WIZARA ZAWEKA MKAKATI WA KUIMARISHA MUUNGANO

Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania Bara na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ya Zanzibar zimeweka mkakati wa pamoja wa kuimarisha ushirikiano wa usimamizi wa maliasili, malikale na kuendeleza utalii kwa maslahi ya pande zote za Muungano.
Hayo yameelezwa  na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi baada ya mkutano wa pamoja wa wizara hizo uliofanyika hivi karibuni katika Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa siku moja uliongozwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Joseph Meza.
Akifungua Mkutano huo wa siku moja,  Maj. Gen. Milanzi alisema pamoja na Wizara hizo kutokuwa za muungano imekuepo haja kubwa ya kukutana kwa ajili kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha sekta ya maliasili na utalii na kukabiliana na changamoto zinazogusa sekta hiyo katika Muungano.
“Tumejadiliana kuona ni namna gani tunaweza kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ya biashara ya mazao ya misitu, biashara ya Wanyamapori inayohusiana na mikataba ya CITES na mikataba mingine ya ndani na ya Kimataifa.
“Tumekubaliana pia kuhuisha sheria zinazokinzana katika usimamizi wa sekta tunazozisimamia ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza katika utekekezaji na hivyo kuathiri Muungano wetu,” alisema Maj. Gen. Milanzi.
Alisema katika mkutano huo wa siku moja wataalamu kutoka pande zote za Muungano waliagizwa kuwasilisha mapendekezo ya namna bora ya kuendesha biashara ya mazao ya misitu na kupendekeza utaratibu wa kufanya biashara kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo.
Alisema kupitia mkutano huo Wizara hizo zimeunda kamati maalum ya kuratibu utekelezaji wa maazimio ya pamoja ya kuimarisha usimamizi bora wa sekta hizo na utatuzi wa changamoto zilizopo kwa kuandaa mapendekezo ya kimkakati ya muda mfupi na mrefu.
“Kamati hiyo itaongozwa na Afisa Mipango Mkuu Msaidizi kutoka Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka (DFNR), Saleh Kombo Khiari na Mchumi kutoka Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Maliasili na Utalii, Mugure Wambura,” alisema Milanzi.
Mbali na hayo alisema kutakuwepo na vikao mbalimbali vya kuimarisha Muungano kupitia Wizara hizo katika ngazi ya wataalamu, Makatibu Wakuu na Mawaziri ambapo kikao kingine kinatarajiwa kufanyika kabla ya tarehe 30 Machi, 2018.