*Ahoji sababu ya kutouzwa, akerwa na bei ghali ya sukari

*Akataa kuruhusu iuzwe nje, Mkurugenzi wa Bodi amkwaza


Wakati Watanzania wakiumizwa na bei ghali ya sukari, imebainika kuwa karibu tani 180,000 za bidhaa hiyo ‘zinaozea’ maghalani katika Jiji la Dar es Salaam na sasa wafanyabiashara wanasaka kibali cha kuiuza nje ya nchi.

Kiasi hicho cha sukari ni tofauti na zaidi ya tani 90,000 zilizozalishwa nchini zinazoendelea kuhifadhiwa kwenye ghala la Kilombero Sugar Co. Ltd, Dar es Salaam.


Kitendo hicho kimemkera Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, na kumfanya ahoji sababu za kiasi hicho cha sukari kuendelea kuhifadhiwa maghalani badala ya kusambazwa iuzwe kwa bei nafuu.


Waziri huyo alieleza kushangazwa na ‘picha’ ya tani 180,000 za sukari iliyoagizwa kutoka India kushindwa kutoa unafuu wa bei kwa wananchi. Waziri alishuhudia sukari nyingi ikiwa imehifadhiwa katika maghala tofauti ya wafanyabiashara wakubwa jijini hapa, wakati alipofanya ziara ya kushitukiza, wiki iliyopita.


Ziara hiyo ililenga kumwezesha kujua sababu za kutoshuka kwa bei ya sukari nchini, licha ya Serikali kutoa vibali vya kuingiza zaidi ya tani 180,000 tangu Machi mwaka huu, huku baadhi ya tani hizo zikisamehewa ushuru kupitia utaratibu maalumu wa Serikali.


Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Henry Semwaza, alikuwa kikwazo kwa Waziri Chiza katika ziara hiyo kwani muda wote alijikita katika kutetea kuwapo kwa bei ghali ya sukari na kampuni ‘zinazobania’ bidhaa hiyo maghalani.

 

Semwaza alisema anaridhika na bei ya sasa inayofikia Sh 2,500 kwa kilo ya sukari katika baadhi ya mikoa nchini, akidai kuwa ikishushwa itawaumiza wafanyabiashara wanaoagiza na kusambaza bidhaa hiyo. Aliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia wafanyabiashara hao vibali vya kuuza sehemu ya sukari hiyo nje ya nchi, kuepusha hasara wanayoweza kuipata kwa kuiuza kwa bei ndogo nchini.


Lakini Waziri huyo alisisitiza mara kadhaa kwamba haoni sababu ya kuruhusu wafanyabiashara wanaoomba vibali vya kusafirisha sukari kwenda kuiuza nje ya nchi katika kipindi hiki ambacho bei yake ni kubwa kupita kawaida nchini. “Sijatoa kibali cha kuuza sukari nje ya nchi kwa sababu bei yake haijashuka nchini, bei ilitakiwa isizidi Sh 1,700 kwa kilo moja ya sukari,” alisema Waziri Chiza.


Kwa sasa bei ya sukari inayoagizwa India na inayozalishwa nchini ni kati ya Sh 2,000 na 2,200 jijini Dar es Salaam na mikoani inauzwa kwa kati ya Sh 2,200 na 2,500 kwa kilo moja, kiasi ambacho ni kero kubwa kwa wananchi wa kawaida. Inaelezwa kwamba Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania imeshapokea maombi ya kampuni kadhaa zinazoomba vibali vya kuuza sukari nje ya nchi, huku Semwaza akiwa kinara wa ‘kuibembeleza’ Serikali iziruhusu.


Kabla ya kutembelea maghala kadhaa ya sukari, Waziri Chiza alizuru Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kujua kama kuna shehena ya sukari iliyokwama kwenye makontena katika Bandari ya Dar es Salaam.


“Nimefika hapa (bandarini) kujiridhisha kama hizo tani 180,000 zilizoagizwa (kutoka India) bado ziko bandarini au zimeshasambazwa… unajua “danger” (hatari) ya kukaa na vitu hivi bandarini ni pamoja na kupanda kwa bei,” alisema, na kuongeza: “Tunataka tunaposamehe ushuru, bei ishuke ili mlaji apate nafuu, lakini pamoja na jitihada hizo za Serikali bado sukari haipungui bei!”


