MwakyembeNamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuvusha salama mwaka 2015 na kutujaalia kuuanza mwaka 2016. Ni vema na haki kumshukuru Mungu wetu kwa kila hali na kila mahali maana yote tunayaweza kwa mapenzi yake na si tu kwa uwezo wetu wenyewe.

Kipekee tunamshukuru Mwenyezi Mungu maana Tanzania Bara imebahatika kuwa na ardhi takribani hekta zaidi ya milioni 89. Eneo hili limegawanywa kiutawala katika mikoa 26; wilaya zaidi ya 130; kata zaidi ya 3,000 na vijiji zaidi ya 12,000.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Tanzania Bara inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 43. Ardhi na watu ni rasilimali muhimu kwa nchi kuweza kujiletea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kutuasa kwamba ili nchi au taifa liweze kuwa na maendeleo linahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Kwa kuwa ardhi ya kutosha tunayo na rasilimali watu ipo ya kutosha, changamoto ni vipi vitu hivi viwili vinatumika kuleta maendeleo endelevu? 

Ili suala hili liweze kufanikiwa vizuri, hatuwezi kukwepa kuwapo kwa siasa safi na uongozi bora. Siasa na sera vinatoa dira na mwelekeo unaotakiwa kuliwezesha taifa kujiletea maendelo. Iwapo siasa na sera zitakuwa zenye mtazamo na malengo chanya kwa wengi, basi inakuwa heri kwa taifa kusonga mbele. Kusema kweli ukisoma sera za kisiasa kupitia vyama vya siasa pamoja na sera za kisekta katika Tanzania unavutiwa na mambo yaliyomo. Hii ni kutokana na maudhui yanayolenga kuinua hali ya maisha kwa kila Mtanzania mijini na vijijini.

Kwa mfano, Sera na Sheria za Ardhi kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi vimeweka bayana matumizi ya rasilimali ardhi kwa upande wa Bara. Kisera na kisheria matumizi katika ardhi yetu yameainishwa vizuri kwamba kuna ardhi ya vijiji; ipo ardhi ya maeneo ya majiji na miji; ipo ardhi iliyohifadhiwa kisheria kwa maslahi ya Taifa, kuna maeneo yametengwa kwa shughuli za uwekezaji na pengine ipo ardhi sehemu nyinginezo ambayo matumizi yake yanasimamiwa na Kamishna wa Ardhi.

Kwa ufupi na kwa uelewa wangu matumizi ya aina hizo za ardhi yanasimamiwa na sheria za sekta husika ikiwamo Sheria ya Usimamizi na Utunzaji wa Mazingira (Environmental Management Act (EMA), 2004) chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais (OMR). Mathalani, usimamizi na uwajibikaji kwa maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ni kwa mujibu wa sheria za sekta husika kama Hifadhi za Misitu chini ya Sheria ya Misitu, Hifadhi za Taifa chini ya Sheria ya TANAPA na Wanyamapori; Mapori ya Akiba (Game Reservesna Game Controlled areas) ni kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori; na kadhalika.

Kwa upande mwingine ipo sheria mahsusi kwa usimamizi na matumizi ya ardhi ya vijiji na sheria ya ardhi inayosimamia matumizi ya maeneo nje ya yale yaliyohifadhiwa na yaliyo chini ya miliki ya vijiji.

Kwa utaratibu huo mzuri, unashangaa kuona bado kuna mizengwe na mwingiliano mkubwa katika matumizi ya ardhi. Mara ngapi sehemu mbalimbali nchini tunasikia au kushuhudia ugomvi kati ya wakulima na wafugaji kuhusu matumizi ya maeneo kwa shughuli za kilimo au machunga?

Kwa nini hali hiyo inatokea kwa kukosa matumizi bora ya ardhi nchini hasa katika ardhi chini ya usimamizi wa Serikali za Vijiji. Miaka kama 10 iliyopita tumeshuhudia ugomvi kati ya wanaosimamia maeneo yaliyohifadhiwa kisheria. Hii inatokana na mwingiliano wa matumizi ya maeneo yaliyohifadhiwa na shughuli za kibinadamu.

Kimsingi ardhi iliyohifadhiwa kisheria inatakiwa itumike na kufanikisha malengo na shughuli zilizokusudiwa. Mathalani, kuhifadhi wanyamapori, kuhifadhi misitu na bioanuai; kuhifadhi vyanzo vya maji; kuhifadhi mikoko, ardhioevu na viumbe wa majini; kuhifadhi maeneo yanye rasilimali-kale na kadhalika. Iwapo mipaka ya maeneo husika inafahamika, inakuwaje binadamu asiheshimu mipaka iliyowekwa na badala yake anaingia katika maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya anavyotaka?

Ujangili umeshamiri nchini. Tembo na faru wengi wameuawa. Maeneo mengi ya misitu yaliyohifadhiwa kisheria yanavamiwa na kuharibiwa kutokana na kilimo, makazi na mifugo.

Watu wanafanya hivyo kwa uelewa kwamba sekta husika wakati mwingine hazina uwezo wa kuyasimamia maeneo yaliyo chini yake kwa kukosa wataalamu, vitendea kazi na rasilimali fedha.

Iwapo sheria zipo na watu wanajua hivyo, inakuwaje wengine hawaziheshimu? Mipaka ya Hifadhi za Taifa inaeleweka, mipaka ya Mapori ya Akiba inaeleweka; na kama mipaka ya misitu iliyohifadhiwa kisheria inafahamika, kwa nini wakulima na wafugaji wanaohama wavamie?

Kwanini mifugo ipelekwe katika Hifadhi za Taifa kama Serengeti au Ruaha au katika Msitu wa Hifadhi wa Biharamulo au Kazimzumbwi, kulikoni? Iwapo ardhi na rasilimali watu vipo, inakuwaje hali hii inajitokeza?

