Barua zangu kadhaa zilizopita nimekuwa nikijadili sifa na vigezo vya kiongozi ajaye na ambaye tunadhani anafaa kushika madaraka kwa Awamu ya Tano ya utawala. Nimetoa sifa ambazo kiongozi wa namna hiyo yupo japokuwa wengine watasema hayupo, lakini yupo tu lazima tukubali.

Hizi siku za karibuni katika mitandao ya jamii kumeibuka kaida ya vijana kurekodi sauti zao na kutumika kuielimisha jamii juu ya kiongozi bora na asiyefaa, nimeita kaida kwa sababu kutumika mahali ambapo hujui kama unatumika ni kama ajua, ajua ambayo sisi zamani ilikuwa haina ubishi — liwe suala la maana au la kijinga tunafanya bila kujiuliza.

Baadhi yao wametumika kuchafua wengine, lakini wenye akili timamu wanajua tu kwamba hiyo ni ajua kwa vibaraka wanaotumwa na wenye akili fupi kama wao, si kipindi cha kutajana majina ni kipindi cha kusikiliza maneno na minong’ono ya wenye nchi wanasemaje, suala la uongozi si la chama ni la nchi, ni lazima kusikiliza wenye nchi wanasemaje.

Sasa hivi kumeibuka kundi la viongozi kada ya kati ambao kazi yao ni kunukuu falsafa za viongozi wa zamani na kujiona ni wanasiasa wazuri kwa hoja zao ambazo hazitekelezeki, wanakurupuka na maneno mazuri kutoka katika vitabu vitakatifu wakijifanya watakatifu na kwamba wanataka mabadiliko yoyote kwa hoja zao.

Kwangu mimi hilo linanipa taabu, nauona uanasiasa huo ni kapuku, ni siasa chafu yenye lengo chafu kwa kuwa kiongozi bora hutoa mfano na si kusikiliza na kuigiza kile kilichofanywa na kiongozi mwingine, utakuwa kiongozi wa copy and paste.

Siasa ni vitendo, siasa ni uchumi, siasa ni kila kitu,  siasa siyo blabla na siasa siyo mahali pa kujificha kwa maovu au mema, siasa ni kazi na siasa ni uongozi, huwezi kuwa mwanasiasa ambaye kazi yake ni kuiga yote yaliyoko katika siasa, siasa ni ubunifu na siasa siyo kusutana, siasa ni utekelezaji.

Viongozi hawa, wengi wao kutaka kujipatia umaarufu kwa wananchi, wamekuwa wajuzi wa kutafuta kauli ambazo zilisemwa na wenzao na zikatekelezeka, wao hawana ubunifu na hawana kitu cha kutekeleza, wapo kuangalia upungufu ambao umejitokeza na wamejisahau kuwa kazi yao ni kutekeleza ni kuongoza, ni vitendo na wao ni kila kitu.

Imekuwa siasa ya maji taka, siasa kama tungo ya muziki mmoja ambao kila mtu anaimba, siasa ya ajua, siasa ya kusema bila kutekeleza siasa ya kuwasemea waliosema maneno mazuri yenye tija kwa maendeleo ya Taifa letu.

Kwa hoja hii bado narudia hoja ya kiongozi wa  Awamu ya Tano kuwa anapaswa kuwa vipi, kiongozi ambaye atatoka katika kundi la kuacha kudesa na kuibua hoja na kuzitendea kazi, nchi yetu inatakiwa itendewe haki katika mambo makuu manne — afya, elimu, uongozi bora na siasa safi.

Najisikia kinyaa kumuona mtu akiigiza maneno matamu ya viongozi wazuri, viongozi ambao walikuwa ni wale wa vitendo, tunapozungumzia afya watuoneshe kuwa wanakerwa na wanajua wanachokiongelea badala ya kukaa mahali na kuomba data ili wazizungumze katika kadamnasi na kujifanya zinawakera huku wakijua fika kuwa panga lenye makali wameshika mpini wake.

Ningependa kuacha kujisikia vibaya kumuona mwanasiasa anayesimama  na kuilaumu Serikali kwa kushindwa kusimamia suala la elimu, wakati mzungumzaji anatakiwa aishauri na kutekeleza majukumu yake kama kiongozi kwa wakati huo. Nakerwa na hali hiyo.

Huwezi kuzungumzia elimu kama mtoto wa kufikia, unatakiwa uoneshe mfano kwa kila kinachowezekana, jenga shule, toa mafunzo kwa walimu, imarisha miundombinu japo ya shule moja ili wengine nao wapate kusema kile ambacho umekifanya. Huo ndiyo uanasiasa, badala ya huu uanasiasa wa kukaa mbele ya televisheni na kuanza kuwasema watu wengine, hiyo ni mipasho, karekodi ili uuze.

Hivi sasa Taifa linaelekea katika makabidhiano ya Serikali ya awamu moja kwenda nyingine, tuache unafiki na kutumiwa, tuache kununuliwa, tuache kunukuu maneno yenye hadhi kuliko sisi. Kama umeshindwa kutekeleza yako usitafute mchawi kwa kuwasemea wengine.

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri