*Walitumia kujinyooshea mapito kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015

Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemalizika wiki iliyopita huku kwa kiasi kikubwa likionekana kugeuzwa kuwa jukwaa la siasa.


Wabunge kutoka vyama vya siasa, hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameonekana kulitumia Bunge hilo kutafuta umaarufu wa kisiasa kwa wananchi. Wabunge kutoka katika vyama hivyo wameweka maslahi ya taifa pembeni na kukumbatia itikadi za vyama vyao.

Hali hiyo imelifanya Bunge kugawanyika vipande na kuwapa wakati mgumu Spika, naibu wake na wenyeviti wa Kamati za Bunge kutekeleza majukumu yao.


Vyama hivyo vimelifanya Bunge kama sehemu ya kuanzishia hoja zao na kisha kuzipeleka katika mikutano ya hadhara ya wananchi.


Wabunge hao pia wamekuwa wakiziweka hoja zao hizo kwenye mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Jamii Forum na Mabadiliko kutafuta kuungwa mkono na watu walio nje ya Bunge.


Habari nyingine kutoka ndani ya Bunge zinaeleza kuwa wabunge kutoka CHADEMA na CCM wamejipanga kuhakikisha wanalitumia Bunge kuwashwishi wapiga kura kuunga mkono vyama vyao katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015.


Hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Iramba Magharibi Mwigulu Nchemba (CCM) na ile ya  Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla (CCM), inaelezwa kuwa ni moja ya  mikakati ya kuwateka vijana wa vyuo vikuu na wa wasio na ajira kuiunga mkono CCM.


Nchemba amewasilisha hoja ya kutaka uanzishwe mfuko wa elimu ya juu na Dk. Kigwangalla amewasilisha hoja ya kutaka uanzishwe mfuko wa taifa wa vijana.


Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), amewasilisha hoja binafsi ya udhaifu wa elimu upatiwe ufumbuzi, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika CHADEMA), amewasilisha hoja ya kero ya maji jijini Dar es Salaam ipatiwe ufumbuzi na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA), amewasilisha hoja ya kushughulikia udhaifu wa Baraza la Mitihani Tanzania (BMT).


Hata hivyo, Bunge limefuta hoja za wabunge wa CHADEMA kwa madai ya kuepuka vurugu zilizojitosheleza Februari 14 bungeni.


Hoja inayoonekana kuharibu taswira ya chama kingine haipitishwi bungeni hata kama ina maslahi ya Taifa. Iliyowasilishwa na Mbatia ilionekana kuwa mwiba mkali kwa CCM baadhi ya wabunge wakiongozwa na Msemaji wa Serikali bungeni, William Lukuvi kuhaha kuhakikisha hoja hiyo inazimwa.


Kuna wakati wabunge kutoka vyama vya upinzani waliamua kusisia kikao cha Bunge kwa kuondoka ndani ya ukumbi wa Bunge.


Inaelezwa kuna mkakati wa kuhakikisha kuwa hoja zinazowasilishwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani zinazoleta picha mbaya kwa Serikali zinakwamishwa.


Mbunge wa Viti Maalumu, Mhandisi Stela Manyanya ameiambia JAMHURI kuwa Bunge kwa sasa limepoteza uelekeo kwa kutanguliza uitikadi badala ya utaifa.


“Bunge limeacha kujadili mambo ya kitaifa sasa kila mbunge akisimama anatetea hoja ya chama chake,” amesema.


Amesema wabunge wamesahau majukumu yao na kujikita katika siasa bungeni hali ambayo inadhorotesha utendaji wa Bunge.


Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (CHADEMA), amesema ili kuepuka tatizo la vyama kuingiza itikadi Serikali inatakiwa kuwa na ilani ya taifa.


“Mbunge ni mwakilishi wa wananchi, chama ni kama ‘conduit’ (bomba) ya kumpeleka mbunge bungeni, akiisha kuapishwa anapaswa kutetea maslahi ya taifa pamoja na kuwa chama ndiyo kilichomteua.


“Lakini hapo hapo kumbuka usipotetea kile kilicholetwa na chama chako unaweza kufukuzwa uanachama na ukifukuzwa ubunge basi tena, hivyo itakupasa kutetea tu hata kama hakuna maslahi kwa taifa bali ni kwa chama.


“Kwa mfumo huu tulionao katika Bunge letu chama tawala kina wabunge wengi na kimeshika dola.


“Sisi tunataka kushika dola hivyo wabunge wake wanatetea chama chao kiendelee kushika dola kwa kutetea hata kile kisicho na maslahi kwa taifa kama unavyoona.


“Sasa nini kifanyike ili kukomesha itikadi za vyama. Hapa kuna shida ya kimtazamo katika kutekeleza sera, au Ilani ya CCM wanasema tunatekeleza ilani ya chama chao.


