Yah: Ni Tanzania tu mzawa anaponyanyaswa na mgeni

Sasa hivi naitafuta Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – iwe ile ya zamani au hata hii mpya – ambayo haijapigiwa kura na kupitishwa na Watanzania.

Tanzania ni moja kati ya mataifa yaliyokuwa na heshima sana kwa raia wake miaka kadhaa iliyopita, ni nchi iliyoheshimika kwa usalama wake na kuwajali wananchi wake, ni nchi iliyokuwa na sauti duniani kwa misimamo yake, heshima ambayo sasa hivi inabidi tuirudishe kwa nguvu zote.

Siku za hivi karibuni tumekuwa tukisikia vilio vya Watanzania juu ya kufanyishwa kazi kupita kiasi na hao wanaoitwa wawekezaji, kutolipwa stahiki zao kwa wakati na pengine kutojua stahiki zao kisheria kutokana na kupindishwa kwa sheria na haki za Mtanzania. Sasa hivi ndiyo tunajua baadhi ya mambo ya msingi kutokana na baadhi ya Watanzania wenzetu kuanza kuonekana walikuwa wakipindisha sheria kwa ‘ulua’ mdogo sana.

Watanzania tunaanza kufunguka macho kila siku tunapojua kuwa baadhi ya wenzetu walitugeuka na kugeuza sheria za nchi kuwa shamba lao la kuvuna mabilioni ambayo kimsingi hayaisaidii nchi wala wao wenyewe, wamelipora Taifa fedha nyingi na kuzificha bila kutumia huku wakivunja sheria na kuwaacha Watanzania wakiwa katika mateso makubwa ndani ya nchi yao huru.

Mambo yote haya yametokana na kugeuza dhana ya madaraka ni amana na kuwa madaraka ni urithi, sasa tunaanza kuivunja dhana hiyo na baadhi yao wameanza kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania wakiaminisha kuwa utawala huu ni wa kidikteta. Naapa nitakuwa wa mwisho kuamini na kupigania hilo, naapa nitaunga mkono hadi tone langu la mwisho la damu kuwaombea wote wenye kutenda haki kwa Watanzania.

Siku za hivi karibuni nimepatwa na mkasa ambao sikuutarajia katika maisha yangu na nchi yangu. Nimezuiliwa kuingia katika nyumba na hata kupita nje ya jengo hilo linalomilikiwa na nchi yangu kama kitegauchumi na mtu anayeitwa mwekezaji Mturuki. Kwa jeuri kubwa kabisa anasema hawezi kunipa sababu za kunizuia lakini hanipendi tu.

Nimemwandikia barua anieleze sababu za kunizuia hadi njia ya kuelekea kwangu lakini hataki kunijibu na badala yake anawatuma walinzi ambao ni Watanzania wenzangu wanaolipwa kidogo sana wanizuie nisisogee eneo hilo kwa manufaa ya matakwa yake. Namkumbuka sana Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na haki za Mtanzania.

Nimejiuliza maswali mengi kutoka kwa Watanzania maelfu kwa maelfu jinsi wanavyonyanyasika na kukosa huduma muhimu, lakini wageni wakiufurahia uhuru ya nchi yetu na kula matunda ya uhuru wetu na sisi tukiendelea kunyanyasika huku tukiwa na viongozi ambao ni Watanzania wenzetu. Swali ni je, hawa viongozi wamenunuliwa kiasi gani hadi waamue kuificha Katiba ya nchi yetu kwa manufaa ya wageni?

Nchi hii sasa hivi Wachina wameshika hatamu kwa kuwapiga Watanzania, kuwafanyisha kazi pasi na malipo halali, je, wawekezaji wana nguvu kuliko vyombo vyetu vya dola? Hivi uamuzi mgumu wa kutumbua majipu unaofanywa na Rais kwanini tunaulaani? Au kwa kuwa anagusa maslahi ya watu wachache wakubwa waliokuwa wanatumia madaraka yao vibaya kwa kwa faida yao?

Sipendi kuaminishana vibaya kwamba wanaonewa hao wanaotumbuliwa, lakini nataka niseme kuwa ni vema sasa akatumbua na majipu mengine makubwa zaidi ili Watanzania tuishi kwa amani ndani ya nchi yetu. Ni vema tukawa maskini lakini tukiwa huru kuliko kuwa matajiri watumwa.

Nimeamua kuzungumzia hili na nitaandika kwa kina waraka huu kuanzia sasa ili mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ujue wahanga wako na uwafanyie kazi; waziri wa uwekezaji uwajue wawekezaji wako, waziri wa sheria uweze kusimamia Katiba na tusisubiri Rais aendelee kutumbua majipu wakati nyie mpo. Narudia kusema kuwa Tanzania ni nchi pekee duniani ambayo mwenye nchi ananyanyaswa na mgeni. Tuone aibu wenye mamlaka.

Mungu ibariki Tanzania na uhuru wetu

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.