Wananchi 3,113 wa Mbarali mkoani Mbeya, waliohamishwa kutoka katika vijiji wilayani humo kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kabla ya kupunjwa fidia za maeneo yao, wamesema Serikali imeshindwa kuwalipa fidia licha ya kutathmini upya maeneo yao mwishoni mwa mwaka 2015.

Wakati harakati za Uchaguzi Mkuu zilipoanza mwaka jana, walitishia kuachana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa sababu za kupunjwa fidia, lakini baadhi ya makada akiwamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, waliamuru tathmini ifanyike upya na wananchi walipwe stahiki kulingana na maeneo badala ya kilichofanyika awali.

Kazi ya uhakiki na uthamini ilifanyika chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali, Halmashauri ya Wilaya hiyo na wadau wengine na taarifa yote kukabidhiwa kwa Abbas Kandoro, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, wananchi walipwe haki zao kulingana uthamini mpya uliokuwa suluhisho la mgogoro huo.

Afisa Mwandamizi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, amelithibitishia JAMHURI kuwa hakuna uwezekano wa wananchi hao kulipwa hata kama watafuatilia suala hilo kwa kina. “Hakuna malipo,” alisema kwa ufupi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Wahanga, Patrick Mnyota, anasema Kandoro alifanya sehemu yake baada ya kukamilika kwa kazi ya uthamini na kwamba taarifa yote imetumwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanapa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mnyota anasema licha ya taarifa hiyo kuwasilishwa kwa mamlaka husika, wameendelea kuzungushwa na Tanapa walioagizwa na wizara kulipa fidia, jambo linaloendelea kuchochea mgogoro.

Anasema mambo ya kuzungushana yameanza mwaka 2007 na baadaye 2008 walipohamishwa kutoka makazi yao kupisha upanuzi wa hifadhi wakalipwa kati ya Sh 4,000 na Sh 10,000 kwa kila ardhi yenye ukubwa wa ekari moja yenye mazao, majengo na usafiri wa kilomita moja Sh. 1,000.

Kiasi cha fidia hiyo kimejumuisha gharama za usafiri na posho ya usumbufu wa pango la nyumba kwa miezi 36, kitendo kinachoelezwa na wakazi hao kuwa uongozi wa mkoa umejinufaisha na kusisitiza kuwa “Danadana hizi zinaashiria kwamba wahusika waligawana fedha hizo.”

Wananchi wanasema kutokana na ubabaishaji wa viongozi kuendelea kutupiana mpira kwa jambo lililo wazi, wanamwomba Rais, Dk. John Magufuli, kuwasaidia kwani wanaendelea kuumizwa na viongozi wachache wasiojali haki za wananchi wanyonge.

“Serikali ya Mheshimiwa Magufuli inapaswa kufanya ukaguzi Tanapa na Wizara ya Maliasili na Utalii kufahamu fedha hizo za malipo ya fidia zimewanufaisha watendaji wepi badala ya kuendelea kuzungushwa wachukuliwe hatua,” anasema Mnyota.

Wanasema baadhi ya viongozi waliokuwapo katika tawala zilizopita wakapewa nafasi katika utawala wa awamu ya tano wakiachwa waendelee na nafasi zao, wataendelea kuwa vizuizi na kumkwamisha Rais kufanya kazi ya kuwatumikia Watanzania kwa maslahi ya nchi yetu.

Fedha zilizotengwa na Tanapa kwa ajili ya fidia, zinadaiwa kuwanufaisha wajanja wachache walioamua kuwadhulumu wananchi waliolipwa fidia ndogo kwa ‘mtutu wa bunduki’, huku wakilazimishwa kuzikagua hundi hizo wakifika katika makazi yao.

Mnyota anasema kwa muda mrefu Kandoro alikuwa akidai kwamba ameandaa ripoti na kuituma Wizara ya Maliasili na Utalii, jambo ambalo halikufanyika kwa wakati, kwani wanapofuatilia wizarani wanaelezwa kuwa haijafikishwa kama alivyokuwa akiwaeleza.

“Agosti 17, mwaka jana, tuliandika barua kwa Waziri Mkuu na tulipofika ofisini kwake, Katibu wake alimpigia simu Kandoro na kuulizia ripoti iliyofanyiwa kazi na wataalamu, akadai kwamba imetumwa wizarani wakati watendaji wa wizara wakikana kuwa hawajaipokea,” anasema Mnyota.

Kutokana na kushindwa kutoa majibu sahihi ya kulipa haki za wananchi hao, Julai 29 na Agosti 3, 2015, Kandoro aliwaeleza kwamba watakuwa na kikao cha pamoja na wataalamu mbalimbali kumalizia kazi yao huku akiendelea kuwadanganya kwamba ripoti imeshatumwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Maliasili.

Hadi sasa, hakuna majibu ya uhakika wa kulipwa fidia huku Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, akiwaeleza kwamba ripoti hiyo haijamfikia ofisini bado iko kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Viongozi hao wameendelea kuwahadaa wananchi kuhusu malipo ya fidia zao. Wakati Waziri akiwaeleza kwamba bado hajafikishiwa ripoti hiyo. Gazeti la JAMHURI lilifanya mahojiano naye wiki iliyopita na akasema ripoti hiyo anayo na inafanyiwa kazi bila kutaja ni siku gani watawalipa.

