Wananchi wamkataa mkuu wa wilaya Kwimba

Taarifa iliyotolewa leo Februari 16, 2018 na ofisi ya waziri mkuu imeeleza kuwa wananchi hao wametoa kauli hiyo baada ya kuzuia msafara wa Majaliwa alipowasili katika ofisi za Halmashauri ya wilaya Kwimba kwa ajili ya kuzungumza na watumishi, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

Wananchi wa wilaya ya Kwimba mkoani hapa wamemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuondoka na mkuu wa wilaya hiyo Mtemi Msafiri kwa madai ya kutoridhishwa na utendaji wake.

Taarifa iliyotolewa leo Februari 16, 2018 na ofisi ya waziri mkuu imeeleza kuwa wananchi hao wametoa kauli hiyo baada ya kuzuia msafara wa Majaliwa alipowasili katika ofisi za Halmashauri ya wilaya Kwimba kwa ajili ya kuzungumza na watumishi, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

Wananchi hao walimkataa mkuu huyo wa wilaya kupitia ujumbe wa mabango 17, Majaliwa kuwataka wananchi hao kuwa watulivu wakati Serikali inafanyia kazi malalamiko yao.

Wananchi hao wamedai Msafiri anatabia ya kuamrisha polisi wawakamate kwa kisingizio cha uzururaji na kisha wanawekwa mahabusu, kisha kutolewa na kupelekwa  kulima kwenye shamba lake.

Waziri Mkuu amesema Serikali inahitaji kila mtumishi atambue majukumu yake na ayatekeleze. “Hakuna atakayeonewa, haki zenu zote tunazitekeleza nanyi mnatakiwa kutenda haki kwa kuwatumikia wananchi.”

Hata hivyo, Majaliwa amemtaka mkuu huyo wa wilaya,  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba, Pendo Malebeja na wakuu wote wa Idara wajitathmini kama kweli wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na kuwatumikia wananchi.

“Mkurugenzi katika kipindi chako chote cha utendaji kuanzia mwaka 2013 hadi leo, fedha nyingi za Serikali zilizoletwa Kwimba zimepotea na hazijulikani zilipo huku miradi mingi bado haijakamilika na muda wote huo Halmashauri imekuwa inapata hati chafu,” amesema Majaliwa.