Katika sehemu ya kwanza ya makala hii, mwandishi alieleza kwa kina umuhimu kwa Watanzania wenyewe kuanza kuchimba madini, ili wafaidike nayo badala ya utaratibu wa sasa unaowanufaisha wageni zaidi. Endelea…

 

KUJIJENGEA UWEZO

 

Inawezekana tunaowaita wawekezaji au wataalamu wa kuchimba madini kutoka nje, iliwachukua muda mrefu kuweza kufikia hapo walipo. Lakini suala la muda mrefu siyo kikwazo ilimradi tu tuwe na dhamira kamili ya kujenga uwezo wetu wa ndani. Vilevile, tuondokane na mtazamo hasi kuwa sisi hatuwezi.

Kusema kweli tunaweza sana na hatuko tofauti na wale wanaotoka nje. Hao wa nje wameongezewa nguvu ya ziada ya kupata utaalamu na uwezo kifedha au kufikia kiwango cha wanaopewa sifa ya ‘wanakopesheka’ na kupatiwa mitaji kutoka kwenye taasisi za fedha nchini na za nje ya nchi.

Tujiulize, nani atatujengea uwezo wa kuyamudu barabara mazingira tuishimo kama si sisi wenyewe? Miaka 50 tangu tupate Uhuru si kipindi kifupi, ni muda wa kutosha. Je, ni miaka mingapi kwa mtu aliyehitimu shahada ya kwanza au aliyehitimu kidato cha sita na mwenye uwezo kiakili kuweza kusoma na kuwa mtaalamu wa miamba na uchimbaji wa madini? Je, ni fedha kiasi gani zinahitajika kuweza kumpata mtaalamu wa aina hiyo aliyebobea katika taaluma ya uchimbaji madini? Haya yote yasitutie hofu maana yamo ndani ya uwezo wetu kama Taifa.

Tukithubutu tutaweza. Kama wao wanaweza, kwa nini sisi tushindwe?  Mimi naamini tunaweza na uwezo wa kufanya hivo upo. Hapa ni suala la uamuzi tu wa tufanye nini na kwa faida ya nani. Iwapo mtazamo utakuwa ni watu binafsi kufaidika na rasilimali tulizo nazo, hapo dhana ya kujijengea uwezo kama nchi itakuwa haipo. Lakini iwapo tunadhamiria Taifa linufaike kwa maana kuwa rasilimali tulizo nazo yakiwamo madini ziwanufaishe wengi mijini na vijijini, basi hatuna budi kuchukua hatua za haraka kujenga uwezo na kudumisha uchumi wetu bila ya kuangalia wawekezaji kutoka nje.

Maana tutakuwa na ari, kasi na nguvu tosha kwa minajili ya kuwekeza sisi wenyewe na kwa faida yetu. Yote haya yanawezekana kwake aaminiye, lakini kwa wenye itikadi ya kutokuamini kuwa Afrika inaweza; hilo litabaki kuwa historia na hadithi za ‘sungura mjanja’.

Iwapo wawekezaji kutoka nje ya Tanzania wataona iko fursa kwao kuwekeza, waje milango itakuwa wazi; lakini wajue wakifanya hivyo iwe ni kwa faida ya wote: siyo wao ‘kuchukua kilicho chao mapema’ na hatimaye kutuachia mashimo makubwa yasiyofukiwa kwa kisingizio eti ‘wamelipa kodi na kutoa huduma nyingine za kijamii (corporate responsibilities).

Hivyo, vyote wafanye lakini na madini watakayoyapata Taifa lijue ni kiasi gani na madini hayo yawe ni faida kwa Watanzania siyo wao kugeuza kilicho chetu kikawa chao baada ya kuchimba na hatimaye kuuza na kusonga mbele huku wakituacha nyuma kwa mithili ya ‘4×4 by far’.

Mimi binafsi sioni kwa nini tushindwe wakati akili tunazo, rasilimali zipo na uwezo wa kifedha mkubwa tu upo. Kinachotakiwa hapa ni usimamizi madhubuti na wenye dhamira ya kweli kwa maendeleo ya Taifa letu.

Kinachotakiwa hapa ni moyo wa kuwekeza wenyewe kama Watanzania na tusisubiri kupokea kodi tu. Kwa kufanya hivyo tunajidumaza. Tufanye kweli, tutafanikiwa. Inawezekana chukua hatua. Ninyi ndiyo mliokalia usukani wa ‘mv Maendeleo Tanzania’ kwa kujenga uwezo wa Tanzania kunufaika na rasilimali madini kwa faida ya Watanzania wote.

Madini katika ardhi ya Tanzania siyo mali ya wawekezaji, bali ni mali yetu. Iweje wao waendelee kutajirika kwa kupata faida kubwa wakati walio wengi wetu wakibaki kuwa walalahoi? Je, ni sawa hiyo?

905 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!