Yah: Kama ningekuwa Waziri wa Usalama Barabarani

Wanangu, nawapa kongole ya kutimiza miaka 51 ya Uhuru mlionao hivi leo, nawapongeza kwa kuwa sisi wana-TANU ni kama ndoto ya kuamini kuwa tumeweza kuhimili vishindo vya wakoloni kwa kipindi chote hiki.

Narudia kusema tena kuwa mmeweza kuvumilia na kupigana na ukoloni mamboleo kwa uwezo wenu na hasa katika kipindi hiki cha utandawazi. Nasema hivi kwa kuwa sasa soko la dunia ambalo ndiyo lingeweza kuwaingiza katika utumwa limeshikiliwa na wakoloni tunaowatarajia.

 

Lakini wanangu, leo nawapa pongezi ya kutotawaliwa na mkoloni na wakati huo huo nawapa pole ya kutawaliwa na mwananchi asiyeweza kutekeleza majukumu yake, matokeo yake ni afadhali tungeendelea kutawaliwa na mkoloni tuleyemtimua enzi za TANU. Katika barua zangu zijazo – panapo majaaliwa –  nitajaribu kusema kama rais angenipa nafasi ya kuwa mmoja wa wasaidizi wake, ningefanya nini katika kumsaidia majukumu yake na kulipeleka taifa katika heshima ya kutimiza miaka hiyo ya uhuru.

 

Leo najaribu kufikiria kama ningeteuliwa kuwa waziri wa usalama barabarani, na kwamba ningekuwa na ruhusa ya kuongeza kanuni katika sheria za usalama barabarani ningefanya mambo yafuatayo:

 

Mosi, kwa jeuri kabisa baada ya kuapishwa ningemwambia rais wangu kuwa naomba tutoe ofa ya miaka kama miwili hivi, kuzitangaza mbuga zetu za wanyama nje ya nchi kwa kuwakaribisha watalii bure bila kulipia kitu chochote na pengo hilo la fedha ningeliziba mimi kupitia wizara yangu ya usalama barabarani.

 

Pili, ningemuomba rais azibe masikio ya wananchi ambao kazi yao ni kulalamika kila kukicha, kana kwamba wao sheria na kanuni haziwahusu na kwamba kwao sheria ni mbaya na sheria hiyo hiyo ni nzuri, kwa lugha nyingine ni vigeugeu, sheria ni nzuri inapowasaidia na mbaya inapowabana!

 

Tatu, ningemuomba rais wangu aniache huru nikusanye mapato ya nchi yetu bila kuingiza siasa kwa kuwa mchezo wa siasa ni kuwafurahisha wananchi lakini pia ni kuwaumiza hao hao wananchi wenyewe bila kujua.

 

Baada ya kiapo ningewaita maafande wangu kwa mbwembwe na jeuri kwamba sasa tufanye kazi ya ukweli bila kuigiza wala kuonea mtu, tungegeuza eneo letu la kazi kuwa taaaluma ya kweli na kwamba ni kitu muhimu katika maisha ya binadamu kutegemea sekta yetu ya barabara.

 

Tungeanza na kanuni na adhabu zake, mfano sheria zote za barabarani tungezipigia mstari kwamba hizo zinatakiwa kuboreshwa, kwa maana zimepitwa na wakati na kwa kuwa sheria za barabarani zinahusu uhai wa mwananchi basi zihusu uhai wa anayevunja mara moja kama mwizi wa simu.

 

Ningeweka kanuni kwa mamlaka niliyonayo kulingana na uhalisia wa maisha, mathalani kutokuwa na leseni na ukaonekana unaendesha chombo chochote adhabu yake iwe milioni moja sanjari na kukiuza chombo chenyewe kwa anayeweza kufuata sheria, potelea mbali lawama ambazo ningezipata baada ya miaka mitano ya utawala wa uwaziri wangu lakini najua nitakumbukwa milele kwa kupunguza ajali za kipumbavu.

 

Kusababisha ajali ya kizembe – iwe kwa ulevi au mazoea –  ni kunyang’anywa leseni na kifungo cha miaka hamsini na kazi ngumu, lakini kama ajali hiyo inahusisha ulemavu wa binadamu au kifo basi adhabu yake ni kifo bila kukata rufaa!

 

Kuvunja sheria ya barabarani, mathalani kuegesha gari mahali pasiporuhusiwa ni jela miaka kumi na adhabu ya chombo chenyewe kuchukuliwa na Serikali kama ni pikipiki watapewa makatibu kata zitatosha, kama ni trekta litapelekwa halmashauri au kijijini likalime kwa manufaa ya taifa, kama ni lori litasomba vifusi kutengeneza barabara, kama ni basi litawasafirisha wananfunzi na walemavu nao wajione huru ndani ya nchi yao.

 

Kuzidisha mwendo au kwenda mwendo mdogo na kusababisha foleni adhabu yake ni laki tano na kunyang’anywa leseni na chombo husika kiuzwe na fedha ziende hazina, kosa hilo ni pamoja na la kuchomekea au kumtukana mwenda kwa miguu, dereva mwenzio, na kadhalika.

 

Ningekaa na vigogo wa wizara yangu katika semina elekezi ya siku mbili na tungetoka na mradi kazi ambao ungeliingizia taifa hili mabilioni ya fedha, bila kutegemea watalii kwa miaka zaidi ya miwili na matokeo yake neno ‘ajali’ lingekuwa msamiati baada ya muda mfupi, lingekuwa ni suala la kujipanga katika wizara yangu ili kuleta mapato na heshima ya taaluma yetu ya udereva na wizara ya usalama barabarani.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo