Waingereza wanasema ‘Politics is a science.’ Tafsiri rahisi ya maneno haya ni kwamba siasa ni taaluma. Ni vizuri Watanzania tukalifahamu na kulizingatia hili. Katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini mwaka 2015, kumekuwapo na viashiria vya rafu za kisiasa.

Baadhi ya wanasiasa wetu wameamua kuchagua maisha ya kucheza rafu za kisiasa. Ingawa sina ushahidi wa moja kwa moja, lakini ninaweza kuamini kuwa rafu za kisiasa zinachezwa na wanasiasa wasio na taaluma ya siasa. Hao bila shaka nia yao kuu ni kupata uongozi na umaarufu wa kisiasa kwa ajili ya kujipatia maslahi binafsi.

 

Kwa bahati mbaya Watanzania wengi wanapenda wanasiasa wenye maneno mengi makali na mahodari wa kuwatuhumu wapinzani wao kwa mabaya, tena pasipo kuonesha uthibitisho wa tuhuma hizo. Hii ni dhana mbaya iliyojengeka Tanzania.

Wakati fulani nilifanikiwa kuibiwa siri ya wanasiasa wanaotumia majukwaa ya kisiasa kucheza rafu za kisiasa kwa kuwapaka wengine matope, ikiwa ni pamoja na kuwazushia uongo na wanaotoa ahadi nyingi ambazo kiuhalisia hazitekelezeki.

 

Mwanasiasa mmoja mstaafu aliyepata kuwa kinara wa kuwazushia wapinzani wake uongo, ili waonekane hawafai katika jamii, aliniibia siri ambayo sasa ninashuhudia ukweli wake hapa Tanzania. Aliniambia, “Watanzania wengi wanapenda kumshabikia mwanasiasa mzungumzaji sana, anayezusha kashfa mbaya dhidi ya wengine na anayewaahidi mambo makubwa makubwa hata kama hayatekelezeki. Hapa Tanzania ukiwa mwanasiasa msema kweli ‘itakula’ kwako.”

 

Kweli, baadaye nimekuja kubaini niliyoambiwa na mwanasiasa huyo ni ukweli mtupu. Watanzania wengi wanawapenda wanasiasa wazushi na wanaowaahidi kuifanya Tanzania kuwa nchi ya asali na maziwa! Nchi ya watu wanaokaa bila kufanya kazi wakisubiri kutafuniwa kila kitu na Serikali ili wao wameze!

 

Leo mwanasiasa wa Kitanzania anaweza kuibuka na kashfa nzito, kwa mfano, akasema rais ameuza nchi, na wananchi wengi wakamshangilia mwanasiasa huyo na kuamini hivyo bila kuhoji imeuzwa kwa nani, kwa bei gani na uthibitisho wake uko wapi.

 

Lakini pia, hapa Tanzania ndipo mahali ambapo mwanasiasa wa anayehitaji uongozi, anaweza kupata ujasiri wa kusimama jukwaani akawaahidi wakazi wa kijiji fulani kwamba atawajengea uwanja wa ndege wa kimataifa ndani ya wiki tatu na kuwanunulia ndege ya kuwasafirisha bure kwenda kokote wanakotaka, na wanakijiji husika wakampigia makofi na kumshangilia kwa vifijo, shangwe na vigelegele!

 

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipata kusema, “Watu tunakubaliana na wazo, lakini mawazo ambayo waziwazi ni ya kijinga, lazima tuyakatae. Mtu mwenye akili timamu akikupa mawazo ya kipumbavu, usipoyakataa anakudharau. Sasa hatuwezi kukubali mambo ya kipumbavu Tanzania.”

 

Je, ni lini Watanzania tutakuwa na uthubutu wa kuyakataa maneno ya kijinga na kipumbavu tunayoambiwa wanasiasa wetu? Wakati ni huu, tuamke.


Kwenye nchi za wengine, mwanasiasa anayetoa ahadi tata lazima ataulizwa na wapigakura husika, ni vipi ataweza kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa kwa kipindi kifupi kiasi hicho na ni wapi atatoa fedha zitakazogharamia mradi mkubwa kiasi hicho. Basi, atadharaulika mbele ya wananchi husika iwapo atashindwa kutoa majibu yenye ushahidi dhahiri. Watanzania wengi hawana uthubutu wa kuhoji vitu vya aina hiyo.

 

Dhana iliyojengwa na Watanzania ya kutokuwa na uthubutu wa kuhoji uthibitisho wa tuhuma na ahadi wanazoambiwa, imeendelea kuwajengea baadhi ya wanasiasa wetu ujasiri wa kucheza rafu za kisiasa, ili kupata uongozi na umaarufu kama si maslahi binafsi katika jamii.


Kimsingi, Tanzania si nchi ya ajabu kiasi cha kutofautiana na mataifa mengine katika masuala ya kisiasa.

Nchi hii ina kila sababu ya kuwa na wananchi waelewa na wasiodanganyika, ina kila sababu ya kuwa na wanasiasa wenye taaluma.

 

Umefika wakati wanasiasa wetu wawathamini wananchi ambao ndiyo wapigakura wao kama si mtaji wao katika jamii. Waepuke kasumba ya kucheza rafu za kisiasa kwa kuwazushia wapinzani wao wa kisiasa kashfa mbaya zisizo na ukweli.

 

Ninasisitiza hili nikiamini kwamba siasa za uzushi zina madhara makubwa katika jamii. Uzushi wa kashfa zisizo za kweli umekuwa ukisababisha watu wanaofaa kuwa viongozi bora na waadilifu kukosa uongozi katika ngazi mbalimbali.

 

Kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani nchini, ni muhimu kwa wanasiasa wetu kuhakikisha wanaepuka kucheza rafu za kisiasa zinazoweza kuishia kuwapatia Watanzania viongozi wabovu. Tunahitaji Tanzania yenye wanasiasa wenye taaluma na isiyo na rafu za kisiasa. Inawezekana.

 

Hii ni changamoto kubwa kwa vyama vyetu vya siasa kama vile Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), NCCR-Mageuzi, Civic United Front (CUF), Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP), miongoni mwa vingine nchini.

0765 649 735


951 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!