Nilikuwa nimekaa natafakari katika kipindi hiki chote cha maisha yangu, ni lini naweza nikajitoa kwa ajili ya Taifa langu, lakini pia nikajiuliza nitaanzia wapi?

Baada ya kuangalia maandiko mbalimbali, nikagundua kuwa naweza kuwa mgombea binafsi, sheria nitakayotumia ni ile ya Mwalimu ambayo alisema naomba nimnukuu:

 

“… Nataka kusema kauli ya mwisho kuhusu sheria ya uchaguzi ilivyo sasa hivi.  Ninalo tatizo moja.  Hili nataka kulisema kwa sababu nadhani ni la msingi kidogo.

“Tulipokubali tuwe na vyama vingi vya siasa tulisema kwamba hivi vyama vingi vina migogoro.  Mnaweza mkawa na chama cha dini, kabila, mkoa kinaitwa Zanzibar au Tanganyika tu.

 

“Tulisema sisi hapana ni Taifa changa.  Lazima tujihadhari na chama kinachoweza kutugawa.  Tunataka chama kinachokubali umoja. Kwa hiyo, tukakataa vyama vya udini, ukabila na vya kutenganisha Tanzania.  Tanzania tukaigawa, sijui inaitwa Tanganyika na Zanzibar. Hapana tukatae vyama vya namna hiyo.

“Kwa hiyo, tuliamua kwamba yawepo masharti ya kisheria yanayozuia vyama kuwa vya namna hiyo.  Hii ni kulinda umoja ili tujenge upya kwa kuwa bado tu wachanga mno. Basi, sheria hiyo ndivyo ilivyotungwa na ndivyo ilivyo.  Huwezi kuanzisha chama ambacho kinakiuka upande huo wa sheria.  Hata hivyo, mimi nadhani sheria imekosea kuzuia wagombea binafsi.

“Nataka nieleze sababu kwa nini nadhani kukosea huku ni kwa msingi na si kwa juu juu.  Hili jambo lililokosewa ni la msingi.

“Ndiyo maana napenda kulisema kwa nini ni la msingi. Linahusu haki yangu na yako ya kupiga kura. Hii ni haki ya uraia. Madhali wewe ni raia wa Tanzania [huna kichaa, huko gerezani, umetimiza umri unaotakiwa wa miaka kumi na minane] una haki ya kupiga kura. Ni haki yako ya uraia. Iko mfukoni mwaka! Hii haki ya kuomba upigiwe kura pia ni haki ya uraia; ni haki yako.

“Unaomba ubunge au chochote kile upigiwe kura na hata unaomba urais, ni haki yako ya uraia; huwezi kunyimwa maadam wewe ni raia wa Tanzania, kisiasa una haki ya kuomba uwe rais.

Ukiwa katika chama ama hupo katika chama.  Unayo haki inayotokana na uraia wako ya kupiga kura na ya kupigiwa kura ambayo haiwezi kudaiwa na mtu ambaye si raia wa Tanzania.

“Aidha, raia wa Tanzania hawezi akanyang’anywa haki hii ya kuomba uongozi wa nchi yake tangu ngazi ya kijiji mpaka ngazi ya Taifa. Iwapo wapo wasio na uwezo huo wa kutaka kuwa rais, hiyo ni shauri nyingine.

“Lakini haki ninayo watakaohukumu kama nina uwezo au sina uwezo ni wananchi. Mimi sasa hivi niko hapa nawaelezeni jinsi ya kuwahukumu wenye uwezo na wasio na uwezo.

“Lakini sisemi hawana haki. Haki hiyo ndiyo inayowafanya ninyi wafanyakazi, ninyi wafanyakazi mnazo haki za wafanyakazi, nikasema “lakini mmoja mmoja hatuwezi, lazima tushirikiane.

Kwa hiyo, mnashirikiana wote kwa pamoja. Hivyo ni zivuri zaidi.

“Tunasema ni vizuri tuiombe na tujaribu kuitumia haki ile ya kuunda vyama. Mnaweza mkaunda vyama. Sijui wangapi wameweza kuingia katika vyama maana tunayo haki hiyo. Hivi sasa mnasema viko kumi na vitatu. Sina hakika kama vimechukua Watanzania wote.

“Watanzania wengine hawamo CCM, hawapo wapi na hawana chama chochote. Hata hivyo, nikikataa kuingia katika chama isiwe sababu ya kuninyang’anya haki yangu ya kupiga na kupigiwa kura. Ninayo tu na naweza nikaamua kuitumia mwenyewe tu!

“Lakini, msije mkanielewa vibaya kuhusu kile ninachotaka kusema kwamba raia yeyote wa Tanzania anaweza kusema ‘mimi mgombea urais’.  Tutamwambia: ‘Ah! Unaweza bwana peke yako, kweli utasimama hivi kwa Tanzania peke yako utapitapita huku na kule watakupigia kura?’

 

Unaweza kumlaumu na kumhukumu useme: Wewe ni mjinga. Lakini huwezi kusema huna haki hiyo. Ni haki yake.  Anaweza kuwa mjinga.  Labda kuwa ni mtu anayedhani kwamba “Watanzania wakishaona uso wangu, hata kama sina kitu, watanichagua. Anaweza kuwa si mgombea makini, lakini ni haki yake” mwisho wa kumnukuu.

Sasa naomba niitumie haki yangu katika uchaguzi wa 2015 kuutaka urais ili niweze kutatua yale ambayo naona wengi wetu yanatuhusu. Hakuna anayejua raha ya kukuna chawa kama hana, sisi maskini ndiyo tunaojua uchungu wa maisha yetu.

Wasalaam,

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri