Wanangu, naamini hamjambo baada ya kupumzika nyumbani na kutafakari maisha yenu ya miaka ijayo na hatima ya kizazi chenu cha dotcom. Sina hakika miaka michache ijayo baada ya dotcom kuzeeka, sijui kutakuwa na kizazi gani?

Wanangu, kuna wakati huwa napata fursa ya kuangalia hizo ziitwazo televisheni au vionambali. Huwa naona sinema za maendeleo, naona mambo ya kufikirika, huwa naona picha za watoto, huwa naona miziki yenu ya kizazi kipya na kuporomoka kwa maadili.

 

Kuna wakati huwa naamua kufunga macho ili angalau siku zangu za kuishi zipate kuwa nyingi hapa duniani. Nasema hivi kwa sababu nakumbuka katika vitabu vitakatifu tunaaswa kuwa tukiheshimu wazazi siku zetu zitakuwa nyingi hapa duniani.

 

Nakiheshimu sana chombo chochote kinachoitwa cha Taifa. Viko vyombo vingi vya kitaifa ambavyo vinafanya madudu, lakini madudu yake yanaweza yasiwe dhahiri kwa sababu hayaonekani moja kwa moja. Kwa upande wa chombo chochote cha habari cha Taifa kunatakiwa kuwe na umakini wa hali ya juu ili kuwaridhisha watazamaji wa kitaifa.

 

Naweza kuwa ni mkosaji kuwasemea walio wengi na hasa kama ni dotcom pia, lakini naweza kuwa na ushauri mzuri kwa kizazi kijacho na kilichopo ili kesho tuwe na mahali pa kuanzia kutoa lawama kwamba hapa ndipo ulipokuwa msingi wa kuporomoka kwa maadili yetu.

 

Nafahamu kwamba hivi sasa kuna vyombo vingi vya habari, na ili viendelee kuwapo ni lazima viwe na wasikilizaji, watazamaji na wasomaji. Vyombo hivi vingi ni mkusanyiko wa vyombo vya watu binafsi na mashirika mbalimbali yenye mlengo tofauti katika kufikisha ujumbe.

 

Leo nimeona ni vema nikazungumzia Televisheni ya Taifa ambayo mimi ni muumini mkuu wake hata kama siitazami mara kwa mara kutokana na matangazo yao. Nasema ni muumini kwa sababu fikra zangu za TBC ile ya pale kiwanda cha bia bado iko katika kichwa changu.

 

Najua zipo televisheni nyingi za mataifa mbalimbali na jinsi ambavyo zinafanya kazi. Najua kuwa kuna wakati utafika ambapo suala la habari litakuwa na nguvu na kuilazimisha Serikali kulazimika kukubali kuwa mhimili mwingine wa dola, lakini wasiwasi wangu ni pale tutakapolazimisha mhimili huu wa ki-dotcom zaidi kuwa na mashiko.

 

Wanangu, mimi ni mzee kwa sasa, lakini nina haki zote za msingi za kupata habari kwa ukweli wake na kupata elimu kila siku kupitia vyombo vya habari, ni haki yangu ya msingi hata kama inanigharimu fedha, lakini si haki yao ya msingi kunilazimisha kujifunza upuuzi kupitia magazeti, redio, televisheni na mitandao mingine ya kijamii.

 

Wanangu, leo nimewiwa deni kubwa kuwakumbusha wenye dhamana ya chombo cha serikali cha habari. Najisikia vibaya kila ninapofungulia chombo kinachoitwa cha serikali, labda hii inatokana na kuviangalia vyombo vingine vya kitaifa na kulinganisha na hicho chetu kiitwacho cha Taifa.

 

Awali, nimesema naikumbuka TBC ile ya ujana wetu, huenda nikawa nafanya kosa, lakini hebu tujiulize ilitunufaisha vipi Watanzania ambao wengi wetu tulikuwa masikini wa elimu na uchanga wa Taifa hili. Je, watangazaji wetu wa wakati huo walikuwa na mlengo gani wa kufikisha ujumbe?

 

Wanangu, ni kweli kwamba dunia inabadilika na hakuna mabadiliko yasiokwenda na wakati, lakini tunapaswa kujua ni mabadiliko gani ambayo yanatulazimisha kufanya mambo ya kijinga katika jamii kwa kisingizio cha kwenda na wakati.

 

Wanangu, najua kuwa kuna ushindani wa kibiashara, maana kwenye biashara kinachotazamwa ni faida zaidi na si matokeo ya kile kilicholeta faida. Lakini katika hili la biashara hatuna sababu ya msingi ya kulazimisha chombo cha Serikali ambacho kinaendeshwa kwa ruzuku itokanayo na kodi za wananchi kufanya biashara na kuliacha Taifa katika mkondo mwingine wa utamaduni usio wetu.

 

Najisikia vibaya kwa sababu nina kitu ambacho labda ninafananisha na hiki kiitwacho cha Taifa yaani Televisheni ya Taifa; Televisheni ya Taifa ambayo tunaangalia kile kinachoonyeshwa ili tujifunze na tukitumie kwa manufaa ya Taifa letu la leo na kesho.

 

Wanangu, kila linapotokea jambo zito hapa nchini jambo la kwanza ninalofanya ni kukimbilia katika vituo vya Taifa kupata ukweli wa jambo hilo. Cha ajabu kila ninaposikiliza na kuangalia huwa naona kichefuchefu, mathalani kuna ajali mbaya ya gari au meli utaona Televisheni ya Taifa inaonyesha muziki wa ki-dotcom.

