Watuhumiwa mauaji, ujangili watoroka

Mahabusu watatu wa kesi za mauji na ujangili wametoroka katika Kituo cha Polisi Meatu mkoani Simiyu.

Polisi mkoani humo imethibitisha kuwapo kwa tukio hilo ;la Februari 19, mwaka huu. Watuhumiwa walitoroka baada ya kutoboa ukuta kwa kutumia ‘kitu chenye ncha kali’.

Polisi saba waliokuwapo kituoni wakati wa tukio hilo, wanashikiliwa kwa mahojiano.

Waliotoroka wametajwa kwa kuwa ni Chiluli Sitta (28), mkazi wa Kijiji cha Mwasungula, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji; na Pascal Masanja (18), mkulima mkazi wa Sapa na Masanja Ndengule (45) mkazi wa Sapa. Wawili hao wa mwisho ni baba na mtoto wake. Wanakabiliwa na kesi ya kukutwa na nyara za serikali kinyume cha sheria.

Polisi wameeleza kuwa mahabusu hao walikuwa wakisubiri kupelekwa katika Gereza la Mahabusu Wilaya ya Maswa.

Askari saba waliokuwa kazini ni D. 5582 CPL Peter (NCO wa zamu), F. 9840 D/C Hussein CID, G. 4806 PC John, G.8602 PC Yassin na WP. 11257 PC Khadija, G. 8371 PC Adam na H. 8410 PC Kher.

“Tukio limekaguliwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu SSP Majaliwa, RCO SSP Shana na Mkuu wa Polisi Meatu, SSP Debora Daud Magiligimba na RCIO ASP Kyando,” kimesema chanzo chetu.