Mkanganyiko huu unatokea kwa sababu mbili kuu:

(i) Matumizi ya ardhi, iwe kwenye maeneo ya kuchungia mifugo, au kilimo ndani ya maeneo ya vijiji, si mazuri kwa kutozingatia misingi endelevu. Badala yake, ardhi inatumiwa ovyo kiasi cha kusababisha uharibifu mkubwa kwa mazingira. Maeneo mengi ya kilimo nchini yamekuwa jangwa. Watu wenye mifugo wanachunga badala ya kufuga. Mamia kwa maelfu ya mifugo yanalundikwa sehemu moja na matokeo yake ni kuharibu malisho.

Maeneo yenye miti yanakatwa na kuchomwa moto; matokeo yake ni uharibifu mkubwa kwa mazingira unaolazimisha wenye mifugo kuhamahama.

(ii) Msukumo wa kisiasa uliojaa maslahi binafsi umekuwa pia kichocheo kwa baadhi ya wananchi kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya wanavyotaka. Unapowakuta wako ndani ya eneo lililohifadhiwa unadhani pengine wapo na hawakujua kwamba ni eneo la hifadhi. Lakini unapowauliza wanajibu: “Tunajua ni eneo la hifadhi, lakini ‘fulani’ katuambia tuje tulime au tuchunge mifugo yetu na yeye ndiye atakayewajibika”.

Ukichunguza unakuta ni kiongozi mkuu wa kisiasa katika eneo husika au katika uongozi ngazi ya kata, jimbo, wilaya au mkoa. Juhudi za kuwaondoa zinapochukuliwa wanakuja juu na kusema: “Waacheni msiwabughudhi wanaganga njaa.” Hata hao waliojenga kwenye maeneo hatarishi kama Msimbazi au kwingineko, kumekuwa na jitihada za kuwaondoa, lakini kikwazo ni wanasiasa. Kwa kuwa wenzetu wamekuwa na sauti za juu na kusikilizwa, wale wanaohusika na usimamizi na utekelezaji wa sheria hukwama na kujikuta wanaacha mambo yaharibike.

Ardhi ipo na ikitumika vizuri kwa misingi endelevu Tanzania hatujafikia hatua ya kulalamika kwa kusema watu wamekuwa wengi sana kiasi cha ardhi kuwa ndogo. Hapana, ni kutotumia ardhi tuliyonayo kwa busara na kutumia teknolojia za kisasa kuzalisha mazao mengi; wachunga mifugo wakaweza kuwa na ardhi ambayo wanaitumia kwa busara na kufugia mifugo badala ya kuhama hama.

Wafuge na watunze mifugo kibiashara: Ufugaji uwe na tija ya kutosha na maeneo ya kufugia yaendelezwe mara kwa mara kuongeza lishe kama nyasi au mimea inayofaa kuliwa na mifugo (fodder plants). Ipo miti mingi inayofaa kuliwa na mifugo, lakini pia inaweza kurutubisha ardhi. Wataalamu wa kilimo, misitu na hifadhi ya mazingira wawasaidie wafugaji waweze kufuga kibiashara badala ya kukimbizana na mifugo.

Nimalizie kwa kushauri kuwa maeneo ya hifadhi kama Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu pamoja na Hifadhi za Misitu yaheshimiwe na kusiwepo shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo.

Tukifuata sheria, taratibu na kanuni hakutakuwapo na migongano wala malalamiko yasiyokuwa ya msingi. Bomoabomoa za sasa zinawakumba wengi, lakini kwa sehemu kubwa wanasiasa wamechangia. Niwaombe Watanzania wenzangu, wakiwamo wanasiasa na viongozi wetu kuzingatia sheria na ushauri wa kitaalamu. Mwananchi ukishauriwa kuwa sheria inakataza kufanya moja, mbili…tekeleza bila shuruti.

Mtu mwingine akikudanganya fikiria mara mbili na tafakari kwa kina nini hatima ya ushauri unaopewa maana mwishowe maumivu yatakuwa kwako. Hakuna haja ya kufyeka mazao ya wakulima iwapo wamelima kwenye maeneo sahihi au kukamata mifugo kama watakuwa wanafugia katika maeneo yaliyopangwa.

Ukipeleka mifugo katika Hifadhi za Taifa itakamatwa maana inakuwa katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria. Chungieni mifugo kwenye maeneo ya kufugia mifugo (rangelands) na si kinyume cha hapo. Sheria ya Mazingira inakataza kujenga kwenye maeneo hatarishi, karibu na vyanzo vya maji, mito na vijito. Kiuhalisia, shughuli za kibinadamu zinatakiwa ziwe umbali wa mita 60 kutoka kingo za mito, lakini unakuta sehemu nyingine nyumba zimejengwa hadi sentimeta chache. Chukua hatua haraka na epuka kubomolewa au kuondolewa kwa lazima. Wizara iwasaidie wafugaji kwa kuainisha maeneo ya kufugia na kuwamilikisha ili waweze kuyatunza kwa kuanzisha ranchi zao badala ya hali ya sasa ya kuhamahama kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine.

Ingawa siasa ya Taifa letu inasema kila Mtanzania anao uhuru wa kuishi mahali anakotaka alimradi havunji sheria za nchi, uhalisia wa mambo ni kuwa watu wanavunja sheria kwa kutojua au kwa makusudi.

Ni kweli kuna uhuru wa Mtanzania kuishi mahali popote anapotaka, lakini kikubwa SHERIA, TARATIBU na KANUNI ziheshimiwe na zifuatwe kikamilifu.

By Jamhuri