Wanangu, leo najua ni Jumanne nyingine ambayo mtakuwa mnatafakari mustakabali wa maisha yenu baada ya kuwa kila siku inayopita mnaona nafuu ya jana. Haya yote yawezekana ni kutokana na kosa lenu la kupiga kura katika kumchagua kiongozi wako kuanzia ngazi ya tawi hadi juu kabisa.

 

Ni dhahiri kuwa kiongozi mmoja hawezi akabadilisha maisha ya wengi kama viongozi wengine watakuwa hawamsaidii kiongozi huyo, na hii inatokana na dhambi ambayo itakuwa imefanywa na mpiga kura.

 

 

Wanangu, nimekuwa nikijaribu kila siku iendayo na mambo yake kuandika waraka wangu kwenu kujaribu kuwakumbusha yale machache ambayo sisi wazazi wenu tuliyapata siku chache baada ya Uhuru. Nawaeleza utamu wa maisha tuliyoishi na adha ambayo tunaiona pamoja na kwamba leo kuna kila kitu. Vitabu vitakatifu vinatufundisha juu ya kuheshimu mamlaka iliyoko madarakani; na ni vitabu hivyo hivyo vinavyowakumbusha walioko madarakani kuheshimu waliowaweka madarakani kwa kuwa hakuna mtawaliwa kama ikiwa hakuna mtawala.


Viongozi ndiyo wenye dhamana ya maisha yetu na sisi tunawategemea wao ili tuweze kuwa na maisha bora na kwa kweli hakuna kiongozi ambaye anachukiwa na anaowaongoza kama waongozwa hawaoni mustakabali wa maisha yao ikiwa nzuri.

Tanganyika naijua zaidi ya Tanzania . Ni kama vile alivyokuwa anasema Julius enzi za uhai wake. Yeye alikuwa anaijua kiutawala zaidi, mimi naijua Tanganyika Kijerumani zaidi. Naijua kwa ramani na rasilimali ambayo ipo ndani ya Tanganyika na siyo rasilimali iliyopo Tanzania sina hakika nayo sana.


Wanangu, leo ni siku mojawapo kati ya siku chache ambazo zinahitimisha miaka ya awamu ya utawala uliopo madarakani. Tumeshuhudia katika Mkutano Mkuu wa chama uliofanyika Dodoma hivi karibuni kiongozi mkuu wa chama akiwaonya viongozi wenzake katika kupigana na vita ya rushwa ndani ya chama chake.


Mwenyekiti alionekana mkali sana juu ya suala la rushwa na anajua kuwa rushwa imetawala katika ngazi mbalimbali za uchaguzi wa chama chao. Alisema kiongozi bora kamwe hawezi kupatikana kwa rushwa. Aliwaonya wanachama wake juu ya rushwa akiamini kuwa uamuzi wao unaweza kuiweka njia panda dola waliyonayo sasa.


Zaidi ya rushwa, alipiga mayowe ya kisiasa kusisitiza kufuta makundi ndani ya chama; makundi ambayo kila mwanachama na Mtanzania wa kawaida anajua kuwa yapo kwa masilahi ya madaraka ya awamu ijayo. Yeye alikiri na kujinasua kuwa hayuko upande wowote wa makundi. Hilo ni jambo jema maana yeye angekuwa katika kundi lolote, basi kundi hilo lingekuwa na kura ya turufu.


Wanangu, nimeamua leo kulizungumza hili kwa sababu kubwa mbili. Awali, ni kwamba sasa namjua rais ajaye, ni rais ambaye hatakuwa mwanachama wa mtandao wowote wa kiongozi wa rushwa, yaani aliyechaguliwa kwa nguvu ya fedha, bali kwa nguvu ya hoja.


Pili, namjua kiongozi na rais ajaye kuwa ni yule asiyetoa rushwa na hata kama tukimwangalia usoni hatutakuwa na shaka naye juu ya suala la rushwa.


Huu si mtihani mkubwa wa kumjua mtu wa namna hiyo. Ni suala la kuweka vigezo mezani halafu tukaaanza kupitia kimoja baada ya kingine na hatimaye atabakia mmoja ambaye huyo wanachama watasimama naye katika kampeni za kumuombea kura ili kupata ridhaa ya kuongoza nchi yetu kwa awamu nyingine.

