Juni Mosi hadi 4, mwaka huu Serikali iliadhimisha Wiki ya Mazingira Duniani kijijini Butiama ikiwakilishwa na kuongozwa na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye ofisi yake ndiyo ina jukumu la kusimamia masuala ya mazingira nchini.

Ni wiki iliyosheheni shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na maonyesho maalumu yaliyojumuisha taasisi, idara za serikali, wanaharakati wa uhifadhi wa mazingira, na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na masuala ya mazingira.

Moja kati ya matukio makubwa ya wiki hiyo ilikuwa ni siku mbili za majadiliano ya kitaifa juu ya changamoto zinazokabili taifa katika kulinda mazingira. Changamoto ziko nyingi.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Mazingira, January Makamba alielezea madhumuni ya majadiliano yale kama fursa kwa Watanzania ya kutafuta majawabu juu ya mbinu za kuhifadhi mazingira na kuangalia jinsi ya kuweka hifadhi ya mazingira ndani ya mipango na mikakati ya maendeleo ya sekta za uchumi na huduma za jamii kama vile uvuvi, kilimo, mifugo, utalii, nishati, na maji.

Aidha, alisema pia itakuwa fursa ya kuangalia mfano wa maisha ya Mwalimu Nyerere kama chachu ya kuhimiza na kuhamasisha hifadhi ya mazingira nchini.

Zilijadiliwa mada mbalimbali kwa muundo wa majopo yaliyoshirikisha wasomi, wazoefu wa masuala ya mazingira, na wananchi wakichangia matokeo ya utafiti, uzoefu, na hali ya mwananchi wa kawaida kupambana na athari na changamoto zinazoibuka kutokana na uharibifu wa mazingira.

Kwa ujumla hali ya mazingira nchini inatisha. Tukijikita kwenye uwepo wa misitu pekee tunaambiwa kuwa kiasi cha ekari 372,000 za misitu zinateketea nchini kila mwaka kukidhi mahitaji mbalimbali ya Watanzania. Tumeambiwa pia kuwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam pekee wanatumia magunia 48,000 ya mkaa kwa siku. Takwimu za aina hii ni nyingi zilizowasilishwa na zinaashiria kuwa, kama taifa, bado hatujafanikiwa kutekeleza mikakati ya uhakika ya kulinda mazingira.

Katika majadiliano mada ya kwanza iliuliza: Tanzania bila mkaa na kuni inawezekana? Ni mada iliyoibua taarifa ya utafiti kuwa asilimia 90 ya matumizi ya nishati ya Watanzania inatokana na matumizi ya kuni na mkaa, sehemu kubwa ya kuni na mkaa huu ikitumika kwa kupikia. Katika takwimu hizi, matumizi ya umeme yanawakilisha asilimia 2 ya matumizi ya nishati ya Watanzania.

Hitimisho la mjadala huu lilifikiwa mapema tu kabla ya kumalizika mjadala wa mada hii ya kwanza. Ukweli ni kuwa huwezi tu ukaamka ghafla na ukasema Watanzania waache kutumia kuni na mkaa. Itaathiri watu wengi bila kuwapo nishati mbadala ya kutumia.

Ni uwepo wa nishati mbadala ndiyo utawafanya Watanzania angalau wapunguze matumizi ya kuni na mkaa. Hata nchi ambazo zinatajwa kuwa zimeendelea bado zinatumia mkaa. Tofauti kati yao na sisi ni kuwa matumizi ya mkaa ni asilimia ndogo sana ya jumla ya matumizi ya nishati ambayo huwakilishwa pia na nishati nyingine, kama jua, upepo, na nyuklia.

Lakini siyo nishati mbadala pekee ambayo itasaidia kupunguza kuathirika kwa mazingira, ikiwa ni pamoja na kuteketea kwa misitu inayozalisha mkaa na kuni.

Lipo suala muhimu la uelewa wa Watanzania wenyewe juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira kama dira muhimu ya kutuhakikishia maendeleo yetu na ya vizazi vijavyo.

Miaka machache iliyopita niliendesha baiskeli kutoka Jiji la Mwanza hadi Dodoma na nilibaini kuwa barabara yote hiyo imetapakaa chupa za plastiki na taka nyingine zinazotupwa na watu kutoka kwenye magari, na hasa mabasi ya abiria yanayotumia barabara hiyo.

