Wakazi wa Manispaa ya Kigamboni, Dar es Salaam, wameulalamikia uongozi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa kushindwa kusambaza umeme kwa wateja wapya, licha ya kulipia huduma hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

 

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamesema Tanesco katika Manispaa hiyo, imekuwa kero kwa wateja ambao wameanza kukata tamaa kupata huduma ya umeme hata baada ya kukamilisha taratibu zote.

Leticia Lubango, mkazi wa Gezaulole mtaa wa Kizani, ameliambia JAMHURI amelipa zaidi ya Sh milioni 1.5 tangu Oktoba mwaka jana,  lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea na hajui lini atapatiwa huduma hiyo.

“Mpaka sasa kuna wateja zaidi ya elfu moja ninaowafahamu ambao tayari wameshalipia fedha kwa ajili ya kupewa huduma ya kufungiwa umeme, lakini kila kukicha pamekuwapo na majibu yasiyoeleweka kutoka kwa watendaji,” amesema Lubango.

 

Amesema viongozi wa Tanesco katika Manispaa ya Kigamboni, wamekuwa wasumbufu katika kutoa huduma ya kufunga umeme, huku wakiendelea kuchukua fedha za wananchi wanaohitaji huduma hiyo.

Hassan Nasoro, mkazi wa Vijibweni Kigamboni, amesema Tanesco Wilaya wamekuwa watu wa ajabu kwa kuendelea kukusanya fedha kutoka kwa wateja kwa ajili ya kazi ambazo hawana uwezo kufanya kwa wakati.

“Huu ni mwaka wa pili tangu nilipe fedha kwa ajili ya kuunganishiwa umeme kwenye nyumba yangu iliyopo Mji Mwema, cha ajabu kila nikifuatilia majibu ninayopewa ni kuwa hakuna nguzo pamoja na nyaya,” amesema Nasoro.

Amesema katika mtaa wake wateja anaowafahamu wanaohitaji huduma hiyo ni zaidi ya hamsini ambao tayari wameshalipia kila kitu kwa ajili ya kupewa huduma hiyo, lakini wamekuwa wakipigwa danadana za hapa na pale.

“Tanesco Wilaya ni kama wamegeuka matapeli wa kuaminika, kwani kila kukicha wanaendelea kupokea fedha toka kwa wateja wapya wakati kuna wateja hadi wa mwaka jana ambao hawajafikiwa na huduma licha ya kulipia kila kitu,” amesema Nasoro.

 

Amesema licha ya shirika hilo kuendelea kukusanya fedha kutoka kwa wateja wapya wenye mahitaji ya kuunganishiwa umeme majumbani, bado hawakosi visingizio kila kukicha; hali inayoendelea kuacha sintofahamu kwa wateja wao.

Akizungumza na JAMHURI, Meneja wa Tanesco Wilaya ya Kigamboni, Mhandisi Richard Widimael, amesema ni kweli ofisi yake imekuwa ikilalamikiwa kutokana na tatizo hilo na kwamba shirika limekuwa likifanya juhudi za dhati za kulitafutia ufumbuzi.

 

“Ni kweli tunao wateja ambao wamelipa tangu mwaka jana lakini hawajapatiwa huduma stahiki…hii inatokana na uhaba wa nguzo  pamoja na vitendea kazi vingine ambavyo ni adimu kupatikana,” amesema Widimael.

Amesema hata miradi ya kuunganisha umeme vijijini umekuwa ukisuasua kutokana na uhaba wa nguzo pamoja na nyaya za kuunganishia nguzo kuwa adimu kiasi cha kusababisha kero kwa wateja wengi.

“Lengo la shirika ni kuunganisha vijiji vyote na huduma za nishati ya umeme kupitia mradi wa REA III ifikapo mwaka 2021, maeneo mengine tunayotarajia kuyafikia  na huduma muhimu za kijamii ni  kama vile vituo vya afya na shule,” amesema Mhandisi Widimael.

 

Amesema kutokana na uhaba wa nguzo, mradi wa REA awamu ya III utatekelezwa kwa kutumia nguzo za zege na hivyo kuondoa changamoto za kuungua kwa nguzo na kukatika umeme mara kwa mara kutokana na matukio ya nguzo kuchomwa moto hasa katika maeneo ya vijijini.

Amesema mpango mkakati wa shirika unaonesha kuwa, vijiji 7,673 vitakapelekewa umeme wa gridi katika mradi wa kusambaza umeme vijiji awamu ya tatu (Turnkey III) utakaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016/17.

 

“Awamu ya kwanza itatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi 2018/19 (REA IIIa) na awamu ya pili itatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2020/21 (REA IIIb),” amesema.

Amebainisha kuwa, kwa mujibu wa taarifa ya maeneo rasmi ya kiserikali kutoka Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Tanzania bara ina jumla ya vijiji 12,259. Kutoka na juhudi za Serikali TANESCO na REA, hadi kufikia Juni 2016 jumla ya vijiji 4,408 sawa na asilimia 36 vimeshafikiwa na umeme mamoja na changamoto zilizopo.

Amesema kati ya vijiji hivyo, 7,673 vitapelekewa umeme wa gridi pia vijiji 178 vitapelekewa umeme wa nje ya gridi kutokana na nishati jadidifu, kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuvipelekea umeme kwa gharama nafuu kwa sasa.

By Jamhuri