*Alitaka zigharimie mashindano ya Miss East Africa


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ameingia katika kashfa mpya baada ya JAMHURI kufanikiwa kupata nyaraka zinazoonyesha namna anavyolishinikiza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) litumie Sh milioni 560 kudhamini mashindano ya urembo ya Miss East Africa.

Wandaaji wa mashindano hayo wamemtumia Nyalandu kufanikisha maombi yao, na haraka haraka, Nyalandu ameiandikia barua Tanapa akitaka itoe fedha hizo ambazo ni sawa na dola 350,000.

 

Nyalandu anashinikiza malipo hayo kwa kigezo kwamba mashindano hayo yatasaidia kutangaza vivutio vya utalii nchini Tanzania na kuwavuta wageni wengi kuzuru nchini.

 

Katika barua yao ya mapendekezo ya kupewa kiasi hicho cha fedha, wandaaji wa mashindano hayo walimtumia Nyalandu kwa matarajio kwamba wangefanikiwa.

 

Hata hivyo, habari za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya Bodi ya Tanapa, zimesema chombo hicho kimeungana na msimamo wa menejimenti wa kukataa kutoa kiasi hicho cha fedha.

 

Msimamo wa Bodi ya Tanapa ni kwamba fedha hizo ni nyingi mno kutumika kudhamini mashindano ambayo kimsingi yanaonekana kutokuwa na tija moja kwa moja katika ukuzaji sekta ya utalii nchini.

 

“Uongozi uliona kiwango kile ni kikubwa mno, ikaonekana wazi kuwa fedha hizo haziwezi kutolewa hasa kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili Watanzania.

 

“Kuna changamoto ya wanafunzi kukosa madawati, vyumba vya madarasa, walimu hawana nyumba, hakuna maabara za kutosha, watu hawana maji wala barabara za uhakika katika maeneo yanayozunguka hifadhi.

 

“Ungekuwa uwendawazimu wa hali ya juu kukubali Sh milioni 560 zitumike kwenye mashindano ya urembo. Watanzania wasingetuelewa kabisa,” kimesema chanzo chetu kutoka ndani ya Bodi ya Tanapa.

 

Baada ya kukataliwa maombi hayo, Nyalandu anasemakana kukasirishwa mno na uamuzi wa Bodi ya Tanapa, kiasi cha kuapa ‘kuwashughulikia’ wale wote waliomkwamisha.

 

Chanzo cha habari kimesema ni kwa mtiririko huo, Naibu Waziri huyo kijana aliamua kuibua suala la Ahsante Tours na mara moja akapandisha hasira kwa kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuanza kuchunguza rushwa ndani ya Tanapa.

 

Ahsante Tours ambao walikuwa wakidaiwa dola 39,000 baada ya kuwa wamekopa dola 70,000 kutoka Tanapa waliishia kulipa dola 31,000 tu na kukalia deni lililosalia.

 

Kampuni hiyo ilitumia ukaribu wao kwa Nyalandu kukwamisha uamuzi wa Bodi ya Tanapa wa kuizuia kampuni hiyo kujihusisha na biashara ya usafirishaji watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA).

 

Kwa kujiamini, ilhali akitambua kuwa alikuwa akivunja kanuni za utendaji kazi, Nyalandu akaiamuru Tanapa iifungulie kampuni hiyo kwa kigezo kwamba kufungwa kwake kungeikosesha Serikali mapato ya mamilioni ya dola na ajira kwa Watanzania zaidi ya 600. Tanapa iligoma kupokea maelekezo haya.

 

Wakati  Nyalandu akitoa tambo hizo, ilibainika kuwa Waziri wake, Balozi Khamis Kagasheki hakuwa na taarifa zozote kuhusu Ahsante Tours; na akashangazwa na msimamo wa Naibu wake wa kutaka kampuni hiyo iendelee na kazi licha ya kudaiwa fedha za umma.

 

Lakini hakuwa Kagasheki pekee aliyeshangazwa na msimamo huo, bali hata Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli ambaye ameilipua Kampuni ya Ahsante Tours.

 

Lembeli ambaye pia ni Mbunge wa Kahama (CCM), mbele ya Balozi Kagasheki alisema  kuwa kampuni hiyo imekubuhu kwa kupitisha wageni kinyemela.

 

“Hii kampuni ndiyo notorious (imekubuhu) kwa kuiba njia… wanaoingiza watu kinyemela huko ndani na Tour Operators (kampuni za utalii) zingine zinafahamu,” alisema.

Aliongeza: “Wenzao wanaituhumu hii kampuni kuwa ni bingwa wa kuiba njia sasa wamebanwa ndiyo hayo yameanza kujitokeza.”

 

Waziri Kagasheki, akionekana kushitushwa na taarifa hiyo, alimgeukia Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi na kumuuliza kama Shirika lina taarifa hizo, na yeye akakiri.

 

Balozi Kagasheki akasema, “ Kama ni kweli basi tuachane na kampuni hii.”

Utaratibu unataka kampuni ya utalii inayotaka kupandisha mgeni mlimani kulipia kwa kadi kupitia tawi lolote la CRDB wakati kwa wanaotembelea mbuga za wanyama hulipia kupitia Exim, lakini kampuni hii inakiuka utaratibu huu.

 

Chini ya utaratibu huo, watalii binafsi ambao wana kadi za Visa au Master Card wanaweza kulipia ada zao moja kwa moja katika vituo vilivyopo kwenye malango ya kuingia katika hifadhi hizo.

 

Kampuni hiyo ya mjini Moshi ilifungiwa baada ya kupitisha watalii katika hifadhi mbalimbali nchini bila kulipa ada na deni hilo kufikia dola 80,000 za Marekani sawa na Sh milioni 155.

 

Kwa upande wake, JAMHURI hadi inakwenda mitamboni ilishindwa kumpata Nyalandu kwani simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa, na hata alipopelekwa ujumbe mfupi wa maandishi, hakujibu.

 

Ahsante Tours waomba radhi, walipa deni

Msimamo wa menejimenti na Bodi ya Tanapa; uamuzi wa Waziri Kagasheki pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, vimesaidia kuifanya Ahsante Tours iandike barua ya kuomba radhi na kulipa deni lote.

 

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Desemba 12, mwaka huu, baada ya kuona mambo yamekuwa magumu, kampuni hiyo iliiandikia barua Tanapa ikiomba radhi kwa yote yaliyotokea, na kuahidi kulipa deni lake.

 

Katika barua hiyo, waliomba wasipelekwe mahakamani kama ulivyokuwa msimamo wa Bodi ya Tanapa.

 

Desemba 17, mwaka huu Ahsante Tours iliweza kuilipa Tanapa deni hilo la dola 39,000 za Marekani ambazo ni sawa na Sh milioni 62.

 

“Hawa fedha walikuwa nazo, si kwamba walikuwa wanashindwa kuzilipa, lakini kiburi walikipata kutoka kwa Nyalandu, tena kwa kuona kuwa hili ni shirika la umma, kiburi kikazidi. Utaratibu huu wa kudhani mashirika ya umma ni ya kuchotwa tu ndiyo ulioua mashirika yetu mengi nchini,” kimesema chanzo chetu.

 

Taarifa hizo zinamaliza upotoshaji ulioenezwa kwamba Ahsante Tours imeruhusiwa kuendelea na shughuli zake baada ya vitisho vya Nyalandu.

 

 

By Jamhuri