Wanangu poleni na uchovu wa mawazo. Sitaki kuwapa kongole ya kazi kwa sababu naomba nikiri wazi kuwa nyote ni wababaishaji na hamna lolote mnalofanya zaidi ya kuungaunnga kile tulichokifanya sisi kwa ujana wetu.

Naomba nichukue fursa hii kuwapongeza vijana wenzangu wa zamani kwa kazi nzuri mliyofanya hadi tukafikia hapa tulipo leo.


Sina nia mbaya ya kuwatukana, la hasha, ila ukweli mnaujua ninyi  mlioguswa na kauli yangu ya kuwaponda ninyi mnaojiita kizazi kipya na mambo yenu ya kisanii kila siku. Mnaacha kufanya mambo ya ukweli mnataka mambo ya kuigiza na ndoto za Alinacha.


Wanangu leo yawezekana nikawa sina kauli nzuri sana, lakini hii inatokana na kile kilichonigusa moyoni mwangu, kama Mtanganyika halisi nisiyetaka uongo katika kutekeleza majukumu ya msingi katika kuliendeleza taifa hili, lililo na ugonjwa wa kutotaka maendeleo miaka yote na awamu zote.


Wanangu kama mtakumbuka tulipata uhuru miaka karibu 50 iliyopita na hivi juzi nakumbuka mmefanya sherehe kubwa ya kuadhimisha miaka hiyo 50 ya uhuru. Mimi na wazee wenzangu tulikuwa tunajiuliza, mnashangilia nini hasa mnachoweza kujivunia kama jambo muhimu sana mlilolifanya kwa kipindi hicho.


Siku zote nadhani nimekuwa mjinga kuhoji mambo ya kizamani kwa akili yangu niliyodhani labda bado yalikuwa na thamani kwa maendeleo yetu ya sasa, na kwamba kwa fikra zangu huenda hayo ndiyo yaliyotufikisha hapa tulipoinua mikono juu na kutembea kifua mbele, na kujisifu kuwa tumeendelea na tunapaswa kufanya sherehe nzito kwa gharama yoyote.

 

Wanangu baada ya Uhuru na miaka michache ya kulisogelea Azimio la Arusha, tulikuwa na usemi wa Kiingereza ambao kwa hakika hata ngumbaru ilikuwa haijaanza, lakini hata mtawaliwa wa huku Maneromango alikuwa anajua maana ya “the big four”.

The big four ilikuwa na ufahari wa kilimo. Nadhani kilimo hicho kamwe hakiwezi kukaribiana kwa dhana tu na hiki kilimo chenu cha kisasa chenye kaulimbiu ya Kilimo Kwanza. The big four ilikuwa ni mikoa halisi ya kilimo – mikoa minne iliyoweza kulisha Taifa hili na masalia yakapelekwa kuuzwa nje kwa faida ya Serikali yetu ya kizamani.


Pamoja na umaskini tuliokuwa nao, lakini tuliweza kuyasaidia mataifa yaliyokumbwa na wimbi au janga la njaa. Tulikuwa na fahari kutoa na si kuomba kama ilivyo leo, tuliwasaidia majirani zetu chakula, tuliwapa chakula wageni wetu kutoka Afrika Kusini waliokuwa katika mafunzo ya kwenda kudai uhuru wao nk.


Kamwe hawakulala na njaa katika ardhi yetu labda huko kwao. Chama cha ukombozi cha Namibia (SWAPO) nao walipewa chakula na wakashiba wakajenga mazingira mazuri ya kwenda kudai kilicho halali katika taifa lao yaani uhuru, na baada ya uhuru wakarejea kutoa shukurani. Sisi tulitembea kifua mbele tukijiona watoa misaada kama yalivyo mataifa mengine yaliyoendelea na kutusaidia.


Wanangu naamini mna akili timamu na mnaona jinsi vile mataifa yanayotupatia msaada yanavyotunyanyasa leo kwa misaada yao. Tunageuzwa kuwa watumwa wa “ndiyo mzee” hata kwa jambo dogo ambalo tungeamua kwa moyo wa dhati kabisa tungeweza kulifanya.

 

Tanganyika ninayoijua mimi kwa  kasi tuliyokuwa tukiifanya kwa maendeleo, hatukuwa watu wa kuomba neti za mbu, hatukuwa na watu wa kuomba dawa za kutibu malaria, kuagiza mbolea, kuleta maduka makubwa tena kutoka kwa watu tulioamini ni makaburu na kuyazika maduka yetu ya asili, yaani ya ushirika.


