Katika kukomesha vitendo vya hujuma zinazofanywa na watendaji kwa wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, amemwagiza Mkuu wa Polisi wilayani, Madaraka Majiga, kuwakamata watumishi wa Idara ya Kilimo waliosambaza mbegu mbovu za mahindi kwa wakulina na hivyo kuwasababishia hasara.

Wakati Gambo akitoa agizo hilo, wadau wa maendeleo wa wilaya hiyo wamepongeza dhamira ya kiongozi huyo kuanza kuisafisha Korogwe.

Wakizungumza na JAMHURI wilayani hapa hivi karibuni, baadhi ya wananchi wamesema Gambo amekuwa kiongozi makini na mfuatiliaji wa mambo na amenusuru kuibwa kwa Sh milioni 79 kutoka Benki ya NMB, kitendo ambacho kiliwahusisha watumishi Halmashauri ya Wilaya hiyo ambao tayari wameshafikishwa mahakamani.

Gambo amelitaka Jeshi la Polisi wilayani Korogwe kufanya uchunguzi kuanzia Ofisi ya Kilimo, mawakala na kwa wote waliohusika kusambaza mbegu mbovu kwa wakulima ili wafikishwe mahakamani kabla ya Julai 15, mwaka huu.

Sakata hilo la wakulima kugawiwa mbegu mbovu limejitokeza katika vijiji mbalimbali vikiwamo vya Kerenge, Kwamazandu na Kwashemshi, ambapo wakulima wamekuwa wakilalamika kugawiwa mbegu zilizooza ambazo zimekuwa hazioti, na hivyo kuwasababishia hasara wananchi hao.

Ili kuweza kudhibiti vitendo vya aina hiyo, mkuu huyo wa wilaya amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote waliohusika, ambapo kwa kuanzia wahusika watakamatwa na kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani sheria ichukue mkondo wake.

Mkuu huyo wa wilaya amewakemea pia watumishi wa Idara ya Kilimo waliokosa uadilifu kiasi cha kudiriki kuhujumu rasilimali za wananchi, kwa kuwasainisha pembejeo kwa utaratibu tofauti na maelekezo yaliyotolewa na serikali.

Kuhusu dhamira yake ya kuisafisha Wilaya ya Korogwe ambayo kwa muda mrefu imedaiwa kufanywa kama ‘shamba la bibi’, kiongozi huyo amesema kwamba katika kuwatumikia wananchi hatajali itikadi za siasa, dini, kabila wala rangi bali atafuata sheria, kanuni na taratibu kuwashughulikia watakaothibitika kuhujumu rasilimali za wananchi.

Ameongeza kuwa ili Korogwe iendelee kuwa salama, kuna haja ya watumishi, viongozi na wananchi kila mmoja kwa nafasi yake kuchukua nafasi yake katika uwajibikaji huku wakizingatia uzalendo na uadilifu wa hali ya juu katika masuala ya usimamizi na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.

Amesema ameamua kuongeza ufuatiliaji zaidi wa masuala yanayohusu rasilimali za umma  baada ya kubaini kwamba baadhi ya watumishi wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea, huku kukiwa na tatizo la udhaifu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo na kusababisha kero kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Gambo amepiga marufuku vitendo vya watendaji  kuingia mikataba holela bila ya kuwashirikisha wanasheria na wananchi husika, kwani vimekuwa vikisababisha kero kwa wananchi na kuwafanya wakose imani na serikali yao.

Pia amepiga marufuku kuendelea kwa matumizi ya fedha kiasi cha Sh 220 za mmojawapo wa miradi ya kilimo cha umwagiliaji wilayani hapa.

Gambo amezuia matumizi ya fedha hizo baada ya kutilia shaka matumizi ya awali na wahusika kushindwa kutoa majibu yanayojitosheleza.

By Jamhuri