Siku ya kwanza naamka asubuhi naona jua limechomoza, nimechoka akili na mwili kwa kazi ngumu na nzito kwa maendeleo ya kaya yangu. Nawaangalia wanangu na Mama Chanja hali kadhalika wamesawajika kwa kilichotokea. Hakuna uchawi wala mazingaombwe ni uwajibikaji wa nguvu ya jana yetu kwa ajili ya kihenge chetu.

Siku inapita bila kuonana kutokana na kazi. Kaulimbiu ni Kilimo cha Kufa na Kupona. Nawaangalia wafanyakazi wa maofisini na viwandani wakiheshimu kulipa fadhila za kuendeleza pale tuliapochiwa jana yetu. Siku hizi starehe hakuna tena ni kujenga nyumba yetu iliyokuwa ikikaliwa na mgeni. 

Muziki upo kwa ajili ya kutupa ari ya uzalendo. Tunajenga nguvu ya kushirikiana kufanya kazi pamoja na kuzalisha kwa wingi ili tusiwe tegemezi. Kwa umaskini wetu tunakiri tutaweza kujitegemea na tunaweza. Tunapinga kuonewa, tunakataa utwana na ubwana na wote tunakubaliana kufanya kazi.  Inawezekana na tunafanikiwa na ndiyo maana kila siku kwetu ni uchovu wa kazi ya jana. 

Siku ya pili naamka nikiwa na uchovu wa kinywaji cha jana tena nikitafutwa na marafiki zangu twende tukazimue ili kutoa uchovu na kuingiza uchovu mpya. Ni siku mpya inayoashiria vikao vingi vya kupokezana kulipa bili za vileo. Sijisikii kwenda kazini lakini wenzangu wameandikisha jina tayari na mwisho wa mwezi ni kitu mfukoni. Maisha yanaenda, sisikii la mwadhini wala la Mama Chanja.

Ni siku ambayo natumia sana akiba yangu kutokana na kufanya kazi siku ya jana yake. Mipaka ya jirani yangu inafunguliwa na kila kizuri tunakiruhusu katika kaya yetu. Ni mfumo wa kaya zote duniani hatuwezi kujitenga. Siku hii inaruhusu wengine kuhoji mambo bila kuulizwa uhalali. Ni siku ambayo mshikamano katika mawazo inaruhusiwa kutenganishwa, mimi na majirani tunakuwa makabila tofauti, itikadi tofauti japokuwa uzalendo tunakuwa nao mmoja.

Siku hii inabadili sura ya maisha yetu. Ni kama tumetoka gizani na kuja nuruni. Tunaviona ambavyo hatukuviona au tulidhani ni hadithi. Siku inapita kwa usingizi mwingine.

Siku ya tatu asubuhi imeanza kwa kukimbizana kuangalia ninamiliki nini, lakini pia hakionekani. Nahisi sarafu imepunguzwa mtaani kwa kufichwa tofauti na jana, lakini napiga moyo konde kuwa liwalo na liwe. Nasikia kelele za mabishano ya watu juu ya nani wa kumsikiliza. Wengine wanasema siyo lazima nimsikilize yule wa jana na juzi, lakini nasahau hayo na kuambiwa dunia imebadilika nigangamale.

Sitaki kuamini kwamba majirani wanaweza kuja kuingia nyumbani kwangu kwa kigezo cha dunia duara. Ule uzembe wa kusahau fursa naanza kuuona. Najutia kudharau juzi yangu, lakini naanza kuona kaya yangu ikigubikwa na ushindani wa machinga. Siwezi kuwazuia kwa sababu ni sera ya wote tuliomo duniani, nakomaa nayo siku ipite.

Usiku wa kuamkia siku ya nne unanitia faraja. Ninabebwa na imani ya ‘pondamali kufa kwaja’ lakini naona mbio zinaongezeka, makelele ya kutaka kusikilizwa yanaongezeka, aliyesimama anatamka wazi kuwa mwenye malalamiko na mawazo mbadala aseme asikike. Wapo ambao wanautumia huo uwanja hata kutukana. Aliyesimama anacheka na kusema hii ni demokrasia, lakini tuheshimu mipaka.

Watu wanakimbizana kidogo na kushika kingi. Wanalima kidogo na kuvuna kingi. Watoto wengi wanaacha kulima na kufanya kazi. Wanabaini fursa pekee ya kuwa wafanyabiashara na madalali. Ni wakati wa mito kiuchumi wengi wananeemeka, lakini neema yenye maswali magumu yasiyopata majibu. Nayo ni siku inapita.

Leo ni siku ya tano ndiyo kwanza alfajiri. Kijasho kinanimiminika, nagombana na Mama Chanja kwa kosa la kusahau mipaka ya shamba letu. Nikimuuliza kwanini alikuwa haangalii anasema alikuwa anashinda katika vikoba na michezo ya kupeana. Ananitia wazimu, lakini na mimi najiuliza; majuzi juzi na jana kwanini sikukumbuka?

Ule wakati wa siku za nyuma kuwa neema ya kuvuna bila kupanda umepita, malezi ya vijana wetu kuwa tegemezi unawaumiza hawawezi tena kufanya kazi. Laana ya kuongea sana bila kufanya kazi inageuka kuwa ajira, lakini kaya inakataa maisha ya kubahatisha, inataka tufanye kazi. Naona hii ndoto kama mapito yake yameenda haraka sana, lakini nasema haya ndiyo maisha, nimeamka.

 

Wasaalam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

By Jamhuri