Wanangu, ka-jua ka leo kananikumbusha mandhari ya miaka mingi kabla Tanganyika haijaanza kuwa jangwa la kutisha na kushindwa kuhimili hali ya ukame na wakati mwingine kukosa maji ambayo yanasababisha hadi tukose umeme na kusababisha kuyumba kwa uchumi  wa mtu mmoja mmoja na nchi.

Nahisi ni maendeleo ambayo yametufikisha hapa na ndiyo maana huwa sielewi sababu ya msingi iliyotufanya miaka ile kuanzisha shule nyingi za msingi na kufundisha somo la kujitegemea na sayansi kimu kwa wanetu walioanza kuhitimu darasa la saba ilikuwa na maana gani.

 

Wanangu, kizazi ambacho kilisoma elimu hiyo wengi wao ndiyo wataalamu na viongozi wetu wa sasa ambao mnashuhudia haya madhira ambayo mnakumbana nayo na huenda kizazi hiki kipya cha dotcom nacho kitaingiza wataalamu na viongozi ambao watatawala na kuongoza makaburi yatokanayo na ukame, jangwa na matatizo ya kujitakia kutokana na tamaa.

 

Yawezekana nisieleweke vizuri na labda nikaonekana mchonganishi baina ya vizazi, la hasha! Ni vema nikaweka wazi kwamba kizazi chetu kilikuwa na dhamira nzuri ya kizazi kijacho. Tuliwafikiria wajukuu, vitukuu, na vilembwe na kizazi kilichofuata kilifikiria watoto wao tu bila wajukuu na huenda kizazi hiki cha dotcom kinajifikiria chenyewe bila hata kufikiria watoto wao.

 

Ni kweli na sitaki tubishane katika hilo, mifano hai ipo mingi na wakati mwingine haina tija sana kuisema, lakini kwa masilahi ya kuuweka ukweli bayana ni vema ikawa wazi kwamba tulijua kuwa tuna madini, lakini tuliamua kutochimba haraka hadi hapo tutakapojitambua.

 

Tulijua kuwa tuna mbuga za wanyama za kutosha na wanyamapori wazuri wanaotafutwa duniani. Tukaamua kuacha kuwinda kwa mtindo wa vitalu hadi hapo tutakapoimarisha ulinzi wa kutosha kutoka kwa majangili weupe na weusi.

 

Tulijua kuwa tuna maeneo mazuri ya kilimo, tena yenye rutuba ya asili, lakini hatukuwakaribisha waitwao wawekezaji ambao watatumia eneo kwa masilahi yao na kuliacha baada ya kuchuma walichokitaka na kutuachia eneo lisilo na rutuba na tija kwetu.

 

Tulijua kuwa tuna misitu mizuri ya asili na tukaamua kuongeza miti ya kupanda ili kuzuia kuharibika vyanzo vyetu vya maji na kuwa na ratiba nzuri za mvua za kilimo ili tupate mavuno ya kutosha. Hatukufikiria kuuza maeneo hayo ili miti ikatwe, isafirishwe kwenda nje na sisi kuachiwa makapi yasiyo na maana pamoja na jangwa lake.

 

Nilieleza jinsi ambavyo tulifanya kazi ngumu kwa kuamini kuwa malipo yetu ya rupia hayakuwa na maana sana zaidi ya hiki ambacho kinaonekana leo. Barabara kuu, njia za reli, mabohari ya msingi, uanzishwaji  wa vijiji ambavyo leo vingine ni miji, miundombinu ya umeme kwa maana ya vyanzo vya maji, utaifishaji wa mali za wakoloni, kujenga zahanati nyingi ambazo leo baadhi yake ni hospitali kubwa, kuanzisha mafunzo ya awali kwa wakunga na madaktari wa awali, nakadhalika.

 

Nina huzuni kubwa moyoni kwa kutojali haya na kuyaangalia kwa jicho kali ambalo tulikuwa nalo enzi zetu. Huenda huo ndiyo u-dotcom kwamba chetu ni chetu na mjanja ni yule mchumia tumbo na siyo mchumia ghala kama ambavyo sisi tulidhani changu ni chetu sote kwa maana ya ujamaa.

 

Napata tabu sana na nina imani hata wazee wenzangu wanapata taabu hii hii niliyonayo na pengine kwa jicho la haraka tukitazamwa tunaweza kudhaniwa kuwa ni wanachama wa vyama vingine vya siasa na kwamba tumekiasi chama chetu cha TANU ambacho kilizaa CCM kwa kukichukia kwa matendo yake ya kubeza yale ambayo tuliona ni ya msingi yakatusukuma kudai Uhuru wa nchi hii iliyokuwa chini ya mkoloni.

