1WAKAZI wa Jiji la Dar es Salaam wanaotumia kituo cha Mabasi cha Gerezani, Kariakoo kilichopo Wilaya ya Ilala wamevutiwa na mazingira bora ya kituo hicho, na baadhi wamependekeza magari ya mwendokasi yaende Mbagala, Ukonga, Mwenge na Buguruni.

 Wameitaka Serikali kuendelea kujenga vituo vya aina hiyo katika maeneo mbalimbali ambayo kuna changamoto ya kutokuwa na miundombinu bora ya vituo.

 Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofaufi, wakazi hao wanasema mazingira na mandhali ya kituo hicho ni mazuri, hali ambayo inawapa faraja kipindi chote wanapokuwa maeneo hayo.

 Faridi Mohamed (25), Mkazi wa Mbagala, Temeke, anasema kituo hicho ni jambo la kujivunia kwani awali walikuwa wanapata shida kutokana na  kutokuwa na kituo rasmi cha daladala za kawaida badala yake daladala hizo zinaegeshwa pembezoni mwa barabara.

“Kituo ni kizuri, kina hewa safi, mazigira yake yanapendeza. Naomba uongozi husika wa kituo hiki wakisimamie kikamilifu,    kwani kuna baadhi ya watu wameanza kutupa uchafu maeneo ambayo siyo rasmi,’’ anasema Mohamed.

 Mkazi wa Kitunda, Doto Kindole (39), anasema miongoni mwa vipaumbele vilivyoweka katika kituo hicho, ni swala la ulinzi kuzuia wapigadebe, usafiri wa baskeli na pikipiki ndani ya kituo.   

 “Kama kuna uwezekano naomba waweke vibao vinavyoelekeza sheria ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima, kwani watu wengine ni wageni na wanakuwa hawajui sheria za kituo hiki,’’ anasema Kindole.

 Philipo Njau (36) Mkazi wa Kipawa, Ilala anasema kituo hicho ni miongoni mwa vituo bora jijini Dar es Salaam, hiyo inatokana na kuwa na sehemu nyingi za kukaa na kupuzika tofauti na kituo cha Mawasiliano.

 Anasema ukiangalia vituo vya mabasi ni wakati  mwafaka kwa Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri kwa sababu ndio chanzo cha maendeleo ya uchumi katika taifa.

 Zainabu Ngusa (34), Mkazi Temeke anasema licha ya kituo hicho kuwa na mwonekano mzuri bado kuna changamoto ya ukosefu wa huduma ya migahawa yenye hadhi, hali ambayo inawapa wakati mgumu wasafiri wanaosubiri magari hapa.

Akizungumza na JAMHURI, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, anasema jiji linahitaji kupata miundombinu bora ya usafiri. Anasema katika uongozi wake vituo vya mabasi vitakuwa rafiki kwa watumiaji.

Anasema katika suala la maendeleo hasa  kuboresha vituo vya mabasi jijini  wakiwa pamoja  na halmashauri zote wamahusika kuratibu maeneo ya kujenga vituo hivyo huku Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi kavu (SUMATRA) wakiwa wanahusika moja kwa moja kupanga maeneo husika ya vituo vya mabasi.

Kupitia mradi wa mabasi yaendayo kasi (UDART) wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamekuwa wakinufaika kutokana na faida kadhaa zinazopatikana hasa kufika katika eneo husika kwa wakati.

Meya Mwita, anasema miundombinu bora ni njia ya pekee kufanikiwa katika maendeleo kwani asilimia kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam hasa wanaoishi maeneo ya barabara  ya Morogoro wamekuwa na furaha baada  kunufaika na UDART kutokana na kile kinachoelewa kuwahi kufika katika maeneo yao ya kazi tofauti na kipindi  cha nyuma.

 “Watngulizi wangu waliofanikiwa kubuni mradi huu wanapaswa kupongezwa licha ya kujitokeza changamoto kadha za uendeshaji ikiwemo maswala ya tiketi ambayo bado haujakaa sawa, lakini naamini kadri muda unavyozidi kwenda watazidi kuboresha na kupiga hatua mbele kimaendeleo katika jiji letu,” anasema Mwita.

Anasema kuboresha miundombinu ya barabara na  vituo vya mabasi  itakuwa ni chanzo cha kuwavutia wafanyabiashara mbalimbali kuja kuwekeza katika sekta ya usafirishaji.

“Nawasihi sana wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, waendelee kuituinza miundombinu ya UDART kwani itaendelea kuwasaidia wao pamoja na watoto, kuitunza iwe jukumu letu sote,’’ anasema Mwita.

  Mnufaika mwingine wa mradi huo, James Emmanuel, Mkazi wa Mbezi anasema usafiri huo umekuwa ni ahueni kubwa kwa wanyonge wengi. Yeye hutumia Sh 1050 kwa mzunguko mmoja, huku akitumia vizuri  muda wa safari, kutokana na kupungua kwa msongamano.

 Kutokana na ufanisi uliopatikana, baadhi ya wananchi wamependekeza Serikali ifute njia za daladala kwa barabara kuu za Kilwa inayotoka Mbagala kuja mjini, Ali Hassan Mwinyi inayotoka Mwenge kwenda Posta, Mandela – inayotoka Bandarini kwenda Ubungo na Nyerere inayotoka Ukonga kwenda Posta.

 “Haya magari ya kasi yakiingia kwenye njia hizi, watumiaji wa magari binafsi watapungua kwa asilimia 60 na hivyo kupunguza msongamamo. Tukisubiri wajenge vituo na barabara maalum, inaweza kuchukua hadi miaka 5 au 10 kabla hatujajenga barabara yenye viwango vya ile ya Morogoro,” anasema Simon Ndege, mkazi wa Mbagala.

By Jamhuri