Katika toleo la Gazeti la JAMHURI la Oktoba 29-Novemba 4 mwaka huu, Jenster Elizabert wa Mwanza amenipongeza kwa kupigania elimu bora Tanzania kwa njia za makala zinazozungumzia masuala mbalimbali ya elimu.

Nashukuru sana kwa kunipongeza na kwa kunitia moyo. Natambua kuwa katika kupigania elimu bora Tanzania siko peke yangu.

Yupo Jenster Elizabert, wapo walimu wasio na idadi na Watanzania wengine wasio na idadi wanaopigania elimu bora Tanzania. Lakini hawana muda wa kuandika.

Kwa bahati mbaya wale walioko Wizara ya Elimu hawajui hilo. Kwa hiyo, wanajiaminisha kwamba ni Halimoja peke yake anayewapigia kelele. Kumbe Watanzania wamechoka na elimu mbovu ambayo watoto wao wanaendelea kupewa huku watoto wa wakubwa wakiendelea kupata elimu bora.

Siku moja nilikuwa nazungumza na marafiki zangu — mmoja wao akanichokoza. Alisema, “Halimoja, nakupongeza sana kwa makala za kupigania elimu bora unazoandika katika Gazeti la JAMHURI. Lakini hujajua bado kwamba unapoteza wakati wako? Nani anajali unachoandika? Wizara ya Elimu ni genge la watu wasiojali matatizo ya elimu yanayoikumba Tanzania. Wanajali maslahi yao.

 

Hakuna mzalendo kule. Subiri tupate Serikali sikivu ndipo uandike. Serikali sikivu itayafanyia kazi yote unayoyaandika. Kwa sasa usipoteze wakati wako. Acha kuandika.” Kabla sijapata nafasi ya kutoa jibu mara rafiki yangu mwingine akadakia.

Hakukubaliana na maneno aliyosema rafiki yangu wa kwanza. Rafiki yangu wa pili alijibu; “Maneno ni ya kumkatisha tamaa Halimoja aache kupigania elimu bora kwa watoto wetu. Hebu tuambie, hiyo Serikali sikivu itapatikana lini? Mimi, kwa mambo mawili, namshauri aendelee kuandika.

Kwanza, anachoandika kinawasaidia wananchi kujua hali halisi ya elimu katika Tanzania yetu ya leo. Pili, Watanzania wa miaka ijayo wakisoma haya anayoyaandika leo watajua kuwa wapo Watanzania waliojitahidi kupigania elimu bora, ila Serikali haikuwa sikivu. Kwa hiyo, Halimoja nakushauri uendelee kuandika.”

Nami naendelea kuandika.

Tunapozungumzia matatizo ya elimu katika Tanzania yetu ya leo, hatuwezi kuficha ukweli kwamba tatizo moja kubwa la elimu Tanzania ni Wizara ya Elimu kukosa viongozi wazalendo. Na badala ya kuona na kukubali ukweli wa mambo, wamekaa kutoa kauli zisizosaidia maendeleo ya elimu Tanzania.

Nakumbuka wabunge walipomtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, ajiuzulu uwaziri kwa kushindwa kusimamia elimu Tanzania, alisema kwamba ana baraka zote za Rais zinazomhalalisha kuendelea kuwa Waziri wa Elimu.

Hapa mtu hukosi kujiuliza. Hizo baraka za rais anazojivunia Waziri ni baraka za kuendelea kuboresha au kuboronga elimu? Wananchi haikosi wanalo jibu.

Nimetangulia kudokeza kuwa tatizo moja kubwa la elimu Tanzania ni Wizara ya Elimu kukosa viongozi wazalendo. Viongozi wazalendo kwa vyovyote wangeyafanyia kazi maoni ya wananchi yanayohusu elimu, wasingesita kurekebisha dosari zilizopo katika mfumo wa elimu Tanzania.

Lakini kwa sababu tuna viongozi wa wizara wanaolinda maslahi yao tu basi, kukosa kwao uzalendo kunasababisha mambo ya wazi kabisa yaachwe bila kufanyiwa marekebisho.

