Wiki moja iliyopita tulikuwa tunamkumbuka Julius, Julius Kambarage Nyerere, yule aliyepata kuwa Rais wenu wa Awamu ya Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Julius ambaye mimi naweza kumkumbuka vizuri ni yule Waziri Mkuu na baadaye Rais wa Tanganyika kijana kutoka Butiama, mtoto wa Mzee Nyerere Burito na Mama Mugaya wa Nyang’ombe.

Wanangu, huwa napata tabu sana ninapowakumbuka watu wa watu, na hasa kama ametangulia mbele ya haki. Mtu wa watu utamjua kwa mambo mengi. Watu watamlilia sana, watu watamkumbuka bila kumtaja, na watu watamtaja kwa namna yoyote ile. Wapo wachache watakaomtaja kwa ubaya na hao ni wachache, lakini wengi watamtaja kwa mema yake.


Julius ni kama Patrice Lumumba, Kwame Nkrumah, Augustino Neto, Samora Machel ambao wote wametangulia mbele ya haki na wapo akina Nelson Mandela, Kenneth Kaunda ambao wapo hai na katika kundi lao nao wanajiona wapweke sasa, maana wenzao wako kusikosikika kauli zao.


Hawa ndiyo wanaokumbukwa na watu katika Bara la Afrika – iwe kwa ubaya au kwa wema. Mimi Mzee Zuzu nawakumbuka kwa wema na kwamba wema wao utaendelea daima kukumbukwa na kuwa wenye tunu kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele.

 

Wanangu, Julius ndiye aliyetufanya tujue mabaya mengi ambayo leo tunayaona. Mabaya kama utumwa, rushwa, uvivu, wizi wa mali ya umma, undugu kazini, ubaya wa magendo, nidhamu ya viongozi, ubepari, umwinyi, ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo.

 

Wanangu, naapia miungu yote kwamba Julius ndiye aliyepigana kwa moyo wa dhati kabisa suala la rushwa na ile kaulimbiu yake ya “rushwa ni adui wa haki”, leo mnaoona kwa macho yenu na akili zenu jinsi rushwa inavyolimeng’enya Taifa kwa urahisi. Penye rushwa haki haipo na haitapatikana labda damu imwagike.


Leo rushwa si suala la kujadili. Tunalishuhudia. Tume zinaundwa haki haitendeki. Julius ninayemfahamu mimi alidiriki kunyoa nywele upande mmoja viongozi waandamizi sita wala rushwa pale Karimjee mwaka 1964. Alidiriki kumchapa viboko ishirini na nne mzalendo aliyepokea rushwa.


Alidiriki kumfukuza tajiri mkubwa wa Kigiriki si tu Tanzania, bali Afrika Mashariki yote asionekane. Julius hakuipenda rushwa wala masalia ya rushwa kwa moyo wa dhati na hata leo akifufuka akisema hataki rushwa hatuna sababu ya kuthibitisha kwa kumwangalia usoni, jibu ni ‘ndiyo’.


Julius hakupenda ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo. Alipiga vita ukoloni mkongwe kwa kutumia siasa hadi tukapata Uhuru. Akasaidia nchi nyingi zinazotuzunguka na hata ambazo hazikutuzunguki, lakini waliokuwa wanataka uhuru alichukua uamuzi mgumu katika kulitekeleza hili.


Aliwasaidia ANC, ZANU-PF, FRELIMO, MPLA, kila chama kikiwa na lengo la kulikomboa taifa lao na hatimaye wakafanikiwa. Wote hao wanamkumbuka Julius katika ukoloni mkongwe. Hakupenda ukoloni mamboleo ambao leo unatutesa, umekuja kwa njia ya uwekezaji na ubinafsishaji.

 

Watanganyika halisi leo ni watumwa ndani ya ardhi yao kwa kigezo cha kuinua hali ya uchumi; uchumi Julius alioukataa kwa nguvu zote kwa kutumia siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Tuliamini katika kujitegemea na tuliweza kujitegemea kwa zaidi ya miaka 23 aliyokaa Ikulu, tukiwa na amani nzuri ya Taifa na kila Mtanzania alishiriki katika kuota moto mtamu wa pato la Taifa. Huyu ndiye Julius ninayeweza kumsemea bila haya mbele za watu.


Julius huyu aliamini kuwa hawezi kuwa tajiri katikati ya masikini walio wengi. Akafariki akiwa masikini wa kweli kama Rais, aliyeonewa imani ya kujengewa nyumba na jeshi letu, masikini aliyeacha pea nane tu za viatu, na aliyewaacha wanawe wajitegemee bila msaada wake kwa kuwa ni Watanzania kama walivyo Watanzania wengine.


Ni Julius aliyewaachia Taifa likiwa na viwanda na mashirika zaidi ya 400 na vikafa kabla hajafa kwa tamaa ya ulafi na rushwa. Ni Julius aliyetengeneza mazingira mazuri ya ajira kwa Watanzania kabla ya ajira  kwa wageni kukomaa kwa sababu ya rushwa. Ni Julius aliyeweza kuilinda nchi yetu kwa kumfanya kila Mtanzania kuwa mzalendo wa kujali usalama wa Taifa lake, masikini rafiki yangu juhudi zake zimeondoka kama alivyoondoka.

 

Mzee Zuzu nasoma maandiko ya Julius. Naangalia picha za Julius, nasikiliza simulizi za Julius, naona ni mwanga tosha kwa yeyote mwenye kutwaa madaraka, lakini najiuliza hawasomi, hawaangalii, hawasikilizi, hawakumbuki? Au hayo ndiyo mambo ya dotcom?


Siku chache baada ya taarifa ya kifo chake huko Ulaya, watu walimlilia hadi wakazirai. Walimzika kwa  mamilioni. Taifa lilizizima. Akazikwa Mwitongo. Ukawa mwisho wa matarajio ya dhati ya kuwa na mtu anayeweza kusema kweli daima bila haya na kumuogopa mtu kwa cheo chake na fedha zake. Huyu ndiye Julius ambaye Waganda wanataka awe Mwenyeheri. Ni Julius ambaye naweza kutembea kifua mbele kwamba alikuwa kiongozi wangu wa kuigwa.


Julius kama ungali duniani na unasoma magazeti kama wanangu wanavyosoma, naomba ujue kuwa nakukumbuka kwa nia yako ya dhati kwa Watanzania ambao wengine leo ni furaha kwa kuwa wanakuzunguka na kufanya uliyoyakataa yaliyokuwa na maana kwa Taifa hili.


Natamani ufufuke uchukue fomu ya urais mwaka 2015 ili tufike tulikotaka tufike baada ya kuchelewa, na kama huwezi kufufuka, basi tupe maono yako kama kawaida nani anatufaa anayeweza japo kuiga robo ya nia yako ya dhati, najua tutafika mbali.

 

Ewe Mwenyeheri, wahenga walisema hakuna anayeweza kuliliwa na wengi na asipewe pepo njema. Sisi tunakulilia katika jehanamu tunapenda ukae mahala pema peponi.

 

Wakatabahu, Bwana awe nawe mtu wa watu. Tutawaangalia wanao daima na Maria nitamtunza kama mjane wa mkweli. Uliipenda sana Tanzania, lakini Mungu alikupenda wewe zaidi, akakuchukua utangulie ili tujue thamani yako. Chema hakidumu, lakini fikra zako nasema zitadumu daima.

Zidumu fikra za Mwenyekiti wa TANU.

Wasalaamu,

Mzee Zuzu,

Uliyeniacha Kipatimo  nikilima.


1093 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!