Watanzania kwa jumla tuna kila sababu ya kuhakikisha dhana ya udini haipati mwanya wa kuvuruga ustawishaji na udumishaji wa amani, ambayo ndiyo msingi wa maendeleo nchini.

JAMHURI tunasema hivyo kutokana na viashiria vibaya vya vurugu zenye sura ya udini, vilivyoanza kuonekana katika siku za karibuni na kutishia amani na utulivu nchini.

 

Mfano, Ijumaa iliyopita, waumini wa dini ya Kiislamu, hususan wafuasi wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda, walijaribu kuvunja sheria za nchi kwa kuandamana bila kibali cha Jeshi la Polisi.

 

Maandamano hayo yalipangwa kuelekea Ikulu jijini Dar es Salaam, kuishinikiza Serikali imwachie huru Sheikh Ponda anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za uchochezi na wizi wa mali.

 

Hata hivyo, JAMHURI tunalipongeza jeshi hilo kwa kufanikiwa kuzuia azma ya kundi hilo la Kiislamu, na kurejesha hali ya kawaida pasipo kusababisha madhara ya kutisha.

 

Tukio hilo ni mwendelezo wa vitendo vya uvunjifu wa amani baada ya vurugu za kuchoma makanisa, kujeruhi watu na uporaji mali mbalimbali, zinazodaiwa kufanywa na kundi hilo la Kiislamu katika eneo la Mbagala, hivi karibuni.

 

Kwa upande wa Zanzibar, kundi la Kiislamu la Uamsho chini ya kiongozi wake, Sheikh Farid Ahmed, limeripotiwa kuhusika kumuua askari polisi, kuharibu makanisa sambamba na uporaji mali mbalimbali. Sisi JAMHURI hatuungi mkono na tunakemea vikali vitendo hivyo na wote wanaojihusisha navyo chini ya kivuli cha udini.

 

Tunatoa wito kwa vyombo vya dola na Watanzania kwa jumla, kushirikiana kupiga vita vitendo hivyo vinavyoashiria kutowesha amani na kuleta machafuko nchini. Watanzania tusikubali kuruhusu udini utupore amani inayoitangaza nchi yetu kimataifa, halafu tulazimike kutumia gharama kubwa kuirudisha.

 

JAMHURI tunaamini Watanzania wote ni ndugu tunaohitaji kuishi kwa upendo, amani, utulivu, kuheshimiana na kuvumiliana bila kuathiri imani zetu za kidini. Hatuoni sababu ya kuvurugana kwa hisia za udini.

1081 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!