Sasa ni miaka kama kumi hivi tangu Serikali ilipotangaza ajira za vijana wapigakura na wenye uchu na maisha bora kama nafasi milioni moja, katika ajira hizo bila kufanya utafiti wa kina naweza nikasema robo tatu ya ajira hizo ni udereva wa pikipiki.

Nashukuru kuwa vile vijiwe vya vijana kukaa na kupiga story vimekwisha ila vijiwe vile vimehamia katika hospitali zetu baada ya ajira kuwatenda wao au kuwatenda waliovamia ajira zao, yaani wapanda bodaboda.

Leo nimekumbuka jambo hili baada ya kukumbuka enzi zetu za kilimo cha kisasa na ajira za vijana, nimekumbuka baada ya kuona mikasa mingi ambayo leo inawakumba vijana ambao wanajiita Taifa la kesho. Najua kuwa vijana wengi wanachukia suala la kilimo na hasa katika kipindi hiki, kipindi ambacho suala la utandawazi na maisha ya kushika kalamu yanatosha kushiba na kuweka akiba. Kwa kigezo hicho peke yake utawala wa kutafuta ajira milioni moja haujapata taabu kuwaridhisha kwa biashara ya bodaboda.

Nikipita mitaani napata hadithi nyingi za mafanikio ya kazi za haraka haraka, naambiwa juu ya mafanikio ya bodaboda na wizi na huko wanakoita ‘kutoka kimaisha’. Napata taarifa za mafanikio ya kuwa ‘mapusha’ kwa maana ya kuuza dawa za kulevya. Pia napata taarifa za vijana kukwea pipa na kuwa container na kisha kutajirika baada ya kurejea nakuutema mzigo.

Haya ni mawazo ya vijana wetu wa leo, vijana ambao hawataki kujituma kwa kufanya kazi halali kwa maisha halali, vijana ambao wamekosa subira ya maisha kwa kuvumilia kulima na kuuza mazao yao. Haya yote nimeyafikiria kutokana na sera za sasa za kisiasa ambazo zina mipango dhaifu kwa maendeleo ya Taifa na mtu mmoja mmoja. Enzi za miaka yetu kuna wakati ambapo sera zilitulazimu kujituma na kuona maendeleo ya nchi ni wajibu wa kila raia wa nchi hii.

Nimeyaangalia maendeleo yetu binafsi, na athari binafsi ambazo zinagharimu maisha yetu na kizazi kijacho, nimeangalia nguvu ya uchumi kichele ambao hatupaswi kujivunia mahali popote kwa uwekezaji huu mdogo kwa nguvu kazi hii tuliyonayo. Wakati tunapata uhuru wa nchi yetu, baadhi ya nchi nyingi duniani zilikuwa maskini kama sisi, leo nchi hizo ni miongoni mwa nchi tajiri duniani baada ya kuwekeza katika kilimo na viwanda, suala ambalo hata sisi watu wa zamani kwa akili zetu zilizofungwa nje ya utandawazi, tulijua.

Sisi tuliwekeza katika kilimo na kutengeneza mazingira mazuri ya vyama vya ushirika, tuliwekeza katika viwanda ambavyo vilitoa ajira ya kutosha kwa vijana wa wakati ule, tulikuwa na viwanda kila mkoa na nchi nzima, viwanda ambavyo leo, mbali ya mahitaji ya bidhaa zake kuwa muhimu duniani, vimegeuka kuwa maghala ya bidhaa za matajiri wachache ambao siyo washirika wetu kiuchumi.

Naangalia ajira ambazo wakati wetu tuliziona kama ni uadui wa maendeleo, ajira ya biashara ndogondogo ambazo enzi zetu tuliona ni kazi za walemavu au wazee, leo zinafanywa na vijana shababi ambao wangeweza kuchukua jukumu la kazi nzito sanjari na nguvu zao. Matokeo ya ajira hizi nyepesi na hatari ambazo tumetayarishiwa na viongozi wetu wanaosimama majukwaani na kutangaza sera za maendeleo, ni matokeo ya kuzalisha ajira ya kuchimba makaburi, ajira ya vijana ombaomba, ajira za madaktari wengi kwa ajili ya kutoa tiba na mwishowe ajira ya kufanikisha usemi wa wazee Taifa la kesho.

Ningelipenda sana viongozi watafakari na kuona hatima ya Taifa na wananchi, wafikirie juu ya uzalendo wa kuwafundisha vijana umuhimu wa kufanya kazi halali, badala ya kuwa na mateja na wauza unga wengi. Ningelipenda viongozi wanaotutawala wafikirie wimbi la vijana wezi ambao hawana namna nyingine yoyote ya kubadili mfumo wa maisha ya kujitegemea, na kujiuliza nini hatima ya kundi hilo kama siyo kuanzisha jeshi jipya la uporaji!

Ningelipenda viongozi wetu watupie macho katika hospitali mbalimbali na kuona kundi la vijana waliokatika miguu na mikono, kutokana na ajali za ajira mpya ya pikipiki na kisha wajiulize hayo ndiyo malengo yao mahususi?

Tumalizeni lakini kumbukeni wapiga kura wenu ni sisi na mna wakati mwingine wa kurudi kuomba kura. Msishangae kuona idadi yetu imepungua kutokana na sera au kushadadia kwenu ajira hizo, ajira zinazowamaliza watoto, vijana, wazazi, wazee na hatimaye viongozi wenyewe.

Wasaalam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

1099 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!