Mhariri

 

Kwanza tunampongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kwa jitihada anazozifanya za kusafisha Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake kwa jumla kwa kuondoa uozo uliokuwamo ndani kwa kipindi kirefu.

 

Wakati jitihanda hizo zikifanyika, Waziri huyo kwa kutokana na barua ambazo zimesambazwa kwa kampuni za uwindaji wa kitalii juu ya Leseni za Uwindaji Bingwa (Professional Hunters License), kwa wazawa na wageni, barua hiyo inatengua Sheria Na. 49 (1) ya Sheria Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009 ambayo utekelezaji wake ulianza msimu wa uwindaji wa mwaka 2010.

 

Sheria imebainisha wazi na bila shaka Waziri aliyemtangulia (Ezekiel Maige) aliiona yafaa; inasema kwa Mwindaji Bingwa Mgeni (Non-Citizen Professional Hunter) akipata safari ya kuendesha kampuni nyingine inabidi arudishe leseni na kibali cha kufanya kazi (work permit) kwa mwajiri wake wa kwanza na kwenda kuanza upya kwa mwajiri wa pili. Hii ilisaidia kwa Wawindaji Bingwa Wazawa kuongeza wigo wa kazi na kipato, maana kwake ilitakiwa kupata barua ya kutokumzuia kutoka kwa mwajiri wake na kwenda kuendesha safari  kwenye kampuni nyingine yoyote (a letter of no objection).

 

Ikumbukwe kuwa kupendeleana wageni kwa wageni ni mkubwa na uko wazi, na kuweka mizani sawa kwa wawindaji bingwa wazawa na wageni ni kuwafanya wazawa kuwa watazamaji ndani ya sekta hii, hata kama Wizara itataka kupata orodha ya uwiano wa asilimia 50 ya wawindaji bingwa wazawa na wageni kwa kila kampuni ya uwindaji  wa kitalii, bado huyu mwindaji bingwa mzawa hatakuwa na chake, maana wao watapeana safari zote ndefu na yeye  kama akilalamika zaidi anaweza kupewa safari fupi moja tu ambayo (a 10 day safari). Mwisho, kwa kisingizio cha hali ya uchumi mbaya duniani au Ulaya (Global Economic crisis or Eurozone crisis) Mwindaji Bingwa huyu ataishia kujenga kambi na doria tu.

 

Tunao uzoefu ambao bado unaendelea  kwa kampuni zilizovaa uzalendo bandia kwa kuajiri wawindaji bingwa wazawa kinadharia, na si kivitendo ambao wanaishia kuendesha safari moja.

 

Tuna hakika Wizara haitafanya uhakiki wa leseni za kuwindia kuwa ni ngapi zimebeba majina ya wazawa, na ni ngapi za wageni wakati wa marejesho. Hii ni kazi ngumu.

 

Tunamuomba Waziri Kagasheki akae na bodi yake ya ushauri na kutafakari zaidi faida ya sheria hii kwa wazawa.

 

 

Mwindaji Bingwa

Arusha

By Jamhuri