Huo ni uchafuzi wa mazingira ambao huwezi kuuona kama unasafiri kwa gari kwenye barabara hiyo, lakini ni matokeo ya kukosekana kwa elimu juu ya njia bora za kutupa takataka, na ukosefu wa elimu ya madhara ya kutupa taka hovyo. Itakuwa vigumu kuhimiza wasimamiaji sera na sheria kutumia usafiri wa baiskeli kwenye barabara kuu kama njia mojawapo ya kubaini ukubwa wa tatizo la utunzaji wa mazingira, lakini ni muhimu kwao kutafakari hatua wanazoweza kuchukua kubaini athari ambazo hazionekani kwa urahisi.

Baada ya mshiriki mmoja katika mjadala wa Butiama kuzungumzia umuhimu wa kutoa elimu kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya chini kabisa mpaka kwenye vyuo vya elimu ya juu, tulikumbushwa na mtoa mada na mshiriki kwenye majadiliano, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, ambayo yeye alishiriki kuitunga, haikusahau umuhimu wa suala la elimu. Sheria inazitaka mamlaka mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, serikali za mitaa, idara mbalimbali, pamoja na taasisi za elimu kuzingatia kutoa elimu ya mazingira kama mkakati mmojawapo wa usimamizi wa mazingira.

Ufafanuzi wa Profesa Kabudi uliweka uwazi ukweli kuwa tunayo sheria nzuri ya usimamizi wa mazingira ambayo inawezekana haitekelezwi kwa ukamilifu wake.

Changamoto nyingine ambayo iliibuka kwenye majadiliano ilikuwa ni jinsi gani mila na desturi zinaweza kulinda mazingira yetu. Tulisikia kutoka kwa mshiriki wa majadiliano, Chifu Japhet Wanzagi, akielezea jinsi gani mila na desturi za kabila la Wazanaki zilitenga maeneo maalumu ya misitu ya mitambiko ambayo miti yake haikuruhusiwa kukatwa. Ni msitu ambayo ililindwa kwa sheria kali za kimila dhidi ya aliyezikiuka.

Kudhoofika kwa mila hizo sasa kumepunguza nguvu ya wazee wanaolinda mila hizo kuchukua hatua dhidi ya wanaozikiuka, pamoja na kuwa sheria iliyopo inatambua uhalali wa mila katika kulinda na kutunza mazingira. Tunalo sasa rika ambalo halikukulia ndani ya ukali wa mila na desturi na hawaoni umuhimu wa kuheshimu hizo mila na desturi.

Ipo changamoto nyingine ambayo iliguswa kidogo kwenye majadiliano ya Butiama. Hii ni jinsi gani tamaa ya utajiri inavyoathiri ulinzi wa mazingira. Miaka michache iliyopita nilimuuliza mtoto wa darasa la pili angependa kufanya kazi gani akimaliza masomo. Alisema baada ya kumaliza masomo kwenye Shule ya Msingi ya kijijini Butiama angeenda kusoma Kenya, halafu angefanya kazi ya kuchoma mkaa.

Ilinichukua siku kadhaa kuelewa mantiki ya mtoto yule kusoma mpaka nje ya mipaka ya nchi yetu halafu kurudi Butiama kuchoma mkaa, lakini naamini nilipata jibu. Inawezekana kuwa akilinganisha majirani zake ametambua mapema tu kuwa mchoma mkaa ndiyo tajiri kuliko wote miongoni mwa majirani; kuliko mwalimu anayemfundisha umuhimu wa kupanda na kuhifadhi miti, kuliko daktari anayemtibu kutokana na magonjwa mbalimbali pamoja na yale yanayoletwa na uchafuzi wa mazingira, kuliko polisi anayekamata wanaokiuka sheria ya mazingira, kuliko hakimu wa mahakama ya mwanzo anayehukumu mtuhumiwa wa uchafuzi wa mazingira.

Hizi ndiyo baadhi ya changamoto zilizoibuka kwenye mjadala wa Butiama wakati wa maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani.

1822 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!