Yah: Naanza kuandika historia ya maisha yangu (3)

Kijiji kikawa na imani nami na kuamua kwa kauli moja katika mkutano wa hadhara kuwa niwe meneja wa duka na basi la kijiji. 

Hapo changamoto zilianza kujitokeza, kwa kuwa nilipaswa kuwa kiongozi wa basi letu, pia liwapo safarini na wakati huohuo nikirejea niwe ninapitia mahesabu na dukani na kuagiza bidhaa ambazo zimepungua. 

Hivyo kamati ya maendeleo ya kijiji ikatangaza kuniajiri na mshahara wangu ulikuwa shilingi mia moja na kumi na tano kwa mwezi.

Mwanga wa maisha bora kwangu na kijiji ukaanzia hapo. Tukafanikiwa kuwa na maendeleo ya vitu vingi vya msingi. Tulijenga shule yetu wenyewe bila kuitegemea serikali, tulijenga zahanati yetu mpaka ikakamilika, tukamtuma mbunge wetu aende kuomba walimu na maofisa afya kwa ajili ya kijiji. Japo hatukuwa na umeme na maji ya bomba lakini tuliishi maisha matamu sana.

Awamu yangu ya kwanza ya uongozi ilianzia katika ngazi ya chini kabisa.Mafunzo ya masista yalinijenga katika kuwatumikia wananchi. Kuna kitu kilipandwa katika fikra zangu za kujiona mimi ni mtumishi wa watu na sitakiwi kutumikiwa, nilijisikia fahari kuanza kuwatumikia watu.

Yalipokuja maazimio mbalimbali ya chama, nilipewa jukumu hili na baadhi ya vijana wasomi wa darasa la saba tulichambua matamko mbalimbali ya nchi kwa ajili ya wananchi wetu. Tulijua maana ya kujitegemea na kuilinda nchi yetu, tulianzisha darasa la siasa ni kilimo na kisha darasa la ulinzi wetu na wa mali zetu.

Mwanzoni mwa miaka ya sabini, lilikuja agizo jingine la kila mtu afanye kazi, lakini agizo lilianza na juhudi za awali kabisa katika kuyatenga maeneo ya kuishi pamoja na maeneo ya hifadhi za taifa. Ni wakati huo ndipo umuhimu wa kuwahi kutayarisha maeneo yetu ulipodhihirika rasmi kwamba hatukuwa tumeishi mahali ambapo palitengwa kwa ajili ya matumizi mengine. Lakini kubwa zaidi ni kwa jinsi ambavyo tulikuwa tumeendeleza eneo letu kwa maana ya kijiji na kukisajili.

Ilikuwa ni furaha kwa wazee wetu kuona kuna mwanga wa matumaini kutoka kwa viongozi wao vijana. Lengo  la kwanza kuwatumikia wananchi likawa limefikia muafaka na lengo la pili la mimi kufanya kazi kama mtu mwenye wajibu kwake na familia nalo likawa limetimia.

Maisha ya kujitolea katika kipindi changu yalihitimishwa vizuri na moyo wa uzalendo kuanzia kwangu hadi walionizunguka. Kila mmoja alifanya kazi yake kwa moyo wa dhati akiamini kuijenga nchi yake na kuilinda nchi yake. 

Kwa ufupi kulikuwa na kipindi kifupi cha nchi yetu kuwa ya maziwa na asali, aliyemaliza darasa la saba na kama hakuchaguliwa alipata kazi katika viwanda mbalimbali.

Aliyemaliza kidato cha nne alipata kazi kabla hata ya matokeo ya mitihani na hali kadhalika aliyemaliza kidato cha sita alipata kazi nzuri zaidi na yenye mshahara mkubwa. Kwa wakati wetu mtu aliyemaliza chuo kikuu alikuwa si tu kwamba anachagua kazi, lakini alikuwa akibembelezwa kufanya kazi sehemu mbalimbali. Nchi ilisheheni viwanda na mashirika makubwa yaliyohitaji wafanyakazi wengi.

Historia ya maisha yangu inakwenda mpaka tulipoingia wakati wa vita ya Uganda. Lilipigwa baragumu tena na mimi mwenyewe baada ya kupewa idhini na mwenyekiti wangu wa kijiji, tukaambiwa kuna taarifa za uvamizi katika taifa letu. 

Tukaambiwa tujitayarishe kwa ajili ya vita, tukaambiwa tuorodheshe majina ya watu wote waliopitia mafunzo ya kijeshi na mgambo, tukawa na kundi kubwa la vijana ambao walikuwa tayari kwa mapambano ya Nduli.

Jukumu langu kubwa lilikuwa ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya utulivu kipindi cha vita na kutoa michango mbalimbali kwa ajili ya vita. 

Jambo jingine lilikuwa kuwaandaa wananchi kisaikolojia kuelewa kwamba vita hii ni yetu sote, si ya wanajeshi peke yao. Kama kijana mwenye weledi nilijipanga kuhakikisha kwamba kila kitu kinakaa vizuri katika himaya yangu pindi ajapo kiongozi niwe na taarifa kamili ya maandalizi.

Ninakumbuka majukumu yaliongezeka sana. Awali nikageuka kuwa mtunza stoo ya kijiji, michango ya wananchi kama chakula na  mifugo nilikabidhiwa ili nami niukabidhi uongozi wa ngazi ya juu yangu. 

Wakati ule si kwamba tulikuwa tumelishwa uzalendo, la hasha! Ninahisi tulikuwa tumeuvaa uzalendo wenyewe.  

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

640 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons