Watano wafukuzwa kazi Benki ya Ushirika

Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Ushirika mkoani Kilimanjaro (KCBL) imewafukuza kazi maofisa wake watano akiwamo Meneja Mkuu wa benki hiyo, Joseph Kingazi, kwa tuhuma za kuhusika katika ufisadi wa mabilioni ya fedha.

Maofisa wengine wa benki hiyo waliofukuzwa kazi kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na  uongozi wa bodi hiyo ni aliyekuwa Meneja Mikopo, Ombeni Masaidi na Asha Kisega ambaye naye ni kutoka Idara ya Mikopo.

Wengine ni  Doe Mashinga aliyekuwa mtunza fedha na Ukundi Mmochi aliyekuwa katibu muhtasi wa meneja mkuu, na baada ya kufukuzwa kazi simu zao zimekuwa hazipatikani huku baadhi yao wakidaiwa kubadilisha namba za simu.

Kabla ya Kingazi kuwa meneja mkuu, alikuwa ndiye mhasibu mkuu wa benki hiyo na alipandishwa kushika nafasi hiyo kwa pendekezo la aliyekuwa meneja wa benki hiyo, Elizabeth Makwabe, sambamba na Ukundi Mmochi.

“Uongozi wa benki unapenda kuutangazia umma kuwa watajwa hapo juu si wafanyakazi tena wa Kilimanjaro Co- operative Bank Limited. Hivyo basi benki haitahusika na taarifa au miamala yoyote itakayofanywa na watu hawa,” imesema taarifa hiyo.

Kabla ya kufukuzwa maofisa hao walipewa barua za kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi na baada ya uchunguzi kukamilika, wakapewa barua za kufukuzwa.

Kufukuzwa kazi kwa maofisa hao kumehitimisha kelele za siku nyingi kutoka kwa baadhi ya wanahisa wa benki hiyo juu ya mwenendo usioridhisha wa benki uliotokana na usimamizi mbovu uliosababisha mtaji wa benki hiyo kuyumba.

Mwenyekiti wa Bodi ya KCBL, Gervas Machimu, pamoja na kukiri kufukuzwa kazi kwa wafanyakazi hao, hakuwa tayari kuingia kwa undani juu ya tuhuma zilizoisukuma benki hiyo kuchukua hatua husika.

Mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo aliyezungumza kwa sharti la kutotaka kutajwa jina lake gazetini, ameliambia JAMHURI kuwa maofisa hao wamefukuzwa kazi kutokana na kuhusika kwa namna fulani katika ufisadi wa mabilioni ya fedha ambao umeifanya benki hiyo kuyumba mara kwa mara.

Mjumbe huyo ametaja eneo ambalo limeiweka pabaya benki hiyo na kufikia hatua ya kusimamisha utoaji wa huduma ni Idara ya Mikopo ambapo maofisa hao wanatuhumiwa kujihusisha na utoaji wa mikopo usiozingatia taratibu za benki.

Ametolea mfano wa vyama vya ushirika wa mazao (AMCOS) 18 pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika cha Same (VUASU) ambavyo vilivuka na deni la zaidi ya shilingi bilioni 1.173 katika msimu wa 2016/2017, kwamba hadi sasa vyama hivyo vimeshindwa kurejesha mkopo huo.

“Kwa utaratibu chama kinapewa fedha kulingana na kiwango cha kahawa wanayokusanya, lakini vyama vingi vimepewa pesa nyingi isiyoendana na kiwango cha kahawa wanayotarajiwa kukusanya na matokeo yake wameshindwa kuzirejesha mpaka sasa,” amesema.

JAMHURI limeona orodha ya vyama hivyo na kiasi cha mkopo walichopewa na kiasi cha pesa kilichorejeshwa KCBL. Katika shilingi bilioni 1.9 zilizotolewa kwa vyama hivyo katika msimu huo, ni shilingi milioni 700 tu ndizo zilizorejeshwa hadi kufikia Juni 30, mwaka 2017, huku kiasi cha shilingi 1,173,869,049 zikiwa bado mikononi mwa vyama hivyo.

Vyama hivyo vya ushirika wa mazao ni miongoni mwa wanahisa 245 wa benki hiyo, wakiwamo pia watu binafsi 307 pamoja na Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na ilikuwa ikihudumia wilaya sita za Mkoa wa Kilimanjaro.

Benki hiyo inayomilikiwa kwa aslimia 69 na Chama Kikuu cha Ushirika  Kilimanjaro (KNCU) ilianzishwa mwaka 1996 ikiwa na lengo la kuwakwamua kiuchumi wakulima wa zao la kahawa mkoani humo kwa kunufaika na mikopo yenye riba nafuu kupitia vyama vyao vya msingi vya ushirika.

Januari mwaka jana, benki hiyo ilikuwa miongoni mwa benki tatu zilizopewa muda wa miezi sita na Benki Kuu (BoT) kutimiza matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji wa shilingi bilioni tano, lakini mpaka sasa benki hiyo imeshindwa kutimiza matakwa hayo.

Baada ya tangazo hilo la BoT, KNCU ilitangaza kuuza shamba lake la kahawa la Lerongo lililopo Wilaya ya Hai likiwa na ukubwa wa ekari 581 kwa ajili ya kuinasua benki hiyo kukwepa rungu la Benki Kuu.

Hata hivyo Januari 18, mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara alizuia uuzwaji wa shamba hilo kutokana na serikali kuwa katika uhakiki wa mali za ushirika na kubaini waliohujumu mali hizo.

Zuio hilo la waziri mkuu likahitimisha safari ya utoaji wa huduma katika benki hiyo huku wateja wenye amana katika benki hiyo wakipewa ukomo wa kuchukua fedha, ambapo kila mwenye amana aliruhusiwa kuchukua shilingi milioni mbili tu.