The big four ilikuwa mahususi kwa kilimo cha mazao ya chakula, na tulikuwa tukijiona fahari kutembea kifua mbele kwa wenzetu waliokuwa na sifa nyingine za kimaendeleo. Mathalani, ilikuwa vigumu kumtambia Msukuma aliyekuwa na sifa ya kuzalisha pamba kwa wingi na kuuza nje baada ya viwanda vyetu vyote vinane kushindwa kuhimili mavuno ya pamba.


Wanangu the big four zilikuwa nyingi sana. Zilikuwapo za kilimo cha mazao ya biashara, uvuvi, ufugaji nakadhalika. Pia zilikuwapo the big four za viwanda kama Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza na Mbeya.


Zilikuwapo the big four za utalii ambao leo kwa bahati nzuri kama ingelikuwa ni enzi zetu, nadhani zingekuwa nyingi zaidi tofauti na hali ilivyo leo. Kausemi ka the big four kalikuwa na nguvu ya ushindani na kuleta maendeleo ambayo yamewafanya wanangu na wajukuu zangu mshangilie miaka 50 ya Uhuru kwa kigezo cha kupiga hatua za kimaendeleo.


Wanangu kinachonikera babu yenu, ni jinsi mnavyoshindwa kubuni mambo yenu kwa awamu yenu na kuyaendeleza kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho, badala ya kuua yale tuliyoasisi wazee kwa akili zetu ndogo zilizotoka kwa wakoloni.


Tuliyobuni ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea mmeyatupa, the big four imegeuka kuwa the big poor, na hayo ndiyo maendeleo nadhani mnayotaka. Mmegeuza siasa yetu kuwa ya kibepari, msimamo wa chetu haupo tena ni msimamo wa chao na familia zao tu.


Wanangu tuliandaa mazingira mazuri ya sote kuota moto wa maendeleo,  hatukubagua wachache waote moto huo na wengine wakae pembeni kuendelea kupata baridi. Tulitaka nyote mpate elimu kwa nguvu ya serikali yenu na siyo nguvu ya mmoja mmoja. Tulitaka nyote kwa nguvu ileile mpate huduma ya afya na si wachache wapate huduma hiyo nje ya nchi na wengi wakose huduma hiyo ndani ya nchi.


Kutokana na kutudharau, kutupa tuliyoasisi kwa nia njema, sasa Watanganyika wenzetu mnapata adha ya ukoloni wa uwekezaji. Mmegeuziwa the big four katika madini, wawekezaji wanachimba na kuyauza nje bila idhini yenu. Tena mnadharauliwa, mnatukanwa, mnanyanyaswa ndani ya aridhi yenu na siku moja mtauzwa kama wanyama kama hamtarejea katika ile imani ya kijinga kwamba mali iliyopo Tanzania ni yetu sote na si ya wachache wanaojiona ni wateule wa kuitumia bila idhini ya wengi.


Wakati wetu kiongozi alikuwa na wajibu wa kujibu amefanya kwa niaba ya nani na kwa faida ya nani. Hatukuwa na vyombo vya kuchunguza rushwa bali sote tulikuwa chombo cha kuchunguza rushwa, tuliamini mlinzi wa nchi ni mwananchi mwenyewe.


Wanangu sitaki kuamini baada ya kuwawezesha kupata elimu mmeamua kuitumia elimu yenu katika siasa inayozidi kutufilisi. Wanaotufilisi kuua the big four mnawajua, na ajira yao iko mikononi mwenu kwa kupiga kura lakini kila siku mnalalamika kama mimi niliyechoka na pengine nisijue siku ya kupiga kura ni lini!


Yawezekana kuna big four nyingine lakini the big four ninayoijua ni the big poor leo, wanaohusika kwa kushirikiana na viongozi wa biashara, kilimo, viwanda, uwekezaji, mifugo na sera wanapaswa kutujibu dhamana yao ni ipi, na tuwafanye nini tuweze kurudisha heshima ya nchi yetu. Ilikuwa ikitoa misaada na si kupokea misaada tena kwa masimango.

 

Wanangu chonde chonde, kumbukeni tumefanya nini kwa faida yenu na ninyi mjiulize mnafanya nini kwa faida ya wanenu, kuna siku mtaulizwa kama si ninyi basi makaburi yenu – mliifanyia nini Tanzania ya wenyewe.

Wasaalam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.


By Jamhuri