Kwangu mimi sikubaliani na wazo hilo kwa kuwa linaletwa hapa tunajadili na linapitishwa na Bunge si chama.


“Ili kuondoa imani hiyo ya wabunge wa CCM kinachotakiwa ni kuunda ilani ya taifa na si ya chama, itakayopitishwa na Bunge, na ambayo itatupa dira kama nchi,” amesema Mchungaji Natse.


Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tanzania cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, amesema wabunge wa CCM wamekuwa wakiangalia zaidi kukilinda chama chao bila kujali umuhimu wa hoja inayojadiliwa ina maslahi kwa taifa.


“Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi hawangalii umuhimu wa hoja bali wanachokifanya ni kumlinda mtu moja moja, au chama chao kisitoke madarakani.


“Ukiangalia hoja iliyowasilishwa na Mbatia (James) ya udhaifu wa elimu ilikuwa na umuhimu mkubwa katika taifa hili, mtoa hoja alieleza vizuri  kuhusu udhaifu katika elimu na  hakuna asiyejua kuwa elimu yetu inalalamikiwa sana na watu wengi.


“Lakini kwa kujua kuwa ilikuwa na mashiko katika taifa hili wakafanya wanavyojua na ikaishia kuwa anachodai ni mtaala lakini kulikuwa na matatizo mengi sana ya kujadili.


Amesema kuwa kutokana na CCM kutaka kuendelea kukaa madarakani na suala hilo kuharibu taratibu za bunge litaendelea hadi utakapofanyika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.


Profesa Baregu amesema kuwa ipo haja ya   kurejea misingi ya utaifa kwa kutoa elimu kwa  ujamaa, maadili, uzalendo ili kuachana na hali ya kutojali ubinafsi na yote yanayozungumzwa kuharibu Bunge na taifa kwa ujumla.


“Bahati nzuri tupo katika mchakato wa kuandaa Katiba mpya, hapa ndipo tunaweza kusema kuwa tunazaliwa upya mambo yote yatafanyika vizuri kwa kuwa Katiba itakuwa na mfumo wa vyama vingi.


Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia amesema kuwa wabunge wamesahau wajibu wa viapo vyao vya kulitumikia taifa na kikitumikia chama.


Amesema jukumu la kwanza la mbunge ni kulitumikia taifa, pili ni jimbo, tatu kukitumikia chama na mwisho ni kuangalia mambo yake binafsi.


“Mimi ni mbunge nimeteuliwa na Rais nilipoapa tu niliapa kuwatumikia Watanzania, ni mbunge wa majimbo yote ya Tanzania, hivyo natakiwa kuanza na utaifa kwanza na si NCCR-Mageuzi,” amesema Mbatia.


Akizungumza na JAMHURI, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, amesema tabia inayofanywa na bunge kwa sasa inatia shaka.


“Wabunge wana maadili na kanuni zao, kanuni za Bunge zipo zinajieleza vizuri, wametunga wenyewe na kuzipitisha wenyewe bila kupitiwa na mtu mwingine.


“Wanalindwa kwa kanuni hizo, kama kuna mtu anaona kaonewa anayo haki ya kwenda kulalamika katika kamati inayohusika lakini kwa sasa wameweka pembeni kanuni hizo na hii inatia wasiwasi.


“Sidhani kama kuna chama ambacho kinawatuma wabunge wake kwenda bungeni kufanya mambo hayo yanayoonekana kwa sasa, kama ni hivyo tunaipeleka wapi nchi hii?


“Bunge ni taasisi ya kisiasa, wabunge wake wanayo fursa ya kujipanga na kuwashawishi wapigakura wake kupitia michango yao lakini wasisahau dhana ya uwakilishi wao bungeni.


Amesema iwapo mbunge atasahau dhana ya uwakilishi atakuwa hakuitendea haki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi bila kujali waliompigia kura na wasiompigia.


Amesema chama tawala hakipaswi kusijisahau na kinapaswa kufahamu kuwa uongozi ni kupokezana kisijinasabu kuwa na wabunge wengi kwa sasa, ipo siku watakuwa wachache.

Amesema pamoja na mabadiliko hayo bado kelele zinazotoka bungeni zitaendelea lakini mwarobaini wake ni Katiba mpya.


Hata hivyo, Dk. Bana ameshangazwa na Bunge kujisahahu na kuingilia muhimili mwingine ilhali hakuna mhimili wenye nguvu kupita mwingine.


“Tuna mihimili mikubwa mitatu lakini  tumeshuhudia Bunge linataka kuwa juu ya muhimili wa utawala hili ni kosa kubwa kwani hakuna mhimili ulio juu ya mwingine, yote ina nguvu sawa.

By Jamhuri