 

Tulidai Uhuru bila kuogopa kwamba kuna siku mkoloni atatushikia rifle na kuamua kutuua, hatukuogopa mabomu tukiamini tunachodai ni haki yetu ya msingi kujitawala na kujiamulia mambo ya msingi sisi wenyewe. Tuliamua hivyo bila kujua busara yetu tunayotumia kudai Uhuru haitamwaga damu, bali itatupatia ushindi wa Uhuru.

 

Wanangu, naomba mniwie radhi na ashakumu si matusi kama nikisema mnatutuma tutupe maganda ya ndizi ambazo mmekula, tutawasimulia wajukuu zetu ambao kamwe hawatasahau jinsi ambavyo babu zao na bibi zao wametendwa.

 

Kama wajukuu kwa akili yao ya mitaala mipya ya elimu watagundua kuwa sisi tulikuwa sahihi kudai Uhuru na kuyatunza mazingira na mali kwa manufaa yao, lakini yametumika vibaya, basi nguvu ya maji itakuja na hapo wale wachache waliogeuza mtaala wa elimu ya kuchumia tumbo wataulizwa na kwa vile sababu ya msingi itakuwa haipo, itabidi watumie nguvu. Hapo damu itamwagika nyingi sana.

 

Kuna wakati fulani miaka ya sabini na tano- sina kumbukumbu vizuri ni mwezi gani na tarehe gani- niliwahi kusikia katika taarifa ya habari baada ya ngoma za kijana mwenzangu marehemu Moris Nyunyusa kwamba Rais wa Uganda amemteua aliyekuwa mesenja wa Benki Kuu ya Uganda kuwa gavana mpya baada ya gavana wa awali kukataa kuchapisha fedha ambazo rais huyo alikuwa akizihitaji.

 

Kila mmoja wakati wetu alishangaa, na kumbukeni kuwa wakati wetu tulisema fedha siyo msingi wa maendeleo, bali siasa safi ardhi, watu na viongozi bora. Tuliamini kuwa pesa ni matokeo ya kazi. Kwa hiyo kila mtu na hasa Mtanzania alimdharau sana kiongozi yule.

 

Siku chache baadaye akaibuka na kisa kingine baada ya kufanya mauaji, alihutubia na kutamka kuwa nanukuu, “Ili sheria iweze kufuatwa ni lazima damu ya mtu imwagike.” mwisho wa kunukuu.

 

Nadhani ndiyo maana tulimwita nduli kwa sababu ya kitendo chake cha kumwaga damu na tulimchukia yeye kwa matendo yake na tuliwaonea huruma Waganda kwa matendo yake na alipojaribu kutuchokoza kule Kagera tukapata sababu ya kumfuata hadi Arua tukahakikisha ameondoka.

 

Wanangu, nimesema haya kwa sababu nyingi. Kwanza, nakumbuka Tanzania ninayoijua mimi hatukuwahi hata kufikiria kupigana na taifa jingine au hata sisi kwa sisi. Tulijenga uhusiano mzuri na mataifa yanayotuzunguka na tukavunja makabila ili tuwe taifa moja.

 

Wanangu, wiki jana nasikia mmeendelea kuuana huko Iringa sehemu moja ambayo inaitwa Nyololo. Kama mtakumbuka katika barua yangu moja niliwaambia kuwa hapo ndipo nilipoachia kazi ya kubeba darubini wakati tukijenga barabara hiyo iendayo Zambia.

 

Kwa hiyo nilipoambiwa kuwa ni Nyololo picha ilinijia Nyololo ile ya wakati ule ya watu wa kuhesabia kwa vidole. Nikajiuliza hivi kwa sasa wapo watu wengi kiasi cha kusababisha maandamano?

 

Leo wanangu naandika barua hii nikijua fika kuwa tayari mambo si mambo katika nchi yetu. Tumekuwa tukimwagana damu bila sababu ya msingi na kwamba damu hiyo haisababishi kufuatwa kwa sheria, bali  ni kupindishwa kwa sheria.

 

Nahofia nguvu ya maji ambayo inaweza ikasababisha tushindwe kuzuia na hapo ndipo mchawi atakapotafutwa kwa udi na uvumba na siku zitakuwa zimeisha.

 

Tanzania ambayo kila mtu alijua ni kisiwa cha amani itabaki kuwa hadithi kwa vilembwekezi vyetu kuwa ilikuwa hivyo zamani na tukaichezea.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

1017 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!