Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, limebaini sehemu ya mtandao wa watuhumiwa wa mauaji 12 yanayoendelea wilayani Mkuranga, Kibiti na Rufiji, akiwamo mwanzilishi wa mauaji hayo, anayetajwa kwa jila la Abdurshakur Ngande Makeo.
Akizungumzia hali ya kiusalama kutokana na vitendo vya mauaji vinavyoendelea katika wilaya hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Onesmo Lyanga, amesema wanaendelea na mapambano na upelelezi kuwatia nguvuni wahusika.
Katika msako huo, Jeshi  la Polisi limefanikiwa kupata picha za watu wanne huku wengine wakiendelea kusakwa. Amewataja watuhumiwa kuwa ni:
1. Faraj Ismail Nangalava
2. Anaf Rashid Kapera
3. Saidi Ngende
4. Omary Abdallah Matimbwa
5. Shaban Kinyangulia
6. Haji Ulatule
7. Ally Ulatule
8. Hassan Uponda
9. Rashid Salim Mtulula
10. Sheikh Hassan Nasri Mzuzuri
11. Hassan Njame
Saidi Ngende inadaiwa kuwa na makazi Ikwiriri na Omary Abdallah Matimbwa anaishi Dar es Salaam ambao picha zao zimepatikana ikiwa ni pamoja na Faraj Ismail Nangalava na Anaf Rashid Kapera.
Amesema wengine wanane bado picha zao hazijapatikana hadi sasa. “Jeshi letu limebaini hayo kwa kushirikiana na wasiri wetu huku tukiendelea na uchunguzi zaidi,” amebainisha.
Kamanda Lyanga amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakipenda kutembelea maeneo ya Kisiwa cha Simbaulanga na Kisiwa cha Saninga, Kijiji cha Nchinga.
Maeneo mengine wanayopenda kutembelea ni Kijiji cha Mfenesini, Kata ya Nyamisati, na maeneo mbalimbali za wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga.
Katika kuhakikisha watuhumiwa hao wanakamatwa, Jeshi la Polisi nchini limetoa mwito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa siri kufichua watuhumiwa kwani wanahatarisha hali ya usalama kimkoa.
Kamanda Lyanga ametangaza zawadi ya Sh milioni 5 kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwao.
Hivi karibuni, jeshi hilo lilitangaza kuwapo kwa mtandao wa majina 102 ya wauaji ambao wanasakwa kudhibiti vitendo vya mauaji vinavyotia hofu wananchi.
Aprili 18-24 katika toleo Na 290 Gazeti hili la JAMHURI, lilichapisha taarifa kuwa matukio ya ujambazi wa kutumia silaha, mauaji ya polisi na viongozi wa vijiji katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, yanahusishwa na vikundi vya vijana wanaopata mafunzo kutoka kwenye kundi la al-Shabaab nchini Somalia.
Kwa miaka minne hadi mitano iliyopita, vijana kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Rufiji, hasa Ikwiriri, wamekuwa wakisajiliwa na kundi hilo la kigaidi, huku wazazi wao wakiambulia ujira wa dola 3,000 za Marekani (zaidi ya Sh milioni 6).
Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa wakazi wa Ikwiriri ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini kwa sababu za kiusalama, amesema kumekuwa na wimbi la vijana wenye umri wa miaka 16-25 kupelekwa kwenye mafunzo huko Somalia.
“Hapa Ikwiriri katika kipindi cha miaka kama mitano iliyopita, kumekuwa na wimbi la vijana wadogo kupelekwa Somalia. Inasemekana wanakwenda kujiunga na kikundi cha al-Shabaab, lakini vijana hao wamekuwa wanapatikana kupitia kwa mawakala kadhaa kwenye misikiti.
“Si kweli kwamba polisi hapa Ikwiriri hawajui, maana hata ukifuatilia wale viongozi wa vijiji ambao wamekuwa wakitoa taarifa za vijana hao, wamekuwa wakiuawa kwa staili inayofanana… sasa hapo unaweza kuona namna zoezi linavyokuwa gumu,” amesema.
Chanzo chetu kingine kimemtaja mtu ambaye jina lake tunalifupisha kwa kifupi kama S.B., kuwa ndiye anayefanya kazi ya udalali wa kuwapeleka vijana hao nchini Somalia, huku wazazi wa watoto hao wakiambiwa kuna kazi wanakwenda kuifanya huko.
Chanzo hicho kimesema hata baada ya baadhi ya wenyeviti wa vijiji kupeleka taarifa za uhusika wa S.B., kilichofuata ni mauaji.
“S.B. alipotea hapa Ikwiriri kwa takribani miaka mitatu, hata baada ya kurejea amekuwa na mali nyingi. Mali ambazo si za kurithi na haziendani na utafutaji wa halali katika kipindi hicho kifupi. Yamekuwa yanasemwa mengi, lakini ukimgusa andaa sanda kabisa,”  kimesema chanzo chetu.
JAMHURI limedokezwa kuwa vijana zaidi ya 27 kutoka maeneo mbalimbali wilayani Rufiji, wamechukuliwa kwenda kujiunga na al-Shabaab, chini ya udalali wa Bwana S.B.
Chanzo hicho kimesema mmoja na vijana ambaye alichukuliwa alishindwa aina ya kazi na akarudi.
Habari ambazo JAMHURI, limezipata zinaonesha kwamba kikundi hicho cha wauaji kimekuwa kikimtumia mtoto mdogo mwenye umri chini ya miaka 18, kuwapelekea chakula huko msituni eneo la Mparange wilayani Rufiji. Jina la mtoto huyo tunahifadhiwa kwa sababu za kitaaluma.
“Kijana huyo mdogo amekuwa akitumiwa na hao wauaji kuwapelekea chakula. Mtoto huyo amekuwa akiwahudumia pasipokuwa na simu. Akikamatwa huyo anaweza kusaidia sana upelelezi wa polisi… hapa kila mtu amejaa hofu kuhusu usalama,” kimesema chanzo chetu.

