*Asisitiza mgawo sawa wa rasilimali

Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, ni Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii. Mei 25, mwaka huu alichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini. Pamoja na mambo mengine, aliitaka Serikali itoe mgawo stahiki wa mapato kwa maeneo yenye rasilimali. Anaamini mawazo yake yanaweza kuwa tiba kwa kuepusha nchi na machafuko kama yale yanayofukuta mkoani Mtwara. Ifuatayo ni hotuba yake, neno kwa neno.

Naomba leo nianze kwa kumshauri Mhe Waziri. Mwaka jana nilitoa ushauri kwa Naibu Waziri, lakini wakati huu, Roho Mtakatifu ameniongoza na kunielekeza nimshauri Waziri mwenyewe kutokana na hali ilivyo hivi sasa hapa nchini kuhusu rasilimali. Namshauri kaka yangu Profesa Muhongo kwa nia njema na kwa lengo la kumsaidia na kuisaidia Serikali. Maandiko Matakatifu yanasema, “Mashauri ya moyoni ni kama kilindi, lakini mwenye ufahamu atayateka” (Mithali 20:09). Nitamshauri Mheshimiwa Waziri kwenye maeneo mawili – kuhusu ‘utoaji wa ahadi’ na ‘manufaa ya rasilimali zetu kwa wananchi’.

 

Kuhusu ahadi, namshauri  Mheshimiwa Waziri kwamba, asitoe tena ahadi. Huu si wakati wa kufanya hivyo. Mwaka 2010, sisi wagombea wa CCM tulitoa ahadi mbalimbali ambazo ziko kwenye Ilani yetu ya CCM. Ahadi hizo ndizo zilikuwa msingi wa sisi kuchaguliwa. Mtekelezaji wa ahadi hizo ni Serikali kupitia bajeti ya kila mwaka.

 

Mwaka jana Mheshimiwa Waziri, kwa mfano katika suala la umeme na hasa kwa jimbo langu la Msalala na Wilaya ya Kahama, alikuja na orodha na ramani za vijiji vitakavyopata umeme kama ifuatavyo:-

 

Jimbo la Msalala alisema vijiji 11 vingepata umeme kupitia miradi miwili ya Electricity V na REA. Vijiji vinne  vya Lunguya, Ikinda, Shilela na Segese alisema vingepata umeme kupitia mpango wa Electricity V, ambao ni mpango unaohusisha kupeleka umeme hadi wilaya za Bukombe na Mbogwe kutokea Ilogi (jimboni kwangu). Mradi huo ambao ni mradi wa zamani tangu 2008 haujaanza kutekelezwa, japo tumesikia mkandarasi amepatikana na kazi itaanza Julai 2013! Hatukutegemea jibu hili. Tulitegemea leo kuona mkandarasi yuko ‘site’ na nguzo zikichimbiwa au hatua nzuri zaidi ya hiyo, lakini sivyo!

 

Vijiji 7 vya Nyambula, Nyamigege, Busangi, Ntobo, Chela, Ngaya na Bulige alivitaja kuwa vingepata umeme kupitia REA. Hakuna hata kimoja kilichopata umeme.

 

Kahama Mjini, Kagongwa na Isaka kuna tatizo la muda mrefu la umeme kukatika mara kwa mara kutokana na uchakavu wa njia ya umeme kutoka Ibadakuli hadi Kahama, km 127. Tuliomba na kuahidiwa kuunganishwa na umeme mkubwa wa Buzwagi ambapo kiasi cha Sh bilioni 10 zilitajwa kuwa zingetumika kuweka kituo kidogo cha kupozea umeme toka Buzwagi na kuimarisha miundombinu. Haijafanyika.

 

Leo, Mheshimwa Waziri amekuja na orodha ile ile na ramani zile zile za mwaka jana! Juzi baada ya Waziri kusoma hotuba yake na kutoa ramani hizi, baadhi ya wananchi walinipigia na kuniulizia kuhusu Hotuba ya Waziri na utekelezaji wa ahadi zake za mwaka jana, niliwaambia kuwa ametupatia tena ramani na orodha! Wananchi wakaniambia, mwambie ‘tunataka umeme, hatutaki ramani’. Hivyo, Mheshimiwa Spika, naomba Waziri asitoe ahadi. Tulitegemea leo atuambie katika vijiji 11 amepeleka umeme vijiji vingapi na kwa nini ameshindwa kupeleka vijiji vote 11 kama alivyoahidi mwaka jana. Tunataka majibu ya kina juu ya utekelezaji wa ahadi na si ahadi mpya.

 

Mgawanyo wa rasilimali za Taifa

Ushauri wa pili kwa Waziri ni kuhusu mgawanyo wa rasilimali za Taifa na maana ya kauli na yanayotokea Mtwara. Ujumbe toka Mtwara ni kuwa Watanzania hawako tayari tena kuachiwa mashimo! Nilivyowaelewa mimi wananchi wa Mtwara, si kwamba wanataka gesi yote ibaki Mtwara, la hasha! Wanataka wajue WATANUFAIKAJE na gesi. Kwa lugha rahisi wananchi hawa wanasema, wanajua kuwa gesi inatakiwa inufaishe Taifa kwa kusafirishwa hadi Dar es Salaam, lakini wao watanufaikaje? Wanataka kujua ‘mgao wao’ ni nini?

