Nimeanza kwa swali hili kutokana na ukweli wa mfumo wetu wa demokrasia kuhoji kila jambo ambalo pengine baadhi yetu tunadhani haliwezekani kutokana na uwezo wetu wa kutafakari mambo. Kuna wakati mwingine kunazuka hoja za msingi, lakini kwa maana ya kupata umaarufu kisiasa katika vyama vyetu.

 Nianze kwa kumpongeza Mhe. Rais kwa kauli ambayo inanikumbusha miaka dahari ya Tanzania yenye neema na mafanikio ya kiuongozi. Tanzania yenye dira na mipango endelevu kwa nia ya kusonga mbele kimaendeleo.

Alipokuwa anasema anahamia Dodoma katika kipindi cha miaka minne na miezi minne nywele zangu zilisimama kwa hofu ya utekelezaji. Nilianza kusikia homa nilipomsikia Waziri Mkuu akisema ndani ya miezi miwili yeye atakuwa amekwishahamia Dodoma kwa hiyo angelipenda kuwaona mawaziri nao wakiwa Dodoma.

Hizi ni kauli ambazo zinapaswa kutolewa na viongozi wenye kuanza kuonyesha mfano wa kile ambacho wangelipenda na wananchi tuwafuate na kuwaunga mikono. Lengo la makao makuu litatimia pale tu ambapo kauli na matendo vitakuwa sawia.

Suala la kuhamia Dodoma tulianza kuzungumza tangu tukiwa vijana wa makamo enzi za siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Tulihasishana kuanza kujenga makao makuu ya nchi yetu, wakati huo Dodoma ilikuwa haifikiki kwa njia zote kama leo.

Tulianzisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ambayo iliwezeshwa kwa kila kitu. Viwanja vikatengwa vya kila wizara na miundo mbinu ilitengenezwa vizuri kiasi kwamba makao makuu ingelikuwa pepo ya Tanzania kwa ubora wake.

Leo yapata miongo kadhaa tangu tulipolisahau jambo hili, kiasi cha kufanya Dodoma kubadili jina na kuwa makao makuu ya kufikirika, wajanja wachache walioweza kuhodhi vizuri madaraka yao walilipoteza suala la Makao Makuu kama vile kuhamia Dodoma ni kosa kubwa la kiutumishi.

Lengo letu wana TANU, lilikuwa kuhakikisha huduma muhimu kwa wananchi zinawafikia kiurahisi, hasa huduma za kiuongozi. Lengo lao hao wachache wenye akili nyingi ilikuwa kuleta ukiritimba katika hili waweze kujipatia riziki kwa matumbo yao binafsi.

Kusogeza huduma kwa jamii ni jambo ambalo lilionwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza, lakini jambo muhimu zaidi ni pale ambapo huduma hizo zinasogezwa kwa lengo kuinua uchumi wa pande zote za nchi na kufikika kiurahisi.

Leo hii Dodoma kwa maana ya miundo mbinu ya kufikika haina ubishi kwamba imekamilika na ni mkoa ambao unaweza kufika siku hiyohiyo kutoka pande zote za nchi yetu. Ni mkoa ambao hauna shughuli nyingi za kibiashara na kuzuia kufanyika kwa mambo mengi ya kimsingi ya Serikali.

Dodoma si kama yalipo makao makuu ya sasa, si mji wa foleni ambazo zinachelewesha shughuli mbalimbali za kitaifa. Ni mji ambao ukibeba dhamana ya makao makuu ya Serikali utaachia Mkoa wa Dar es Salaam kuwa mji wa biashara, ambazo kimsingi ni za muhimu kwa mstakabali wa taifa letu.

Hivi sasa mji umeelemewa. Wachumi wanazungumzia athari zinazopatikana kutokana na kujaza magari na foleni. Wachumi wanazungumzia uchelewaji wa watumishi kazini. Wachumi wanazungumzia fursa ya kupanua wigo wa huduma ulivyogubikwa na wakaazi waliopo.

Kwangu mimi hoja ya mwanzo enzi zetu ndio ninayoiona ya msingi. Kusogeza huduma kwa wananchi na kujipanga upya muundo wa Mji wa Dodoma kukidhi haja ya utoaji wa huduma. Ningeshauri uamuzi huu usiingiliwe na wanasiasa na uwe wa Serikali kwa maana ya kuwasaidia wananchi wote bila kujali itikadi za vyama.

 

Wasaalam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo. 

By Jamhuri