Nimelala nikaota njozi mbaya sana kwa kuonyeshwa mtu ambaye namfahamu lakini siye, kuna mtu kasema amka umuangalie Julius yuko mbele yako, nami kwa haraka nikaamka ili nimsimulie tumefikia wapi katika kuenzi yale ambayo alituusia kama taifa.

La kwanza kabisa ni kumwambia ile hifadhi ambayo ilikuwa bado haijapandishwa hadhi ndiyo hii tumeipandisha hadhi na leo tunaizindua.

Nilipoamka na kukutana na mwalimu ambaye simfahamu na ninalazimishwa kuwa ndiye, almanusra nirudishe kadi yangu ya chama ambacho naamini nitakufa nacho, kwa sababu siku zangu si nyingi sana za mtu kunishawishi niondoke kwenye chama kilichonilea mpaka leo.

Nilitaka kuchukua uamuzi huo kwa sababu nilikuwa kama naaminishwa kwamba tumemsahau Mwalimu mapema mno na kidogo nilitaka kufikiri kwamba huenda kwa kifo chake tumemsahau yeye na mambo yake.

Najua nimechelewa kutoa maoni yangu, sababu zipo nyingi. Kwanza huku Kipatimo ni mbali kuyasikia yanayoendelea kila siku huko duniani, kama tujuavyo Tanzania ya sasa ina mambo mengi sana na muda ni mfupi.

Pili, hata niliposikia nilijipa muda kujiridhisha kama yanayozungumzwa ni kweli ama la, nikajiridhisha kwamba ni kweli. Tatu, nilitaka kusikia wenzangu waliomuona huyo Julius wa Burigi wanasemaje? Na mwisho, kauli ya wahusika wanasemaje?

Nilijiridhisha na picha iliyoonekana katika mitandao japo sina hakika kama ndiyo hiyo iliyowekwa katika mbuga hiyo, kwamba huyo wanayesema ni Mwalimu nadhani walitaka kutumia kwa muda tu wakati wakijiandaa kumtafuta aliye halisi.

Lakini jambo la maana zaidi ni kauli ya kiongozi aliyehusika kuomba radhi na kwamba sanamu ya  Mwalimu mwenyewe itawekwa. Nikafarijika sana, naamini mpaka leo kila kitu kitakuwa sawa na hata nikienda kule kutalii nitapata nafasi ya kupiga picha na sanamu ya Mwalimu mwenyewe.

Naanza kwanza waraka wangu kwa kupongeza yale mawazo tu ya kusema lazima awepo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika mbuga hii muhimu kwa ajili ya utalii na kuongeza mapato kwa taifa.

Idadi ya mbuga na vivutio vingine ni jambo la kujivunia sana kama taifa, nimesikia pia kuna eneo jingine huko Kusini ambalo ni eneo lililosahauliwa kama eneo tengefu lenye uoto wa asili na sasa linaanza kufanyiwa kazi ili nalo litengwe kwa ajili ya utalii, haya ndiyo yalikuwa mawazo ya Mwalimu katika mbuga na madini na kufanya hivi ni ishara tosha ya kuenzi kile ambacho alikiamini kwa masilahi mapana ya Watanzania.

Sasa nizungumzie sanamu ile ya Burigi na umuhimu wa kuwa na sura ya Mwalimu ambaye sisi wachache tulibahatika kukutana na kukaa naye tukanywa chai pamoja na tukajadili mambo muhimu ya taifa hili. Kwa asiyejua, nimwambie tu sura ya Mwalimu ilikuwa ikisema kila kitu hata kama hajatamka, kwa lugha rahisi sana ni kusema Mwalimu alikuwa kama Mwenge wa Uhuru ambao unasema kwa kuwaka moto.

Inawezekana kabisa tukawa na mboni ambazo zimetofautiana katika kufananisha vitu na hili liko wazi kwa kuwa wapo wanaoona rangi nyekundu kuwa ya kijani na kwamba sasa kimepita kipindi kirefu sana ambapo kuna vijana wengi waliozaliwa na hawana picha halisi ya Julius ambaye sisi wachache tunamjua na kumkumbuka.

Hiki ni kizazi cha kufanya kazi mbalimbali na kufanya marejeo mengi ambayo pengine yanamrejea Mwalimu bila kujua na kumfahamu anayemrejea, najua na sina shaka aliyefinyanga sanamu ile alikuwa hajazaliwa wakati wa Mwalimu, pia hakutaka kufanya marejeo yoyote kutoka katika vitabu mbalimbali.

Lakini kazi ya usanii inasema kazi unayoifanya inatakiwa itoe sauti kuliko ile kazi uliyoifanya. Nikiri wazi sanamu halisi ya Mwalimu katika mbuga ya Burigi inaweza kusema zaidi kuliko maelezo ambayo yangetolewa na kazi ambayo imefanywa. Kwanza, ndiye aliyesimamia mbuga zote hata zile ambazo hazikupandishwa hadhi wakati wake kama hiyo ya Burigi. Sina shaka kuhusu uamuzi wa busara uliofanywa wa kuweka sanamu yake hapo.

Lakini lazima nikiri kuwa kwa kosa hili lililofanywa ni dalili kwamba tunaanza kumsahau Mwalimu kwa sura yake na kutia hofu juu ya matendo na maono yake ya wakati ule. Dhana ya kuenzi ni pamoja na kumkumbuka yeye kwa sura zake zote. Sisi wachache tunaweza kumkumbuka akiwa Pugu kisha kukisimamia chama, kuongoza taifa kwa miaka yote kabla ya kung’atuka, mtoa ushauri kwa chama na mwisho, kifo chake. TUTAFAKARI.

Wasalamu,

Mzee Zuzu, 

Kipatimo.

329 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!