 

Kilio cha wananchi kwenye maeneo yenye rasilimali, si cha Mtwara peke yake. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais mwaka 2008 aliniteua kuwa mjumbe katika tume ya kupitia upya sera, sheria na mikataba ya madini ili kuishauri Serikali namna ya kuondoa malalamiko ya wananchi kuwa madini hayawanufaishi! Kuundwa kwa tume ile kulitokana na ukweli kuwa tayari kulikuwapo na malalamiko kama ya Mtwara, japo si ya kutumia njia kama iliyotumika Mtwara.

 

Tume ya Bomani ilizungukia maeneo yote yenye rasilimali za madini na kuzungumza na wananchi. Tulifanya mikutano ya hadhara Geita, Bulyanhulu, Kiwira, Mererani na kadhalika. Sehemu zote hizi na nyingine, wananchi walisema ‘wanataka wapate mgawo wa mrabaha pamoja na manufaa zaidi kutokana na rasilimali zilizoko maeneo yao’.

 

Tume ya Bomani ilitembelea nchi nyingine duniani ili kujifunza namna nchi hizo zinavyosimamia na kugawa manufaa ya rasilimali kwa wananchi wao. Sehemu zote tulizotembelea hatukuona nchi yenye mfumo kama wa Tanzania, ambako rasilimali hutumika bila kipaumbele kwenye maeneo zinapotoka! Ndipo Tume ya Bomani ikapendekeza, pamoja na mambo mengine, kwamba mrabaha ugawanywe baina ya Serikali Kuu (asilimia 60) na Halmashauri/Wilaya pale madini yalipo (asilimia 40). Ushauri huu ulitokana na uzoefu tulioupata kwa wenzetu na ulitokana na kilio cha wananchi tuliozungumza nao. Hivyo, kilio cha wananchi wa Mtwara si kigeni na ninaamini, ushauri wa Tume ya Bomani ukitekelezwa, hakutakuwa na malalamiko.

 

Tunaposema tunataka manufaa ya rasilimali zetu hatumaanishi Taifa lisipate, tunataka tugawane. Kwani:-

 

Ndivyo ilivyo kote duniani na wameendelea kuwa mataifa yenye umoja. Hoja ya kwamba tukigawana rasilimali kutapunguza utaifa si ya kweli. Nchi kama Kenya, India, Marekani, China, Afrika Kusini na kadhalika wako hivyo na wameendelea kuwa mataifa imara.

 

Tume ya Bomani iliona na kupendekeza mrabaha usiende wote Hazina, kiasi cha asilimia 40 kibaki kwenye wilaya.

 

Hapa kwetu, mbona kwenye rasilimali nyingine tunafanya? Wanyamapori, kwa mfano, tunasema asilimia 25 ya mapato yatokanayo na uwindaji wa kitalii yabaki kwenye maeneo ya uwindaji. Tumefanya hivyo na Taifa limeendelea kuwa moja?

 

Tuwasikilizeni wananchi na tusiendelee kuwaudhi na kuwasononesha. Wasukuma, kwa mfano, si wapole wala si wajinga kama inavyodhaniwa. Hawapendi na hawajakubali kuona Mwadui inajenga London na Johannesburg na kuacha Shinyanga ilivyo.

 

Hawapendi kuona Tulawaka hadi inafungwa mwaka huu imejenga Toronto na kuiacha Biharamulo na umaskini uliopo. Hawapendi kuona Golden Pride (Resolute) ikijenga Adelaide, Perth (Australia) na kuiacha Nzega ilivyo! Hawapendi kuona Kahama iko ilivyo (bila lami, madawati, maji n.k.) huku Bulyanhulu na Buzwagi ikineemesha walioweka fedha na wanaouza bidhaa (kemikali, mitambo n.k.) kutoka Toronto na London.

 

Hawapendi kabisa kuona Geita ikibaki ilivyo huku madini ya hapo yakijenga Johannesburg, Accra na London. Watu hawa ni WAVUMILIVU, si wapole wala wajinga. Na Uvumilivu una mwisho! Hivi sasa kutokana na utandawazi, wanaona na kusikia Mtwara wanapata punguzo la asilimia 50 kuunganishiwa umeme, wanajengewa viwanda, wanalipwa asilimia 0.3 service levy n.k. Yanayotokea Mtwara yanawachochea nao kudai, na mbaya zaidi, tunawalazimisha kudai kwa mbinu tofauti na zile walizokuwa wakitumia siku zote bila mafanikio.

 

Naishauri sana Serikali, ione ukweli juu ya kugawana rasilimali hizi baina ya “taifa, wananchi jirani na wawekezaji”. Utatu huu uwe utatu mtakatifu wa manufaa. Naishauri Serikali, ikubali mapendekezo ya Tume ya Bomani au kama haiamini, basi unahitajika mjadala mpana, huru na wa kweli na maamuzi magumu na ya haraka yafanywe ya kuziondolea masononeko jamii zilizo jirani na rasilimali.

 

TUSIFANYE UWEPO WA RASILIMALI KWENYE ENEO FULANI KUWA BALAA, BALI IWE BARAKA KWENYE ENEO HILO.

By Jamhuri