Kuna wakati huwa nakumbuka jitihada za Serikali kutukusanya pamoja katika vijiji vya Ujamaa miaka ile ya operesheni sogeza vijiji, ili wananchi tupate huduma za jamii wote kwa pamoja zilizokuwa zikitolewa bure na Serikali, huduma za maji, elimu, afya na ulinzi.

Operesheni ile ilikuwa ngumu kwa kuwa wengi wetu tulikuwa bado hatujaelimika juu ya umuhimu wa huduma hizo na kwamba upatikanaji wake ulihitaji tusogezwe mahali pamoja – iwe kwa hiyari au kwa nguvu, lakini lengo lilikuwa ni kuhakikisha tunapata huduma hizo bila kujali athari za mtu mmoja mmoja.

Maendeleo ya nchi na wananchi yametufikisha mahali ambapo kila mmoja anaweza kutoa maoni yake na ushauri kwa serikali yake muda wowote bila kuvunja sheria, maendeleo haya yametufanya tuwe wadadisi wa mambo ya msingi kwa mustakabali wa Taifa letu.

Tulipokubali mfumo wa vyama vingi tulikubali upinzani wa hoja kwa mambo ya msingi, hatukukubali ushindani wa kubishana kwa kuwa kila mtu ana mtazamo wake katika jambo fulani, na ndiyo maana katika misingi ya demokrasia dhana ya wengi wape inapewa kipaumbele.

Wiki kadhaa zilizopita, lilikuwapo suala la maandamano ya kutaka kupinga unaoitwa udikteta wa viongozi walioko madarakani. Viongozi walioko madarakani walitoa mawazo yao kwamba Taifa limefika hapa lilipo kwa umaskini kutokana na kutofanya kazi, uvivu umetamalaki miongoni mwetu kiasi kwamba nguvu kazi nyingi inaishia katika magenge ya siasa za majukwaani.

Serikali ya awamu ya tano imejipambanua kwa kaulimbiu ya ‘hapa kazi tu’, kauli ambayo inakinzana na kubweteka kwa kutofanya kazi na kusababisha kuendelea na umaskini ambao ni janga kubwa kwa wananchi wa Tanzania waliokosa huduma muhimu za msingi kutoka katika Serikali yao. Serikali ya awamu ya tano ilinadi sera za mabadiliko ya kiuchumi na siyo mabadiliko ya kisiasa kama ambavyo baadhi yetu tunaaminishwa, Serikali ya awamu ya tano imeweka pembeni suala la siasa na kuamua kufanya kazi zaidi.

Wanasiasa wengine hawakubaliani na hilo kwa kuwa wengi wao wamegeuza uwanja wa siasa kuwa ajira ya kudumu, wamewageuza wananchi kuwa mtaji wa kisiasa na kuwayumbisha wanavyotaka kwa kutumia kigezo cha demokrasia ya vyama kufanya siasa muda wote.

Mimi naamini siasa safi ni ile ya kujenga hoja ya kimaendeleo, siyo kupinga maendeleo. Taifa letu kwa kipindi kirefu limekuwa la vijana wengi kutofanya kazi, limekuwa Taifa la madalali, limekuwa Taifa la maneno zaidi badala ya kufanya kazi, Serikali ya awamu ya tano ililiona hilo na kuamua kulitekeleza kwa vitendo.

Suala hili halina tofauti na suala ambalo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alilianzisha, suala la nguvu kazi, katika kipindi kile tulikubaliana siasa itafanywa jioni baada ya kazi, tulikubaliana kila mtu ni lazima afanye kazi, tulikubaliana hakuna kiongozi ambaye hatakuwa mfano mbaya kwa wananchi.

Yote haya ni masuala ya kukumbushana ili kuhakikisha Taifa linapata maendeleo, tutakumbushana suala la elimu,  suala la usafi, ulinzi, afya na mengine.

Miaka mingi imepita tangu tupate uhuru, lakini hiyo haimaanishi kwamba mipango ya Serikali sasa inaeleweka bayana kwa wananchi, ndiyo maana hata suala la kodi tunazidi kukumbushwa kila siku kwamba ni jukumu letu kuhakikisha tunalipa bila kushurutishwa.

Mataifa mengine duniani yanayojua umuhimu wa kodi, wananchi wake walipata elimu hiyo mapema na kuona suala hilo ni suala la msingi lisilohitaji mjadala wakati wa kulipa, mtu huona aibu kutolipa kodi, na mtu hujikuta akipeleka kodi bila kuulizwa.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo

1002 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!