Serikali imetolea majibu kauli za Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na ile ya Umoja wa Ulaya (EU) ambazo kwa nyakati tofauti zilionyesha kuwa kuna changamoto katika masuala ya ulinzi nchini wakitolea mifano ya kutoweka kwa baadhi ya watu pamoja na kukamatwa/kufungwa kwa wanasiasa.

Aidha, serikali pia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imetoa majibu kuhusu madai kwamba imekiuka kanuni za vikwazo vya kisilaha za Umoja wa Mataifa (UN) ilizoiwekea Korea Kaskazini.

Katika kujibu tuhuma hiyo, Waziri Balozi Mahiga kwenye taarifa aliyoitoa Machi 2, 2018 ameeleza kwamba, Tanzania itaendelea kuheshimu vikwanzo ambavyo UN umeiwekea Korea Kaskazini.

Kuhusu suala la awali, serikali imesema kuwa mabalozi hawa wameonyesha kutokuelewa hali ya kisiasa inayoendelea nchini na changamoto za kisiasa ambazo serikali imepitia kwa kipindi cha miezi 18 iliyopita ambacho kilikuwa kipindi kibaya zaidi.

Balozi Mahiga amesema kwamba ni jambo la kawaida kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa chini, kutoa ripoti kuhusu hali ya kisiasa na usalama kwa nchi zao, lakini, serikali inashangazwa na ukimya uliokuwa umetanda miongoni mwa balozi hizo katika mauaji yaliyokuwa yakiendelea Wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji, lakini sasa hali imetulia kule, ndio wanajitokeza na kuzungumzia masuala ya usalama.

Mauaji yaliyotokea katika wilaya za Mkoa wa Pwani, kwa kiasi kikubwa yalihusisha wananchama wa CCM, na wananchi wasiokuwa na hatia. Licha ya msisitizo mkubwa wa matukio haya katika vyombo vya habari vya ndani, hakuna balozi au mshirika yeyote aliyetoa neno kuzungumzia au kulaani mauji hayo, aliandika Balozi Mahiga.

Amesema kuwa, kumekuwapo na mbinu mbalimbali za kuichafua serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt Magufuli, na hivyo ni vyema mabalozi wakaelewa mbinu hizo kabla ya kutoa taarifa ambazo wakati mwingine sio za kweli, au za kuibua hisia kali miongoni mwa wananchi.

Wizara imesema kwamba, mabalozi wanakaribishwa katika meza ya majadiliano pale wanapoona tukio ambao si sahihi ili waweze kupewa majibu yenye ufasaha, lakini pia wakati huo huo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kupata majibu kuhusu mauaji ya raia ambayo yanahisishwa na siasa.

1557 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!