Tanzania imetajwa kufanya vizuri katika kukomesha mauaji dhidi ya watu wenye ualbino.

Mwaka 2006 Tanzania iliingia kwenye historia mbaya baada ya watu hao kuanza kuuawa kwa imani za kishirikina.

Takwimu zilizotolewa Septemba 21, 2014 na Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) zilibainisha kuwa mwaka 2006 hadi 2014, watu 74 walipoteza maisha kwa mikasa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, 56 walinusurika kifo na kati ya hao 11 wameachwa na ulemavu wa kudumu.

Kulingana na TAS, makaburi 18 ya watu hao wenye ualbino yamefukuliwa na viungo vyao vilikuwa vikitumiwa na waganga wa kienyeji kutapeli watu.

Uchunguzi unabainisha kuwa baadhi ya raia kutoka mataifa tofauti ya kigeni wamekuwa wakizuru Tanzania kujifunza mbinu za kukomesha madhila hayo.

Eneo la Kanda ya Ziwa ndilo linalotajwa kuwahi kukumbwa zaidi na mikasa hiyo, ingawa kwa sasa imekoma baada ya jamii kuelimika.

Hivi karibuni ujumbe wa watu 10 kutoka mataifa saba ya Bara la Afrika na Ulaya, umezuru Tanzania kujifunza mbinu ilizotumia kukomesha mauaji ya watu hao.

Ujumbe huo ni kutoka nchi za Zimbabwe, Uganda, Zambia, Kenya, Malawi, Burundi na Uholanzi.

Katika wiki kadhaa zilizopita, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewahi kuzungumzia suala la usalama wa raia wote nchini.

“Kazi yetu ni kulinda raia na mali zao. Vyombo vya dola vipo imara kukabiliana na mhalifu wa aina yoyote atakayejaribu kutishia usalama wa nchi,” amesema Waziri Lugola.

Kutokana na kauli hali hiyo, Shirika la Kimataifa la Under The Same Sun (UTSS) lenye makazi yake nchini Canada limesema Tanzania imepiga hatua kukomesha mauaji hayo.

“Mwaka 2008 kulikuwa na matukio 40 yaliyoripotiwa juu ya ukatili dhidi ya wenye ualbino. Mwaka 2018 yameripotiwa matukio manane tu. Sasa utaona kutoka matukio 40 hadi manane, huu ni ushindi wa nchi, ni ushindi wa dunia,” amesema Rais wa UTSS Peter Ash.

Amesema ni vema tatizo la mauaji na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ualbino liendelee kubaki historia, lisijirudie.

“Tupendane sote,” amesema Ash alipozungumza na wanahabari jijini Mwanza kwenye kilele cha Summer Camp 2019.

UTSS iliyoasisiwa mwaka 2009 inahusika kupiga vita mauaji ya watu wenye ualbino.

Mwaka huu shirika hilo limetimiza miaka 10 tangu kuasisiwa kwake, na nguvu zaidi imeelekezwa kuisaidia jamii hiyo kwa njia ya utoaji elimu.

Ash amesema litakuwa jambo jema Tanzania ikiwa ya kwanza duniani kupata rais wa nchi mwenye ualbino siku moja.

Wakati hali ikiwa hivyo hapa nchini, taarifa zinafichua kuwa katika nchi za Malawi, Zimbabwe na Zambia mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino yameendelea kuripotiwa.

Ash ameueleza ulimwengu kuwa watoto 400 wenye ualbino wanasomeshwa na UTSS hapa Tanzania huku wakinufaika pia na mpango wa matibabu.

“Unyanyapaa dhidi ya watu wenye ualbino itakuwa ni historia iliyofifia,” rais huyo wa UTSS ambaye pia ni mtu mwenye ualbino ameongeza.

Katika hatua nyingine, kiongozi wa dini kutoka Canada, Brad Sumner, ameshauri watu wenye ualbino washirikishwe pia kwenye uimbaji wa kwaya.

“Hata ngoma tucheze nao. Wanajua kucheza,” amesema Sumner.

19 kunyongwa

Taarifa zilizopo kwenye mitandao ya kijamii zinasema watu 19 wamehukumiwa kifo baada ya mahakama nchini kuwakuta na hatia ya mauaji ya watu hao wenye ualbino.

Taarifa hizo zilizomkariri Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, zinasema zaidi ya watu 130 walikamatwa wakidaiwa kuhusika katika mauaji ya watu hao, kati ya mwaka 2006 na 2015.

Nchi za Afrika Mashariki, ikiwamo Burundi na Kenya zimewahi kukumbwa na mashambulizi hayo.

Berthasia Patrick, Mkurugenzi Mtendaji wa UTSS Tanzania, amesema watu wenye ulemavu wa aina yoyote hawapaswi kufanyiwa unyanyapaa bali kuheshimiwa.

Mafunzo yameshaanza kutolewa na UTSS yakiwashirikisha wadau kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, lengo ni kueneza kampeni ya kutokomeza simanzi kwa jamii hiyo.

