwa kwa jina hilo na wala hakuna mfanyakazi yeyote wa benki aliyelipwa fedha toka kwenye akaunti ya VIP.

Wito kwa umma
Benki ya Mkombozi inachukua fursa hii kuwatarifu wateja wake na umma kutopotoshwa na taarifa au tuhuma zilizofafanuliwa hapo juu na kuwataka wateja wake wote kutokuwa na hofu yeyote kwani benki ipo imara na inafanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na Benki Kuu ya Tanzania. Benki inawataarifu wateja wake na Watanzania kwa ujumla kutoyumbishwa na tuhuma hizo ambazo hazina ukweli ndani yake na badala yake waitumie benki yao kwa shughuli za maendeleo ya nchi yetu.
Pamoja tunajenga nchi na uchumi wa nchi yetu.
Hitimisho
Benki ya biashara ya Mkombozi haijihusishi na haitajihusisha na utakatishaji wa fedha chafu.

1474 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!