DODOMA
EDITHA MAJURA
Shule ya Msingi Nzuguni ‘B’ ya mkoani Dodoma, inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya
madarasa hivyo kuwalazimu wanafunzi kusoma kwa zamu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo, ndiye mlezi
wa shule hiyo yenye wanafunzi 2,402, madarasa tisa na matundu manane ya vyoo.
Uchunguzi wa JAMHURI, umebaini kuwa ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vyumba
vya madarasa, wanafunzi wanaingia darasani kwa kupokezana kwa awamu mbili.
Pamoja na hilo, wakati mwingine wanalazimika kufundishiwa nje, chini ya miti na ubao
uliotengenezwa katika hali inayowezesha kuuhamisha kwa urahisi.
Afisa Elimu wa Wilaya ya Dodoma, Misungwi Kigosi, amesema changamoto ya upungufu wa
vyumba vya madarasa mjini humo ipo karibu kwa shule zote wilayani humo.
Amesema kutokana na hali hiyo, imeelezwa wanafunzi kuingia darasani kwa zamu na kufanyika
ujenzi wa madarasa chini ya viongozi wa mitaa na kata.
Mbali na upungufu wa madarasa, wanafunzi wa shule hususani wanaotokea mtaa wa Nzuguni
‘C’ wanakabiliwa na hatari ya kufa maji wanapovuka kwenye korongo linalotenganisha eneo hilo
na Nzuguni ‘B’ ilipo shule yao.
Mara kadhaa, wazazi na walezi wa wanafunzi hao wanawazuia watoto kwenda shule ama
kurudi nyumbani nyakati za mvua kubwa.
Mratibu wa Elimu wa kata hiyo, Sospeter Ramadhan, amethibitisha kuwapo changamoto hiyo
na kusema wameishaishirikisha Serikali ya Mtaa wa Nzuguni ‘C’ ili watenge eneo kwa ajili ya
ujenzi wa shule.
Kigosi amethibitisha kufahamu adha wanayoipata wanafunzi wa Nzuguni ‘B’ na kwamba
amewahi kushiriki kuvusha watoto kwenye daraja lililokuwa limefunikwa kwa maji wakati wa
mvua.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nzuguni ‘C’, Idrissa Bale, amesema wakazi wa mtaa
huo wameafikiana kutoa eneo walilopewa na Taasisi ya Kilimo Tanzania (TASO) mwaka 2009
kutumika kwa gulio, lakini sasa litawekezwa kwa ujenzi wa shule.
“Eneo ni kubwa, limezungushiwa uzio na linafaa kwa ujenzi, hata mwaka jana Mkurugenzi
Mtendaji, (Godwin Kunambi), alifika tukampeleka akalikagua na kuridhishwa,” amesema.
Hata hivyo, Bale amemkariri Diwani wa kata hiyo, Aloyce Luhega, akisema uongozi wa
manispaa unaamini kwamba eneo hilo bado lipo chini ya TASO, hivyo kubadili matumizi yake ni
lazima kuihusisha taasisi hiyo.
Kuhusu ujenzi wa shule hiyo, Afisa Elimu wa Wilaya ya Dodoma, Kigosi, amesema uongozi wa
eneo hilo unapaswa kuainisha maeneo yanayofaa kwa ujenzi, kisha wafuate taratibu
zilizowekwa.
Amesema taratibu hizo ni pamoja na kushirikisha nguvu za wananchi kuanzia ujenzi wa msingi
mpaka kufunga ‘lenta’, ili Serikali iwajibike kukamilisha sehemu inayobaki.
Diwani wa Nzuguni, Aloyce Luhega, alipotafutwa na JAMHURI kuielezea kadhia hiyo,
hakupatikana kwa madai kuwa yuko katika kikao na baadaye kueleza kwamba amesafiri
kwenda kumuuguza dada yake.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge, amesema utatuzi wa changamoto
hiyo ni kwa upande wa Nzuguni ‘C’ kujenga shule katika eneo hilo.

2508 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!