 

Sipendi kufananisha na vituo vingine vya mataifa yaliyoendelea, lakini naamini hata sisi tuna mambo mengi ambayo tunapaswa kuyaangalia na kusikiliza ya maana zaidi kuliko hayo ambayo labda yapo kibiashara. Tuna mambo ya maana sana katika kilimo, viwanda, historia na kadhalika.

 

Napata tabu sana ninapoona vyombo vingine ambavyo si vya kitaifa na wala havina ruzuku vinapokuwa na vipindi vizuri vya elimu na matukio ya dharura  vikionyesha; na chombo chetu kiitwacho cha Taifa kikiwa na kipindi kingine kabisa tena kisicho na tija.

 

Wanangu, nazidi kulalamikia Televisheni yetu ya Taifa kuonesha miziki tena isiyo na staha wakati kuna mijadala mizuri iliyopo mbele ya Taifa ikisubiri kutatuliwa, na kuna taarifa nyingi za Serikali ambazo hazijawafikia wananchi ambao ndiyo wamiliki halali wa chombo hicho.

 

Mimi nazeeka, lakini kuna mambo ambayo kamwe sitayasahau na nimejifunza kupitia TBC ya zamani na  Redio Dar es salaam na mwishoni Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ambayo leo mnaiita TBC Taifa. Nimejifunza ukulima wa kisasa, ufugaji, ujamaa, ushirika, umoja na amani, mshikamano, ulinzi, biashara na kadhalika.

 

Naweza kusema namshukuru Mungu kuwa baadhi ya vipindi hivyo bado vipo TBC Taifa japokuwa baadhi yake vimepoteza mwelekeo. Yawezekana ni kutokana na kutokuwa na ratiba nzuri ya kuvitangaza – wakati wa ukame tunafundishwa kilimo cha wakati wa masika, hapo bado ndipo kichwa kinaponiuma!

 

Lakini Televisheni yetu ya Taifa siiungi mkono kamwe, ni mara chache sana sana wanaweza kwenda na jambo kwa wakati. Televisheni yetu ningependa niifananishe na kampuni ya filamu miaka ile ya ujana wetu ambako tulioneshwa kilimo cha kisasa, hotuba za viongozi wa TANU zenye kuhamasisha mshikamano baina ya Watanzania na wakati mwingine matukio ya hatari na jinsi ya kujihami.

 

Leo televisheni yetu mbali ya kutoonekana vizuri na kuwa na ubunifu wa matangazo yake, muda mrefu hatuoni jambo la kutufundisha kama ilivyokuwa wakati wa Kampuni ya Filamu Tanzania. Najua kuwa wao ndiyo wenye maktaba nzuri ya matukio mengi muhimu ambayo yangeweza kuliokoa Taifa hili katika mambo ambayo yanajiri kwa wakati husika.

 

Wanangu, hivi sasa Tanzania tuna mgogoro wa dini. Hivi hatuna hotuba nzuri za viongozi wa zamani waliofanikisha kupiga vita suala la udini hadi tukafikia kuwa ndugu? Hatuna kipindi chochote ambacho kinaweza kutufundisha mshikamano tuliokuwa nao zamani ambao sasa ni mpasuko na mnyukano ulio mbele yetu? Nini dhima ya chombo cha Serikali katika kutoa tahadhari na kufundisha?

 

Iweje vyombo vingine visivyo vya Serikali vinaweza kuonesha mambo mazuri na kwa wakati, lakini chombo chetu tunachokiendesha kwa kodi zetu kiwe kinasuasua kila siku kwa visingizio vya hapa na pale? Nawakumbuka watangazaji wengi sana na wengi wao wako mbele ya haki waliokuwa Redio Dar es salaam na mwanzoni mwa Redio Tanzania kwa kazi nzuri ya kuhamasisha maendeleo, mshikamano na amani katika Taifa hili.

 

Walitoa burudani za miziki yenye mafundisho katika vipindi maalumu kama, Wakati wa Kazi, Ugua Pole, Chaguo la Msikilizaji, Ngoma Zetu, Weekend Show na walizingatia muda wa kazi za msikilizaji na muda wa kutoa burudani.

 

Hainiingii akilini kuona Televisheni ya Taifa inapiga muziki wa kizazi kipya saa tano asubuhi badala ya kuwa na mwalimu anayefundisha wakulima au wanafunzi!

 

Hainiingii akilini kupiga muziki usiku wakati tungeweza kuona marejeo ya mijadala mbalimbali ya viongozi wa zamani, sasa, Bunge, vipindi vya utalii, na kadhalika.

 

Naahidi kuendelea kulizungumzia hili tena na hasa hasa kwa televisheni yetu ambayo inabidi ibadilike ifanye kazi ya kitaifa si kukuza miziki ya dotcom, kutuonesha maungo ya wasanii, kutufundisha matusi kupitia miziki hiyo na kutuzalishia kundi la watoto wavivu ambao kazi yao ni kukaa nyumbani kuangalia TV ya Taifa ikimwaga radhi!

 

Kwa kweli nasikitika sielewi nisikilize nini, nitazame nini au nisome nini; kisa ni maendeleo. Sielewi wenye dhamana wanaweza kuwa na kumbukumbu kama zetu kuikabili Redio Dar es Salaam au Redio Tanzania. Naikumbuka TBC ya kweli, siyo yenu ambayo ipo ki-dotcom kabisa.

 

Wasalaam

Mzee Zuzu

Kipatimo

 

 

 

By Jamhuri