 

Nitatoa mifano. Kuna suala la wanafunzi wa shule za sekondari kuendelea kufundishwa Somo la Uraia (Civics) kwa lugha ya Kiingereza. Somo la Uraia limekusudiwa kuwajengea vijana wetu moyo wa uzalendo.

Ni somo linalozungumzia maisha ya kila siku ya Taifa lao, kwa nini somo hili lifundishwe kwa lugha ya kigeni? Kwa nini masuala ya Taifa yasifundishwe kwa kutumia lugha ya Taifa? Tutafanikiwa vipi kuwajengea vijana wetu moyo wa uzalendo kama hawaelewi vizuri lugha inayotumika kuwafundisha uzalendo?

Kwa kweli ni aibu kwa Taifa huru kama Tanzania kufundisha masuala ya Taifa kwa lugha ya kigeni. Hayo ni matokeo ya Wizara ya Elimu kukosa viongozi wazalendo.

Tuna hili Somo la Stadi za Kazi lililokusudiwa kuwasaidia watoto wetu kujiandaa kwa kujiajiri wenyewe, hasa wale wanaorudi nyumbani baada ya kumaliza elimu ya msingi.

Miaka nenda miaka rudi viongozi wa wizara wameendelea kupeleka mashuleni vitabu vya stadi za kazi, ambavyo vinawapatia asilimia kumi ya fedha kutoka kwa wachapishaji wa vitabu.

Lakini wakati wote somo hili halina vifaa vya kufundishia na halina walimu waliopewa mafunzo ya kuwasaidia kufundisha somo hilo.

Kwa hivyo, somo hilo si kama tu linawapotezea wakati walimu na wanafunzi wao, bali pia linasababisha vijana wetu wanaomaliza darasa la saba kushinda vijiweni. Hawana cha kufanya.

Somo la Stadi za Kazi halikuwasaidia kujiajiri wenyewe. Wizara ya Elimu haikusimamia Somo la Stadi za Kazi. Imesimamia vitabu vya Stadi za Kazi vinavyonufaisha wale walioko wizarani. Ni matokeo mengine ya Wizara ya Elimu kukosa viongozi wazalendo. Kwa kuwa watoto wao hawana matatizo ya ajira, basi kwao si kitu watoto wa maskini wakikosa ajira.

Halafu kuna suala la fedha ya rada iliyokusudiwa kuzipatia shule vitabu na madawati. Vitabu vilivyopangwa kununuliwa kutokana na fedha ya rada ni vitabu ambavyo tayari walimu wamekwisha kuvitumia katika kufundishia mashuleni. Lakini ni vitabu ambavyo kwa muda mrefu walimu wamelalamika kuwa ni vibovu.

Kwa hiyo, ilitazamiwa kuwa kabla vitabu hivyo havijachapishwa upya na kupelekwa mashuleni, zingefanyika angalau semina za siku moja moja za walimu wa masomo hayo waliopo Dar es Salaam, ambao wangetoa maoni kwa niaba ya wenzao walioko mikoani ni  vitabu vipi visichapishwe upya na vitabu vipi vichapishwe upya na marekebisho gani.

Lakini walichoona vyema viongozi wa Wizara ya Elimu ni kuelewana na wachapishaji wa vitabu. Wakati wa kuvichapisha na kuvisambaza mashuleni vitabu hivyo vibovu, kazi hiyo walitakiwa kuikamilisha Septemba mwaka huu. Na wameikamilisha. Wameikamilisha kazi ya kusambaza vitabu vibovu mashuleni vitakavyoendelea kuwapa elimu mbovu  watoto wa maskini Tanzania.

wachapishaji walitakiwa kufanya kazi hiyo kwa miezi sita, basi kuanzia Januari hadi Mei vitabu hivyo vinaweza kupitiwa na walimu na kufanyiwa marekebisho. Juni mpaka Novemba vingeweza kuchapwa na kusambazwa mashuleni kabla ya mwaka mpya wa shule.

Lakini viongozi wa Wizara ya Elimu kwa kukosa uzalendo waliamua kupata chao haraka haraka. Shule zikasambaziwa vitabu vibovu.

Hii ndiyo hali halisi ya uongozi wa elimu Tanzania.

1147 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!