Hali ilivyo Mkuranga, Kibiti na Rufiji
Hali ya usalama katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji imezidi kuwa ya wasiwasi, huku vyombo vya usalama vikiweka zuio katika maeneo hayo.
Baadhi ya mazuio hayo ni kupiga marufuku kuendesha pikipiki kuanzia saa 12:00 jioni, wananchi hasa maeneo ya Ikwiriri wilayani Rufiji wamekuwa wakitakiwa kulala mapema.
Katika mahojiano na Mbunge wa Jimbo la Kibiti, Ally Ungando, anasema hali si nzuri kutokana na ukweli kwamba wananchi na hata yeye wako katika sintofahamu ya kiusalama.
Ungando amesema yeye binafsi yuko kwenye hatari. “Naomba nisiwe mzungumzaji maana mwenyewe niko katika ‘danger zone’, viongozi wangu wa vijiji wanauawa, huoni kwamba anayefuata hapo ni mimi? Nisingependa kulizungumzia hata kidogo, unanitafutia balaa, sitaki kuongea kwenye vyombo vya habari, maana nikiongea utaandika kwenye magazeti, na hao wenzetu (wauaji) wanasoma. Hapa mimi nasubiri hatima yangu.”
Wakati Mbunge wa Kibiti akizungumza na JAMHURI, Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega, yeye amesema hawezi kuzungumzia jambo hilo, badala yake anasubiri uchunguzi wa vyombo vya dola ukamilike.
 
Matukio la Kibiti
Polisi wanane wameshauawa wakiwa kazini. Tukio la kuuawa kwa askari wanane limetokea ikiwa ni siku chache baada ya askari wa Jeshi la Polisi kuwaua kwa risasi wanaume watatu waliokuwa wamevalia baibui.
Wanaume hao waliokuwa na pikipiki mbili, walikuwa wakijaribu kukwepa vizuizi vya polisi vilivyokuwa vimewekwa katika Daraja la Mkapa.
Mei, 2016
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Saidi Mbwana, aliuawa kwa kupigwa risasi.

Oktoba, 2016
Aliyekuwa  Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyambunda, Ally Milandu, aliuawa baada ya kuvamiwa na watu wanne waliompiga risasi mbili.

Novemba, 2016
Wenyeviti wawili wa vitongoji vya kijiji hicho waliuawa kwa kupigwa risasi.

Januari, 2017
Mfanyabiashara Oswald Mrope aliuawa kwa kupigwa risasi mbele ya familia yake.

Februari 3, 2017
Watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga, na kuichoma moto huku yeye mwenyewe akifanikiwa kutoroka.

Februari 24, 2017
Watu watatu akiwamo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, waliuawa kwa risasi.

April 13, 2017
Polisi wanane waliuawa na watu wasiofahamika katika kijiji cha Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti. Inspekta Peter Kigugu, F.3451 Koplo Francis, F.6990 PC Haruna, G.3247 PC Jackson, H.5503 PC Siwale, H.1872 PC Zacharia, H.7629 PC Maswi na H.7680 PC Ayoub.

Mei 12, 2017
Katibu wa CCM, Kata ya Bungu, Alife Mtulia, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyambunda, Wilaya ya Kibiti aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake.

Mei 18, 2017
Mwenyekiti wa CCM, Tawi la Njianne Wilaya ya Kibiti, Iddy Kirungu, aliuawa na mwanaye Nurdin kujeruhiwa kwa risasi.
 Mwaka 2013 mauaji yalitokea wilayani Kilindi mkoani Tanga, ambako msikiti wa Madina ulibainika katikati ya pori kati ya Tanga na Bagamoyo.
Mwaka 2014, vijana waliokuwa wakipewa mafunzo ya kigaidi walikamatwa mkoani Mtwara wakiwa wanapewa mafunzo tayari kujiunga na al-Shabaab.

By Jamhuri