Katika hali ya kushangaza, wananchi walimetafuta waziri wiki iliyopita, ila akawaeleza kuwa hajaipata bado iko kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ambaye naye amekana akidai aliiwasilisha muda mrefu Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mgogoro huo uliibuka mwaka 2007 walipohamishwa kwa nguvu kutoka katika maeneo yao kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kulipwa fidia ndogo kwa mtutu wa bunduki huku wengi wao wakiambulia hundi za Sh 4,000 na Sh 10,000 kwa eneo lenye ukubwa ekari moja hadi 10.

Tangu walipolazimishwa kuchukua hundi hizo na kuondoka katika maeneo hayo, wamekuwa wakifuatilia haki zao kwa miaka 10 Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini wamekuwa wakipatiwa majibu yasiyokuwa na ufumbuzi wa mgogoro huo kutokana na wahusika kutupiana mpira huku wakijua kupunjwa kwa malipo kuliwanufaisha baadhi ya viongozi wachache serikalini.

Wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa sasa wa Mbeya, Amos Makala kuingilia mgogoro huo, vinginevyo naye akiedelea kukaa kimya watajua kuwa hana msaada kwao.

Mwishoni mwa mwaka jana JAMHURI liliripoti mgogoro huo ambao umeibua mvutano wa taasisi mbalimbali za Serikali ambazo zimelalamikiwa kwamba zimehusika kuwapunja fidia wananchi na kiasi kikubwa cha fedha za umma kuwanufaisha watu wachache.

Baada gazeti hili kuandika kwa undani kuhusu mgogoro huo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanapa, Ofisi ya Waziri Mkuu na uongozi wa Mkoa wa Mbeya kwa pamoja, walikubaliana kufanya uthamini mwingine kwa kupima maeneo hayo na kuandaa fidia mpya kwa wananchi lakini licha ya kazi hiyo kumalizika, kwa zaidi ya miezi minne sasa, hakuna kinachoendelea.

Waziri Mkuu (wakati huo), Mizengo Pinda, alipofikishiwa malalamiko yao, aliamuru iundwe kamati iliyowashirikisha wakuu wa mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa na kuagiza wananchi wakutane na mthamini mkuu wa Serikali.

Machi 12, 2015 Kandoro, akiwa ameambatana na wakuu wa mikoa hiyo –  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, na Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, walikutana na wananchi hao wilayani Mbarali na kusikiliza malalamiko yao.

Baada ya kusikiliza hoja zao, ahadi ilitolewa kwamba fidia hiyo ingelipwa, lakini hadi sasa hakuna ufumbuzi wowote uliopatikana zaidi ya wahusika kutupiana mpira.

Kamati iliyoundwa kwa maagizo ya Waziri Mkuu, iliteua wajumbe  Esteria Ndaga, Athman Mohamed, Mkaguzi wa fedha za ndani kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mthamini wa Ardhi wa Wilaya ya Mbarali, wataalamu wengine kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Usalama wa Taifa na Takukuru, lakini imeshindwa kukamilisha ufumbuzi wa suala hilo.

Aprili 16 na 17, 2015 aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu, aliagiza kamati hiyo kufanya tathmini upya na kukamilisha kazi ya kuwalipa wananchi hao fidia zao, huku tangazo la Serikali Na 28 likiwa limeagiza wananchi ambao hawakufanyiwa tathmini nao warudi katika maeneo yao.

Pamoja na agizo hilo la Nyalandu, Mnyota anasema hakuna utekelezaji wowote na kwamba wamejiridhisha kwamba maagizo hayo yaliyotolewa bila utekelezaji ni ulaghai wa wazi uliofanywa na watendaji wa serikali.

Anasema Mei 15, 2015 jana Kamati ya Wahanga wa uhamisho huo waliopunjwa fidia zao, iliamua kurudi tena kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Ofisa Ardhi wa Mkoa, lakini wakaelezwa na Katibu wake, George Kikosa, kwamba taarifa ya tathmini imepelekwa kwa Waziri Mkuu tangu Mei 5, mwaka jana.

Anasema kiasi cha Sh bilioni 6 kinadaiwa kutumika kuwalipa baaadhi ya wahanga walioambulia kati ya Sh 4,000 na 10,000 ikijumuisha nauli ya kusafirisha mizigo yao na kwamba kitendo hicho ni cha kihuni.

Novemba 7, 2013 Ofisi ya Waziri Mkuu iliwaandikia barua wananchi hao na kuwataka kuwa na subira wakati akishughulikia haki zao za madai ya fidia ya ardhi.

 “Kamati ya walalamikaji ipeleke maombi yao rasmi kwa Mthamini Mkuu wa Serikali,” inaeleza sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Buberwa kwa niaba ya Katibu wa Waziri Mkuu, na nakala kupelekwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Maliasili na Utalii, Katibu Mkuu wa CCM na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

By Jamhuri