Yah: Tanzania ilikuwa nyumba ya amani Afrika

Nimekumbuka kuna siku nilisikia kwamba vita ya uchumi sasa hivi ni kubwa na inapiganwa sana duniani baina ya nchi na nchi, vita hii ina lengo la kumiliki njia za uchumi kwa mataifa mbalimbali ili kuweza kuendelea kwa mataifa machache na mengine kubaki maskini, dhana hiyo haikumaanisha vita dhidi ya uhai wa watoto ambayo taifa letu limejikita.

Nimeshawishika kuandika waraka huu hivi sasa kwa sababu bado nina kumbukumbu ya kauli za viongozi na matokeo yake chanya. Kuna wakati kiongozi mmoja mkubwa wa taifa hili aliwahi kusema, nanukuu: “Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe.” Kilichotokea baada ya hapo ni vijana kudhani kupora na kuiba ni matokeo ya nguvu zao za kufanya uhalifu.

Sina sababu ya salamu, kwa hofu kwamba huenda ninaowatakia salamu za heri miongoni mwao ni hao wahalifu ambao wametibua nyongo za watu wengi na wengine kuwaliza, kitendo cha kupoteza maisha ya watoto kwa imani za kishirikina hakiwezi kuungwa mkono kwa kigezo cha vita dhidi ya uchumi wa wajinga wachache ambao mara zote huwa hawafanikiwi.

Hakuna utajiri ambao una nasaba na damu ya mtu, dhambi kubwa kama hiyo haitakuacha salama na wala haitakufanya ujione tajiri mwenye amani kamwe katika maisha yako, kufanya kazi kwa bidii ndio mwanzo wa mafanikio ya kila jambo, hauwezi kukaa bila kufanya kazi na ukaamua kumwaga damu ya viumbe vitakatifu, tena malaika, vya Mwenyezi Mungu na ukafanikiwa, never on earth!

Nianze kwa kutoa shukurani kwa baadhi ya viongozi na watendaji ambao wamefika eneo la tukio na kuchukua hatua, nawaamini sana watendaji wetu kwa uchunguzi, najua ni wapi huwa tunakosea lakini katika hili nawaombeni sana wahusika wote waliotajwa watafutwe na wakamatwe, kusiwepo namna ya kusingizia wala kuingia katika mitego ya kujipatia fedha kwa kusingizia, hii ni dhambi kubwa na itawatesa sana watu wengi.

Dhana ya vita ya kiuchumi nimeielezea hapo juu, kwamba mtu mmoja mmoja tena kwa kumuogopa Mungu apigane na ardhi yake ili apate mazao, apambane na mifugo yake ili apate uzao wa mifugo, achangamke na biashara yake ili aweze kuwa na akiba ya kipato chake, hizo ndizo njia pekee ambazo mtu anaweza kujikwamua kama taifa binafsi katika uchumi wake, hakuna njia ya mkato wala ya kishirikina katika kufanikiwa.

Tanzania ya zamani enzi tukipata uhuru nadhani ilikuwa ni pepo kwa baadhi ya maitaifa mengine ambayo yalimwaga damu kupata uhuru wake au hayakumwaga damu kutokana na misimamo ambayo ilijengwa nchini Tanzania na kufanikisha uhuru wao.

Kwa ufupi Tanzania ilikuwa sebule nzuri yenye amani kwa baadhi ya mataifa mengine yaliyotuzunguka na yaliyo mbali nasi, Tanzania ile iko wapi?

Ilikuwa ni Tanzania yenye utu na ubinadamu, Tanzania ya kumuona Mwafrika mwenzako kuwa ni ndugu, nchi ambayo tuliweza kuomba maji kunywa mahali popote bila kuwa na woga au nongwa, nchi ambayo tuliweza kuomba kulala nyumba yoyote lilipoingia giza bila hofu yoyote.

Kula chakula kwa mtu yeyote bila kuzingatia jinsia na anayekupatia mahitaji unayohitaji na kama watoto tuliweza kwenda kucheza mahali popote kwa raha na amani miyoni mwetu bila kuhofia au kuwa na hisia zozote za ubaya, hiyo ndiyo Tanzania niliyoishi mimi na wengine wa rika langu.

Ulikuwepo undugu wa Mtanzania kwa Mtanzania, haukuwepo uadui, tulishikamana, adui yetu mkubwa alikuwa Ujinga, Maradhi na Umaskini, katu hakuwahi kuwa binadamu mwenzetu. Huo ubinadamu na utu umepotelea wapi?

Hivi turudishe kujuana kwa kutumia barua za mabalozi na kadi za chama dunia ya leo? Haya ndiyo maendeleo ambayo sisi watu wa zamani tuliopitwa na wakati tunapaswa kuchekwa kwa ujinga wetu? Hivi ni kipi kinatuponza kizazi hiki cha mitandao? Au ingekuwa bora wazazi wenu wachinjwe ili msizaliwe?

Naandika barua hii nikitaka kujua ni kweli Watanzania mumekuwa maadui kiasi hiki? Kumbukeni Tanzania ilikuwa nyumba ya amani ya Afrika, kila mtu alikimbilia hapa na sisi tulililinda taifa letu kwa uzalendo uliotukuka, nyie mnatupeleka wapi na hizo teknolojia za Ujinga, Maradhi na Umaskini?

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.