Tumesikia kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo mbioni kuwashughulikia wanachama wake wanaodaiwa kukisaliti chama chao wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana. Ni uchaguzi ule wa kihistoria ambao tulishuhudia ushindani mkubwa.

Haijulikani CCM itatumia njia gani kuwapata wasaliti wake kwa haki.

Suala hili linaweza kuonekana kama ni suala la CCM peke yake. Kwa hiyo, mtu anayejaribu kuliandika gazetini anaweza kuonekana kama mtu anayevamia mambo yasiyomhusu.

Lakini CCM ni chama cha utawala. Utawala wake unamhusu mwanachama na asiye mwanachama wa CCM. Lakini kilichofanyika, CCM inaweza kuwa fundisho kwa vyama vya upinzani.

Ni katika mazingira hayo tunalazimika kuliangalia kwa macho mawili suala hili la wasaliti wa Chama Cha Mapinduzi.

Kuna hatari moja inayotunyemelea katika kuliangalia suala hili. Iko hatari ya kuwachukulia hatua watuhumiwa bila kutafuta sababu kwa nini watu hao waliamua kukisaliti chama chao. Si vizuri kutafuta jibu tu bila kutafuta kinga itakayozuia jambo hilo la usaliti kujirudia.

Wakati wa ukoloni tulikuwa na huduma za afya. Na leo tunazo pia huduma za afya. Tofauti yake moja kubwa ni mkoloni alitilia mkazo tiba, na sisi tunalitia mkazo kinga. Na tuna sababu mbili za kufanya hivyo.

Kwanza, kinga inasaidia wananchi kutopata magonjwa. Na pili, kuna magonjwa mengine yaliyozuka miaka hii ambayo hayana tiba ya uhakika.

Vivyo hivyo, ni vyema tukatafuta wale wanaoitwa ‘wasaliti’ walifanya nini na kwa nini walifanya hivyo. Tusishughulike na matokeo, tushughulike na chanzo.

Kwa kifupi, wale wanachama wa CCM wanaotuhumiwa kwa usaliti ni wanachama wanaodaiwa kushirikiana na watu wa Ukawa kuiangusha CCM. Ni wanachama wa CCM walioonekana kumuunga mkono mtu aliyegombea kiti cha urais kupitia Ukawa, naye si mwingine bali ni Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania.

Hapana shaka wapo wanachama wa CCM waliomuunga mkono kwa wazi hata kuamua kuhama naye, na wapo wanachama waliofanya mambo kwa siri.

Hapa hakuna mtu anayeweza kuilaumu CCM kwa kuwachukulia hatua wasaliti wake. Lakini CCM inatakiwa kutenda haki kwa kutafuta sababu za kisayansi kwa nini ilifanya vibaya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

CCM isifanye makosa kuwashika wanachama wake uchawi wakati hawajui uchawi.

Si kweli kwamba CCM ilifanya vibaya uchaguzi wa mwaka jana eti kwa sababu ilisalitiwa na baadhi ya wanachama wake. Huko ni kufumbia macho sababu za wazi kabisa zilizoifanya CCM kufanya vibaya katika uchaguzi huo, kiasi cha watu wengine kuamini kwamba ilishindwa uchaguzi huo.

Matokeo mabaya ya uchaguzi kwa upande wa CCM hayakusababishwa na wasaliti. Yalisababishwa na mambo mawili; kwanza, uteuzi mbovu wa wagombea katika chama, na pili, utendaji mbovu wa Serikali ya CCM.

Kwa upande wa uteuzi mbovu wa mgombea urais ndani ya CCM, sisi sote tulisikia kwamba mwenyekiti wa CCM alikwenda kwenye Mkutano Mkuu wa Uchaguzi akiwa na majina ya watu watano mfukoni mwake, aliokuwa amewateua bila kufuata taratibu za chama.

Kitendo hicho hakikuwaridhisha watu waliogombea nafasi hiyo na wafuasi wao. Kwa kweli baada ya uteuzi ule watu waliokuwa karibu na rais kama vile makamu wa rais na waziri mkuu wake ambao pia walikuwa wamegombea nafasi hiyo, hawakusikika tena.

Uteuzi ule uliokuwa wa upendeleo na kubebana, ulileta hasira kwa wote waliogombea nafasi ya urais baada ya kutoa shilingi milioni moja na kuzunguka nchi nzima kutafuta wadhamini na kukuta kwamba mwisho wa siku majina yao hayakujadiliwa!

Kitendo hicho ndicho kilichovuruga umoja ndani ya CCM na kwa kweli ndicho kilichosaliti chama.

Utendaji mbovu wa Serikali ya CCM iliyomaliza muda wake pia ulichangia kwa kiasi kikubwa kufanya vibaya kwa chama katika uchaguzi ule.

Chukua, kwa mfano, Dar es Salaam majimbo yote ya uchaguzi na kata zote zingeweza kuchukuliwa na watu wa Ukawa kama wasingeshindana wenyewe kwa wenyewe. Ni katika mazingira hayo, halmashauri za mitaa za Dar es Salaam zimechukuliwa na Ukawa.

Basi CCM itafanya makosa makubwa ikianza kufukuzana kwa madai ya usaliti, wakati ukweli uko wazi kuhusu kilichosababisha CCM kufanya vibaya katika uchaguzi uliopita.

By Jamhuri