Kulingana na Berthasia, watu wenye ualbino wanatakiwa kuheshimiwa na kushirikishwa katika masuala ya kijamii, wakati taifa likiwa katika mwelekeo wa uchumi wa kati na viwanda.

“Hakuna tena mauaji. Tuimarishe furaha yetu sote,” Berthasia, Mkurugenzi wa UTSS Tanzania amesema.

Ameeleza UTSS kwa kutambua umuhimu wa jamii hiyo katika maendeleo, imekuwa ikitoa ufadhili wa masomo dhidi yao.

Tayari kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kulainisha ngozi za wenye ualbino kimeshajengwa nchini.

“Hiki kiwanda kipo KCMC Mkoa wa Kilimanjaro. Tunasambaza na kugawa haya mafuta kwa wanafunzi tunaowahudumia bure,” amesema Berthasia. Ameshauri watu wenye ulemavu waitwe kwa majina au vyeo vyao.

“Kama humjui jina muite kaka, dada, mdogo wangu au mkubwa wangu,” amesisitiza Berthasia.

Bennet Phunyanya, kutoka Chama cha Watu wenye Ualbino Zambia, amewaambia waandishi wa habari jijini Mwanza kuwa usalama dhidi ya jamii hiyo lazima utiliwe mkazo zaidi.

Amesema bado kuna wasiwasi juu ya usalama wa watu wenye ualbino nchini Zambia na Afrika kwa ujumla.

“Tumeelezwa takriban watu wenye ualbino 20 hawajulikani walipo,” Phunyanya amesema.

Mkurugenzi wa taasisi ya kimataifa ya Josephat Tona Foundation Europe (JTFE), Josephat Tonna, amesema waliohusika na mauaji ya raia hao lazima washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Alfred Kapole, Kiongozi wa Jumuiya ya Watu wenye Ualbino Mkoa wa Mwanza (TAS), ameshauri nchi za Kiafrika kuiwekea jamii hiyo mazingira rafiki ya kiuchumi na ajira ili kuinusuru katika maradhi ya kansa ya ngozi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta ya MOIL, Altaf Hirani Mansoor, kwa upande wake amesema ataendelea kupiga vita manyanyaso kwa jamii.

“Nitaendelea kuunga mkono mapambano ya kujenga amani na usalama wa raia katika ukanda huu,” amesema Mansoor ambaye ni Mlezi wa Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS) Mkoa wa Mwanza.

Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu, Herbert Temba, amesema wamekuwa wakitenga bajeti kusaidia jamii hiyo yenye ualbino.

“Tumeweza kutoa elimu ya uelewa Kata ya Dutwa, Nkololo, Sapiwi, Ngulyati na Kasoli. Tumenunua na kuwapatia simu 25 ili wawe wanatoa taarifa,” ameeleza Temba.

Mwalimu Mahenda Kulwa kutoka Mkoa wa Shinyanga amesema jamii imefarijika kuona mapambano ya kumlinda mtu mwenye ualbino, yamefanikiwa zaidi.

“Sisi watu wenye ualbino ingawa tuna uoni hafifu, lakini tuna uwezo mkubwa kielimu kuzidi hata wengine. Tumefanikiwa. Tumeshinda sote,” amesema Kulwa.

Clara Maliwa ametoa ushuhuda wa simanzi iliyompata akisema aliondolewa kazini kwa sababu ni mwenye ualbino.

Ingawa alikataa kuitaja kampuni iliyofanya kitendo hicho dhidi yake, amesema kitendo hicho kilimpa simanzi isiyokuwa kifani.

“Niliambiwa kwa vile wewe huoni vizuri hii kazi hautaiweza. Lilipokuja suala la kupunguzwa kazi nilikuwa wa kwanza kuondoshwa,” amesema.

Naye Kondo Seif ameshauri watu wenye ualbino kuvaa mavazi yanayofunika miili yao ili kukwepa ugonjwa wa kansa.

“Kinachotakiwa ni wewe mwenyewe kujilinda usichomwe jua. Vaa kofia, suruali na shati zinazofunika mwili. Vaa viatu pia. Usiache mwili wako wazi, ufunike kwa mavazi hautashambuliwa na kansa,” amesema Seif, Ofisa Uraghibishaji kutoka UTSS.

Daktari wa masuala ya saikolojia kutoka Huwaii, Marekani, Dk. George Rhoades, amewahi kuhimiza umuhimu wa kushirikishwa shughuli za kijamii watu wenye ualbino.

Kwa mujibu wa Dk. Rhoades, ipo sababu ya uundwaji wa Mahakama ya Kimataifa itakayoshughulika na haki za watoto wenye ulemavu duniani.

“Nadhani umesema jambo jema sana, kuwapo kwa mahakama hii inayoangazia matatizo ya watoto wenye ualbino itasaidia. Lakini, viongozi wetu wafundishwe kuhusu kusimamia sheria,” amesema.

Dk. Rhoades anayetoa huduma katika kliniki ya masuala ya saikolojia nchini Marekani amesema: “Tuwape faraja watu hawa.”

630 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!