Nianze kwa kuwapongeza kutimiza miaka makumi kadhaa ya Muungano, yaani Muungano ambao leo mnadai kuwa una kero ambazo sisi wakati tukiungana tuliona siyo kero za Muungano bali ni chachu za Muungano, na ndizo zinazofanya utamu wa Muungano kuwapo. 
Sina hakika, lakini nadhani inatokana na watu wengi kuelimika katika tasnia ya haki, sheria, siasa, madaraka, ukiritimba, utamaduni na ujazi wa demokrasia ndani ya Taifa letu. Naomba kuuliza, kero gani ya Muungano ambayo haina nasaba ya madaraka, ubinafsi na siasa? Hongereni pia kwa kuwa na elimu hiyo ya Katiba na Muungano. 
Mbali ya hiyo, napata taabu kufanya tathmini ya mambo yanayolikabili Taifa hili kwa sasa likiwamo suala la Katiba, lakini na masuala mengine muhimu kwa mustakabali wa Taifa lenye neema na nguvu kazi katika miaka michache ijayo. 
Nathubutu kusema kuwa Bunge hili litakapoisha, tuanzishe mijadala mingine kama vile tatizo la malaria, biashara ya bodaboda na hatima ya nguvu kazi, sheria za raia na barabarani na utekelezaji wake, dawa za kulevya, uwekezaji na madhara yake, uingizaji bidhaa feki nchini, rushwa na gharama zake, ugaidi unaochipuka na athari zake. 
Hii ni mijadala michache inayoweza kufanywa na wananchi na kuundiwa tume itakayoweza kukusanya maoni mapema, ili kukabiliana na changamoto ya kuwakosa wananchi walioko katika hatari ya kuangamia kutokana na madhara yanayoweza kupatikana.   Ukweli sitaki kuamini kama nchi yetu ina viongozi ambao wanafuata sheria ambazo hazishikiki kwa maana ya kwenda na wakati. Kuna mambo ya hatari ambayo kimsingi yanatakiwa kupewa tahadhari ili kuweza kukabiliana nayo. 
Nchi yetu ina matatizo mengi, lakini tatizo kubwa sana ni la elimu. Suala la afya silipatii umuhimu sana kwa sababu siyo ufumbuzi wa elimu ila elimu ni ufumbuzi wa afya, hiyo ni falsafa yangu haihitaji mjadala wa kupima nguvu ya hoja ndani ya falsafa hiyo. 
Wakati tukipata uhuru tulijipangia vipaumbele vyetu kutokana na mazingira tuliyokuwa nayo na tukiamini kuwa tunatakiwa kujitegemea baada ya muda mfupi. Moja ya vipaumbele hivyo ni elimu, afya, kilimo, ushirika na uongozi thabiti. 
Leo napenda nizungumzie elimu na madhara yake kwa kupuuza vipaumbele tulivyoviweka. Elimu ndiyo msingi mkubwa wa mtu kujitambua, kutambua na kutambuliwa. Elimu ni kinga ya maradhi yote ya kipumbavu, elimu ni msingi wa maendeleo, maendeleo ambayo hayapimwi kwa kigezo cha fedha. 
Kwa bahati nzuri tuliweka msingi mzuri wa elimu enzi zetu, tulijihakikishia kuwa kila Mtanzania lazima apate elimu ya msingi. Ndani ya elimu hiyo tuliweka mtaala wa elimu ya kujitegemea na ndiyo maana miaka michache tulikuwa na mafundi wengi, wakulima na wasomi wengi, wafugaji wa kisasa wa kutosha, wauguzi wa awali wa kila nyanja kama ukunga, huduma ya kwanza, manesi, na madaktari wa awali wengi. 
Tulianzisha vyuo vya kati kwa masomo ya kumwendeleza kijana aliyeshindwa kuendelea na masomo ya juu. Tulianzisha kisomo cha watu wazima kukabiliana na changamoto za haraka kwa kizazi kilichokuwa hakina hatima ya muda mrefu. Tulifundishwa katika viwanja vya michezo kwa sinema na madarasa yanayotembea kutoka kwa wataalamu wetu wachache. 
Hali hii iliendelea kwa michango ya wazazi kujitolea kwa manufaa ya watoto wao, kupata vitabu bure kutoka serikalini, madaftari, chaki, rula, walimu na kadhalika. Ulikuwa moyo wa kizalendo. Uzalendo ambao si wa kuigiza kama ilivyo leo, ambapo mzalendo ni yule anayetafuna rasilimali za Taifa akijificha kwa kutumia kalamu na sheria. 
Wakati wetu wa kusoma tulifundishwa mambo mengi na zaidi ya elimu ya kujitegemea pia tulifundishwa jinsi ya kuchukua tahadhari dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza, yaani ‘risk management’ kama mnavyoiita siku hizi kisiasa. 
Nawapenda sana wale wachache wanaoyaona madhara mbele yetu na wakathubutu kutamka kuwa hapa tunafanya makosa hata kama kauli zao zinabezwa na hao wanaoitwa wazalendo wa kweli kwa Taifa lao la wasomi wanaokaririshwa kila siku na kushindwa kujua hatari inayowakabili. 
Ni kiongozi gani ambaye ameona madhara ya bodaboda, dawa za kulevya, dawa feki, uvunjifu wa sheria, rushwa, bomu la ajira, malaria na kwamba baada ya miongo kadhaa tutakuwa hatuna vijana wa kuliendesha Taifa hili zaidi ya watoto na wazee, na kiongozi huyo akajiita ni kiongozi mahiri nchini? Tafakari, chukua hatua. 
Wasaalamu,
Mzee Zuzu
Kipatimo.

By Jamhuri