Wanangu, naandika waraka huu uwafikie hapo mlipo na muweze kutafakari na kuwasaidia wajumbe wenu wa mkutano mkuu kumchagua kiongozi asiye na shaka kabisa na anayeweza kuandika kiurahisi kwa Watanzania hawa ambao wamechoka na ukali wa maisha ya leo.


Mimi na umri wangu huu nadiriki kusema kuing’oa CCM madarakani kunahitaji nguvu ya ziada, tena yenye hoja na mashiko, na kama mnakumbuka Julius pia alisema viache vije vyama vingi vya siasa ili CCM iweze kuimarika; na kuimarika huko kutatokana na CCM kukabili hoja na ahadi zilizopo mbele na muafaka kwa wakati huo.


Vyama vingi vya siasa vitaona upungufu ulioko ndani ya chama tawala na vitasema kama sehemu ya sera zao na kama CCM wakifanya makosa ya kudharau kile ambacho kimeonwa na vyama vingine vya siasa basi ndiyo mwisho wa CCM kushika dola.


Wanangu, Mwenyekiti wa CCM amesema pale Kizota juu ya kutekeleza ahadi za chama chao. Amewaeleza wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Nane nini wafanye ili kukabiliana na hali halisi iliyopo sasa. Anahitaji msaada wa wasaidizi wake katika kupambana na ukali wa maisha kwa wapiga kura ili watakaporudi tena kuomba kura kwa wananchi kusiwe na pingamizi.


Wasiwasi wangu ni kwamba maneno ya Mwenyekiti wao huenda baadhi ya wajumbe hawakuyaelewa. Hawakuyaelewa kwa maana ya kumsaidia kutafuta kura kwa kutoa msaada kwake kupigania maendeleo na vita juu ya rushwa. Baadhi wamebweteka katika makundi wakisubiri awamu ijayo waingie madarakani kuiongoza dola.


Mimi kama mzee ningependa Mwenyekiti atahadharishe wazi kuwa iwapo wajumbe watafanya tofauti na anavyotarajia, basi wasishangae kuona wanayaacha madaraka ya dola kwa chama kingine ambacho kinapigania kuingia madarakani kwa hoja na sera ambazo hazijatekelezwa na chama chao.


Wanangu, sasa namjua rais ajaye hii ndiyo hoja yangu ya msingi siku zijazo naweza kumtaja. Namjua kama mtu asiye wa makundi na ninamjua kama mkataa rushwa na asiyetoa wala kupokea, namjua kama rais atakayelazimishwa kuchukua fomu na siyo anayelazimisha kuchukua fomu, namjua kama mzalendo mwenye uchungu na hali ya Watanzania anayeona kero na umasikini wetu na dhuluma tunayofanyiwa.


Wanangu, naikumbuka Tanganyika tuliyokuwa nayo sisi wakati wa Mjerumani na siyo Mwingereza , Tanganyika yenye ramani ya madini yenye shule nyingi za seminari, na yenye kujenga miundombinu ya kizamani. Ni Tanganyika ile ambayo tuliishi peponi japo tulikuwa chini ya mkoloni. Ningeipenda Tanganyika ile irudi iwe Tanganyika ya leo tena ambayo tuko huru, tukimiliki madini yetu, shule zetu na tukila kwa pamoja na kusaza; na masazo yawe yetu sote.


Chama Cha Mapinduzi mmefanya demokrasia ambayo pia mmejua kuwa mlikuwa na demokrasia ya rushwa ndani ya chama. Nashauri kama mzee wenu waacheni wala rushwa na watoa rushwa msafishe chama mapema kabla jua halijazama. Mkifanya hivyo vyama vingine vitawasindikiza katika uchaguzi, pasi na hivyo nyinyi mtageuka kuwa wasindikizaji katika uchaguzi ujao.


Wana wangu, nawapenda sana na hasa wanaTANU wenzangu ambao mmebahatika kulipia uanachama wa CCM. Mimi nimeshindwa kutokana na ukali wa maisha.

 

Wasalaam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo

By Jamhuri