Meneja wa Bishara na Masoko wa TPA, Henry Arika, alimweleza Waziri Chiza kwamba hakuna shehena ya sukari bandarini na kufafanua kuwa kazi ya Mamlaka hiyo ni kupakua mizigo kutoka melini na kuipeleka bandari kavu. Alimdokeza pia Waziri kwamba sehemu kubwa ya sukari iliyoagizwa kutoka India bado inatunzwa katika bandari kavu zinazoendeshwa na kampuni mbalimbali za watu binafsi, Dar es Salaam.


Waziri Chiza alibisha hodi katika kampuni ya Al-Hushoom Investment (T) Ltd ambako Meneja Uendeshaji wa kampuni hiyo, Naushad Sharma, alikiri kuwapo kwa makontena 20 yaliyohifadhi tani 20,480 za sukari iliyoagizwa kutoka India.


“Hizi tani 20,480 za sukari ziko hapa kwa miezi miwili sasa zikisubiri mmiliki wake atulipe dola 52,000 za Marekani (sawa na Sh milioni 81.64) tunazomdai kama gharama ya kumtunzia hapa baada ya kutolewa bandarini,” alisema Sharma.


Aliposikia hivyo, Waziri alidakia kwa kusema: “Ni wazi kuwa huyo mfanyabiashara akiikomboa sukari hiyo kutoka hapa, mwisho wa siku atakayeumia ni mlaji wa kawaida.”

Kwa upande wake, Kampuni ya DRTC Ltd ilikiri kutunza zaidi ya tani 2,500 iliyotoka India, huku Meneja Mkuu Mary Musira akimwonesha Waziri baadhi ya mifuko iliyohifadhi bidhaa hiyo ikiwa imeanza kuharibika.


Meneja wa DRTC alitaja sababu kuu ya kusita kusambaza sukari hiyo Dar es Salaam na mikoani kuwa ni hofu ya kuiuza kwa bei ndogo na hivyo kupata hasara. “Bei tuliyotarajia kuuza wakati tunaiagiza (Machi, mwaka huu) si ile inayouzwa kwa sasa… kuna sukari nyingi kuliko mahitaji ya walaji nchini,” alisema Musira.


Kwingineko katika ghala la Kilombero Sugar Co. Ltd, kunakohifadhiwa zaidi ya tani 90,000 za sukari, uongozi wa kampuni hiyo unasaka kibali cha kuuza sehemu ya sukari hiyo nje ya nchi kwa madai ya kokosa soko nchini. Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bashir Harron, alimwomba Waziri Chiza kibali cha kuuza angalau tani 30,000 nje ya nchi, ombi ambalo hata hivyo halikuridhiwa na Waziri huyo.

 

Kwa upande mwingine, Waziri Chiza alionesha dalili za kukubali madai ya baadhi ya watu kwamba baadhi ya wafanyabiashara hao wana mpango wa kuiuza sukari hiyo nje ya nchi kupata faida kubwa, ndiyo maana wamekuwa wazito wa kuisambaza nchini. “Kuna uwezekano kwamba sukari hii (inayoendelea kuhifadhiwa maghalani) inasubiri kusafirishwa kwenda kuuzwa nje ya nchi kama vile Uganda, Burundi, Rwanda na Kenya ambako inadaiwa bei ni kubwa,” alisema Waziri Chiza.


Waziri huyo alisema ukiritimba wa baadhi ya watendaji wa Serikali katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Fedha, na Bodi ya Sukari Tanzania katika kushughulikia mchakato wa kuingiza na kusambaza sukari, unachangia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo nchini.


Kutokana na hali hiyo, aliahidi kuitisha mkutano na mamlaka hizo, waagizaji, wasambazaji na wauzaji wa sukari kutafuta ufumbuzi wa mrundikano wa bidhaa hiyo maghalani ili  kuwapatia unafuu wananchi. Waziri Chiza ameonesha dhamira ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo la bei ghali ya sukari kuwapunguzia mzigo wananchi, lakini juhudi zake hizo zinahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa mamlaka nyingine za Serikali, ikiwamo Bodi ya Sukari Tanzania na wafanyabiashara ya bidhaa hiyo.


 

1772 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!